Kuna tabia moja muhimu sana mabayo watu wote waliofikia mafanikio makubwa wanayo. Tabia hii ndio imewezesha baadhi ya watu kuwa wanamuziki bora, wengine kuwa wachezaji bora na hata wengine kufikia mafanikio makubwa sana kwenye biashara na kazi.
Mwezi huu wa tisa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA tutajadili tabia hii moja muhimu sana ambayo bila ya kuwa nayo huwezi kujenga tabia nyingine unazohitaji ili kufanikiwa. Bila ya tabia hii utahangaika sana lakini utashindwa kupata majibu unayotarajia.
Tabia hii ni NIDHAMU BINAFSI.
Kwa jumanne tano tulizonazo mwezi huu wa tisa tutakwenda kujifunza yote ya msingi kuhusiana na tabia ya nidhamu binafsi. Mambo tutakayoyazungumzia kwa mfuatano ni;
1. Maana ya nidhamu binafsi.
2. Umuhimu na faida za nidhamu binafsi.
2. Jinsi ya kujenga nidhamu binafsi.
3. Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuendelea kuwa na nidhamu binafsi.
5. Uhusiano wa nidhamu binafsi na mafanikio makubwa.
Jumanne ya leo tutaanza na maana ya nidhamu binafsi. Jumanne zitakazofuata tutajifunza hayo mengine, mpaka kufikia mwisho wa mwezi huu utakuwa umeshajenga misingi imara ya kukuwezesha kuwa na nidhamu binafsi.
Nini maana ya nidhamu binafsi?
Nidhamu binafsi ni pale ambapo unaweza kujithibiti au kujitawala wewe mwenyewe.
Nidhamu binafsi ni pale unapoweza kujizuia kufanya mambo kwa kuendeshwa kwa hisia au tamaa.
Nidhamu binafsi ni pale ambapo unaweka malengo na mipango na kuweza kuifuata bila ya kutetereka au kubadilishwa na vitu vingine.
Tofauti na watu wengi wanavyoelewa nidhamu binafsi sio kujitesa, au kujinyima, bali ni tabia ambayo inakufanya uweze kujitawala zaidi.
Nidhamu binafsi ni uhuru.
Watu wengi wanaamini na kufikiri kwamba unapokuwa na nidhamu binafsi unakuwa hauko huru kufanya chochote unachotaka. Au unakuwa mtumwa wako mwenyewe au wa misingi uliyojiwekewa mwenyewe. Hii ni kinyume kabisa na maana ya nidhamu binafsi.
Nidhamu binafsi ndio itakayokuletea uhuru wa kweli. Unapoweza kujitawala na kuzuia kuendeshwa na hisia ndio unaweza kuwa huru na kuamua ufanye nini. Katika maisha huwezi kufanya chochote unachotaka hata kama ungekuwa nani au ungekuwa na uwezo mkubwa kiasi gani. Kila kitu kina kiwango na unapokuwa na nidhamu binafsi ndio unaweza kuheshimu viwango hivyo.
Kwa mfano hata uwe na fedha nyingi kiasi gani huwezi kuamua kula au kunywa kila kitu roho yako inapenda. Kwa kufanya hivi utakuwa unajitengeneza kuwa mtumwa wa ulevi na uteja na baadae kuishia kuwa na afya mbovu.
Ni lazima kila mtu kuwa na nidhamu binafsi.
Huwezi kufikia mafanikio yoyote kwenye maisha yako kama huna nidhamu binafsi. Nidhamu binafsi ndio itakufanya uweze kuweka na kufikia malengo makubwa. Nidhamu binafsi ndio itakufanya uweze kuvumilia hata pale mambo yanapokuwa magumu. Na nidhamu binafsi ndio itakuepusha na kufanya maamuzi yanayosukumwa na hisia.
Nidhamu binafsi ndio inayokuwezesha kufanya kile unachotaka kufanya badala ya kufanya kile unachojisikia kufanya.
Nidhamu binafsi ndio inayokuwezesha kupuuza raha ya muda mfupi ili uweze kufaidi furaha ya muda mrefu.
Ni lazima kwa wewe kuwa na nidhamu binafsi ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Tutajifunza zaidi kuhusu umuhimu wa nidhamu binafsi kwenye makala ijayo.
Jiunge ili kujifunza tabia hii muhimu.
Kama mpaka sasa bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA jiunge leo ili uweze kupata nafasi ya kujifunza tabia hii muhimu sana kwenye maisha yako. Gharama ya kupata mafunzo haya ya tabia za mafanikio na pia kupata makala za biashara na ujasiriamali ni tsh elfu kumi kwa mwaka. Kujiunga tuma tsh elfu kumi kwenye namba 0717396253/0755953887 na kisha bonyeza maandishi haya kujaza fomu ya kujiunga na uanachama wako utadhibitishwa.
Fanya hivyo leo hii ili usikose nafasi hii nzuri ya kujifunza na kuweza kufikia MAFANIKIO MAKUBWA.
Nakutakia kila la kheri katika kujenga tabia ya kuwa na nidhamu binafsi.
TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.