Kuna nguvu moja inayokuwezesha kufanikiwa na kupata chochote unachotaka. Nguvu hii inaweza kushinda vikwazo, changamoto na hata kushindwa.
Nguvu hii ni NGUVU YA KUAMINI.
Bila nguvu ya kuamini una uhakika wa kushindwa kwenye jambo lolote unalofanya. Kwa kuwa nayo kufanikiwa ni uhakika.
Nguvu ya kuamini inaweza kukupatia mambo haya matatu;
1. Inaweza kukufanya uwe vile unavyotaka kuwa. Vile ulivyo inasaidia kile utakachopata.
2. Inakuwezasha kuweza kufanya kile unachotaka kufanya. Kile unachofanya kinasaidia kufikia kile unachotaka.
3. Inakuwezesha kupata chochote unachotaka kuwa nacho. Kama unaamini utapata.
Nguvu ya imani ndio msingi wa dini zote duniani. “yote yanawezekana kwa wale waaminio” huu ni mstari unaotumika sana kwenye dini mbalimbali.
Hii ndio nguvu ya ulumwengu iliyopo mikononi mwako;
Unaweza kuwa vile unavyotaka kuwa, unaweza kupata chochote unachotaka kupata na unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya kama utaamini kwamba unaweza.
Watu wote maarufu na mashuhuri waliofanya mambo makubwa duniani walikuwa wanaamini sana kwenye uwezo wao wa kuleta mabadiliko. Wanasayansi wamedhibitisha kwamba chochote ambacho ubongo wa binadamu unaweza kufikiri na kuamini basi anaweza kukipata.
Kama una kiu sana ya kupata kile unachotaka kupata na ukawa na imani kwamba unaweza kukipata ni lazima utakipata. Kama unataka kuwa tajiri utakuwa tajiri, kama unataka kuwa msomi utakuwa msomi, kama unataka kufanikiwa utafanikiwa, ila yote haya yatatokana na wewe kuamini bila ya wasi wasi wowote kwamba unaweza kupata kile unachotaka kupata.
Misingi ya kuamini ni sawa na kupiga simu, unapata namba uliyopiga. Kama unaamini unaweza kufanikiwa lazima utafanikiwa. Kama unaamini huwezi kufanikiwa, hutaweza kufanikiwa hata ungefanya kitu gani. Kwa hiyo ulivyo sasa ni kutokana na imani iliyopo ndani yako.
Watu wote waliofikia mafanikio makubwa walikuwa na imani kubwa kwenye uwezo wao binafsi wa kufikia mafanikio.
Kama na wewe utaamini ndani ya uwezo wako binafsi utaweza kufikia chochote unachotaka. Ila inabidi uwe una imani kubwa na ufikirie kile unachotaka kufikia kila wakati.
Amini kwamba una uwezo mkubwa, amini kwamba unaweza kuwa, kufanya au kupata chochote unachotaka na pia amini sana kwenye kile unachofanya. Kama imani yako itakuwa kubwa kiasi cha kutoyumbishwa na chochote hakika utaweza kufikia kile unachotaka.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.