Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.

Mwaka 1990 rafiki yake Robert, Mike alichukua urithi wa mali za baba yake na kuendeleza yale mazuri ambayo baba yake alikuwa anayafanya. Aliweza kumlea vizuri Mike na hatimaye aliweza kuendeleza mali hizo vizuri na yeye na mke wake walikuwa matajiri wakubwa sana.

Mwaka 1994 Robert alistaafu akiwa na miaka 47, na mke wake alikuwa na miaka 37. Kustaafu hakumaanishi kutokufanya kazi. Kwa Robert na mke wake kunamaanisha kwamba kama wakifanya kazi au hata wasipofanya kazi bado mali zao zitaendelea kuzalisha na kukua zaidi. Kwao inamaanisha uhuru ambapo mali zao zinazalisha bila hata ya wao kuwepo moja kwa moja. Robert anafananisha kutengeneza mali zinazozalisha ili kustaafu mapema ni sawa na kupanda mti ambapo mwanzoni utaumwagilia maji ila baadae unakuwa na mizizi mirefu hivyo huna haja ya kumwagilia tena. Na wakati huo unaendelea kunufaika na kivuli kizuri au matunda yanayotokana na mti huo.

Robert anasema kila akizungumza na watu huwa wanamuuliza wafanye nini ili nao waweze kuwa na uhuru wa kifedha? Waanzie wapi? Je kuna kitabu kizuri wanaweza kusoma? Je ni siri gani inayoweza kuwapatia mafanikio?(nina hakika haya ni maswalia ambayo umekuwa unajiuliza muda mrefu).

Robert anawajibu maswali yote hayo kwa kutumia elimu aliyopatiwa na RICH DAD, kama unataka kuwa tajiri ni lazima uwe na elimu ya fedha(uelewa wa fedha). Wazo hili lilimuingia Robert kwenye kichwa chake na aliweza kulifanyia kazi.

Robert anasema kama unataka kujenga gorofa refu sana cha kwanza ni lazima uchimbe shimo refu sana na kuweka msingi imara. Kama unataka kujenga kibanda unaweka msingi kidogo tu. Anasema watu wengi kwenye kujenga utajiri wanajaribu kujenga ghorofa refu kwenye msingi mdogo. Anasema mfumo wa elimu haujaweka kipaumbele kwenye kufundisha watu maswala ya fedha na hivyo wanafuzni wanahitimu masomo bila ya kuwa na elimu hii muhimu.

Kutokana na kukosa elimu hii wanajikuta kwenye maisha magumu na madeni mengi na hivyo wanafikiria kitakachoweza kuwatoa hapo ni kutafuta njia ya kuwa tajiri haraka. Wanaanza kujenga ghorofa kubwa kwenye msingi mdogo. Baadae matatizo makubwa yanatokea na kujikuta wanarudi kule kule walikokuwa.

Robert anasema somo la hesabu za fedha(accounting) ni somo lisilopendwa na wengi ila ndio somo muhimu sana kwenye maisha. Swali ni je unawezaje kufundisha somo hili lisilopendwa kwa watu hasa kwa watoto? Jibu ni kwamba fanya iwe rahisi. Kwa mfano RICH DAD aliwafundisha Robert na Mike kwa njia rahisi sana akitumia picha na maneno na baadae mahesabu.

Robert anasema kama unataka kuwa tajiri kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kujua ni tofauti kati ya mali zinazozalisha(ASSETS) na mali zisizozalisha(LIABILITIES) na ukishajua hivi uanze kununua assets na uache kununua liabilities. Hii ndio sheria ya kwanza ya kuelekea kwenye utajiri. Inaonekana ni sheria rahisi ila watu wengi wanashindwa kuitekeleza. Watu wengi wanateseka na fedha kwa sababu hawajui tofauti kati ya mali zinazozalisha na mali zisizozalisha.

Watu matajiri wananunua mali zinazozalisha(assets) ila watu masikini wnanunua mali zisizozalisha(liabilities) ila wanafikiri wamenunua assets. Hii ni kwa sababu hawajui tofauti hizo mbili.

Je ni nini tofauti kati ya ASSETS na LIABILITIES.

Rich dad aliwafundisha vijana hawa wawili kwa lugha rahisi sana tofauti kati ya assets na liabilities.

ASSETS(mali zinazozalisha) ni mali yoyote ambayo inaingiza fedha kwenye mfuko wako. Kwa mfano nyumba ya kupangisha, gari la biashara, biashara au shamba linalozalisha.

LIABILITY(mali zisizozalisha) ni mali yoyote ambayo inatoa fedha kwenye mfuko wako. Yaani wewe unatoa fedha na kuweka kwenye mali hiyo. Kwa mfano gari ya kutembelea, nyumba ya kuishi na vitu vingine vya kifahari.

Nina halika kwa hapa tu umeshaanza kuchanganyikiwa, hasa unaposikia kwamba nyumba yako unayoishi ni liability wakati ukienda benki wanakuambia ni asset. Ni kweli ni asset kwa benki ila ni liability kwako. Nyumbaunayoishi unailipia gharama mbalimbali ila hakuna fedha yoyote unayoipata moja kwa moja kutoka kwenye nyumba hiyo. Hivyo hivyo kwa gari ya kutembelea.

Robert anasema kama unataka kuwa tajiri nunua ASSETS na kama unataka kuwa masikini nunua LIABILITIES. Anasema watu masikini sio kwamba hawapati fedha ila wanatumia fedha zao kununua mali zisizozalisha.

Rich dad aliwafundisha kwa michoro hii miwili.

Mchoro wa kwanza unaonesha mzunguko wa fedha wa mtu masikini. Anapata kipato ila kinakwenda kwenye matumizi(expenses) hivyo kinaisha na anasubiri kipato kingine.

poor financial

Mchoro wa pili unaonesha mzunguko wa fedha wa mtu tajiri ambapo fedha inatoka kwenye mapato na kwenda moja kwa moja kwenye kununua mali inayozalisha na baadae kupata kipato zaidi ambacho anatumia kwenye matumizi ya kawaida na pia kununua mali nyingine inayozalisha.

rich financial

Hii ndio tofauti kubwa kati ya tajiri na masikini, hata kama wataanza na kipato sawa, baada ya muda tajiri atakuwa na mali nyingi wakati masikini atakuwa bado anateseka na fedha.

Tofauti kubwa kati ya tajiri na masikini ni jinsi gani wanatumia fedha zao baada ya kuzipata.

Mtu ambaye hajajifunza elimu hii hata akipewa fedha nyingi kiasi gani bado ataendelea kuwa na matatizo ya fedha. Kwa sababu fedha zitakavyoongezeka ndivyo matumizi yanavyoongezeka. Hii ndio sababu kubwa watu wanaopata fedha nyingi kwa wakati mmoja kama urithi, mafao, kushinda bahati na sibu au kupewa zawadi kazini huwa wanarudi kwenye matatizo yao ya fedha muda mfupi. Wakati mwngine hujikuta kwenye hali baya zaidi ya hata walivyokuwa hawajapata fedha hizo.

Tunajifunza nini hapa?

Kuna mengi ya kujifunza katika sehemu hii ya uchambuzi;

1. Ni muhimu kuwa na elimu ya fedha ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha.

2. Tofauti ya tajiri na masikini sio kwenye fedha wanazopata ila kwenye matumizi ya fedha wanazopata.

3. Ni muhimu kujua tofauti kati ya ASSETS na LIABILITIES.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.