Kuwa mtu wa mafanikio au ili uweze kufanikiwa kwa kile unachofanya hauhitaji kuwa na bahati wala hauhitaji kuwa na digirii fulani au ujihusishe sana na nguvu za giza ndipo ufanikiwe. Unachohitaji ni kuwa na maarifa sahihi na kujua mambo  muhimu kwako  yatakayokuongoza kwenye mafanikio (Soma zaidi Hivi ndivyo unavyoweza kufikia viwango bora vya mafanikio, bila ya kutumia uchawi )
Mara nyingi watu wengi wanapata shida katika maisha kwa kukosa au kushindwa kufanyia kazi maarifa haya ambayo yapo, na ujifunza mara kwa mara kupitia AMKA MTANZANIA. Na kutokana na kukokujua maarifa haya muhimu unayotakiwa kuwa nayo ili kufanikiwa kwa kile unachokifanya wengi wamejikuta wakiwa ni watu wa kulalamika sana kwa sababu ya maisha kuwa magumu na kukosa pesa.
Jiulize, kwa nini uendelee kulalamika na kulaumu mambo yale yale kila siku, kwamba sina mtaji, oooh sikusoma sana wakati uwezo wa kuishi ukiwa na pesa nyingi unao. Ukichunguza na kufatilia kwa makini utagundua kuwa  hauhitaji kuwa na pesa nyingi kuweza kutimiza mipango na malengo uliyojiwekea. Kwani pesa sio tatizo la kweli sana katika maisha yako tatizo ni wewe mwenyewe ndio kikwazo cha mafanikio yako.
Ili ufanikiwe kwa kile unachofanya unahitaji  kujua vitu muhimu tu kwako ambavyo mwisho vitakuongoza kwenye mafanikio na kuwa huru kifedha. Vitu gani muhimu unavyotakiwa navyo ili kufanikiwa kwa kila unachokifanya?
Hivi ndivyo vitu muhimu unavyotakiwa kuwa navyo ili kufanikiwa kwa kile unachokifanya:-
1. Unahitaji kuwa na Muda.
Unahitaji kuwa na muda ili kufanikiwa kwa kile unachokifanya. Ni lazima utenge muda wa kufikia ndoto zako. Kama utakuwa unaweka malengo makubwa na unataka kuyafikia kwa muda mfupi , utakuwa unakosea sana na hii itasababisha ukatishwe tamaa kumbe muda uliojiwekea kufikia malengo yako ni mfupi.
Jiulize mwenyewe ni muda kiasi gani umetenga kufikia malengo yako uliyojiwekea? Muda ni muhimu sana ili kutimiza malengo yako. Kama unataka kufikia ndoto na malengo yako makubwa uliyojiwekea acha kupoteza muda wako kwa namna yoyote ile. Tumia muda wako vizuri na kumbuka muda ni kitu muhimu ili kufanikisha kile unachokifanya.
 
 
2 .  Unahitaji kuwa na  Wazo.
Mafanikio yoyote yale yanatokana na mawazo na sio pesa. Ni muhimu sana kuwa na wazo ili kufanikiwa kwa kile unachokifanya. Tatizo walilonalo wengi ni kutokuamini sana mawazo waliyonayo na kujikuta wanaamini mawazo ya watu wengine na kuyafanyia kazi.
Acha kujidharau wala kujishusha tumia wazo ulilonalo kukufanikisha. Una mawazo mazuri sana ambayo hujayaweka kwenye utendaji kwa asilimia zote. Kama una wazo la kuanzisha kitu fulani au biashara anzisha na acha tabia ile ya kuulizia ulizia sana. Chukua hatua ya kufanyia kazi mawazo mazuri uliyonayo na hakika utafanikiwa.

3.  Unahitaji kuchukua hatua kwa vitendo.

Ili uweze kufanikiwa kwa kile unachofanya hakikisha unafanyia kazi mawazo uliyonayo kwa vitendo. Chukua hatua hii muhimu kwako ya kufanyia kazi ndoto zako na usiishie kuwaza tu na kuongea sana hiyo haitakusaidia katika maisha yako. Tekeleza na fanyia kazi ndoto zako kila siku hata kama ni kwa sehemu ndogo lakini utakuwa ndio umesogea kuelekea kuzifikia ndoto na malengo yako. 
4.  Unahitaji kuwa na njaa kubwa ya mafanikio.
Moja ya kitu muhimu kitakachokusaidia kufikia ndoto zako kwa kasi na haraka ni njaa ya mafanikio unayoyataka. Huwezi kufanikiwa kama huna hamu na shauku kubwa ya kufanikiwa ndani mwako. Mafanikio uliyonayo au unayoyataka yanategemea kiu uliyonayo juu ya mafanikio hayo. Kiwango cha njaa au kiu uliyonayo ndicho kitakachosababisha ufanikiwe kwa kiwango fulani katika maisha yako.
Unapokuwa na njaa hii ya mafanikio au hasira kubwa ya mafanikio ndiyo itakayokufanya ufanye lolote linalowezekana mpaka ufanikiwe. Jiulize mwenyewe una hasira na njaa kiasi gani ili kuhakikisha unatimiza na kuyafikia malengo yako makubwa uliyojiwekea.
 5. Unahitaji kung’ang’ania sana ndoto zako.
Hakikisha katika maisha yako kisikuzuie kitu chochote kufikia ndoto na malengo yako makubwa ukiyojiwekea. Katika safari ya maisha tunapitia mambo mengi sana na kuna wakati unakuwa unahisi kama unataka kukata tamaa. Unapokutana na hali kama hii usikate tamaa endelea kung’ang’ania na kushikilia ndoto zako mpaka zitimie.
Kumbuka watu wengi wenye mafanikio hapa Duniani ni watu wa kunga’ang’ania ndoto zao mpaka kuzifikisha mwisho. Kama kweli una kiu ya kutaka kufanikiwa kwa kile unachokifanya jifunze kung’ang’ania ndoto zako mafanikiio utayaona.
Hivi ndivyo vitu muhimu unavyotakiwa kuwa navyo katika maisha yako ili kufanikiwa kwa kile unachofanya. Endelea kujifunza kila siku kupitia mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ili kujiwekea hazina bora ya maarifa itakayokupa ukombozi mkubwa wa maisha. Pia karibu sana katikaKISIMA CHA MAARIFA kwa kujifunza zaidi,  kumbuka mwezi huu wa tisa tunakuja na siku 30 za mafanikio.
Kwa kipindi hiki cha siku 30 utajifunza makala moja kila siku inayoeleza siri kubwa na muhimu ya wewe kufikia viwango bora vya mafanikio unayoyataka. Hakikisha usikose kutumia fursa hii kubwa itakayoleta mapinduzi makubwa katika maisha yako. ( kupata utaratibu kamili na jinsi ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuwasiliane kwa amakirita@gmail.com au 0717 396253 )
 Nakutakia ushindi mkubwa katika safari yako muhimu ya maisha iwe ya ushindi.
DAIMA TUKO PAMOJA!
IMANI NGWANGWALU- 0767048035/ingwangwalu@gmail.com