Kutokana na kazi kubwa ninayoifanya kupitia AMKA MTANZANIA, KISIMA CHA MAARIFA, GAZETI MTANZANIA na hata sehemu nyingine kwenye mtandao, watu wengi wamekuwa wakitafuta nafasi ya kuonana na mimi. Nafurahi sana kuwa sehemu ya suluhisho la matatizo yanayotukumba watu wengi. Na kama ilivyo falsafa kubwa ninayoishi nayo kwamba unaweza kupata chochote unachotaka kama utawasaidia watu wengi zaidi kupata wanachotaka(unaweza kuisoma vizuri kwa kubonyeza hapa) nafurahi kuendelea kufanya hivi.

Pamoja na hayo yote bado sio rahisi kwa kila mtu kuweza kuonana na mimi. Kuna watu ambao wako mbali sana na hata wale wa karibu kuna gharama gharama kidogo ambazo sio kila mmoja anaweza kuzilipia. Kwa kuliona hili nilianzisha kipengele cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa. Watu wengi wamekuwa wakiandika changamoto zao na nimekuwa nazipatia majibu kila siku ya jumatatu. Pia watu wengi wamekuwa wakiniandika kwa email, ujumbe wa simu na hata kupiga simu kuhusiana na changamoto mbalimbali.

amka na badilika2

Sasa leo nimeona nichukue nafasi hii kukuambia mambo haya kumi ambayo kama ungepata nafasi ya kukutana na mimi ana kwa ana ningekwambia na kama ukiyazingatia utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

1. Wewe ni wa pekee, wewe una uwezo mkubwa sana kuliko unaoutumia sasa. Katika dunia yenye watu zaidi ya bilioni saba hakuna hata mmoja aliyefanana na wewe kwa kila kitu. Hivyo wewe una uwezo usioweza kulinganishwa na binadamu mwingine yeyote. Tumia uwezo huu mkubwa katika shughuli zako na utafikia mafanikio makubwa. Pia tumia ubunifu mkubwa ulioko ndani yako kuwa wa kipekee.

2. Fanya kitu ambacho unakipenda. Usipoteze maisha yako kwa kila siku kufanya kitu ambacho hukipendi. Kwa kufanya hivi utakuwa kama unasukumwa na hutaweza kufikia mafanikio makubwa. Kama kuna kitu ambacho unakifanya sasa ila hukipendi anza mipango ya kuacha kukifanya. Kama kazi au biashara unayoifanya huipendi usiendelee kupoteza muda wako, jipange kuachana nayo na kufanya ile unayoipenda.

Watu wengi wamekuwa wakiniuliza wafanye biashara gani ambayo itawalipa? Jibu ni rahisi sana, fanya biashara inayohusiana na kitu unachokipenda, kwa njia hii utafikia mafanikio makubwa sana. Soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi.

MTANZANIA

3. Chagua kitu kimoja au vichache vya kufanya kwenye maisha yako.

Kuna vitu vingi sana vinakutamanisha uvifanye kwenye maisha yako. Lakini huwezi kuwa na muda au msukumo wa kufanya kila kitu unachotamani kufanya. Hivyo basi chagua kitu kimoja, au vitu vichache ambavyo ndio utafanya kwenye maisha yako. Kitu hiko ulichochagua hakikisha unakifanya kwa moyo wako wote na hakikisha unakuwa bora kuliko mtu mwingine yoyote anayekifanya au aliyewahi kukifanya. Hivi ndivyo unavyoweza kufikia mafanikio makubwa.

4. Changamoto hazikwepeki. Utajitahidi sana kufanya kila kilicho ndani ya uwezo wako ili maisha yako yawe vizuri lakini hutaweza kuzikwepapa changamoto. Unaweza kufanya kila kitu vizuri kabisa, halafu akaja mtu mwingine akakuangusha. Ndivyo dunia ilivyo, changamoto ni sehemu ya maisha yetu na ndio zinatufanya tuendelee zaidi. Hivyo badala ya kulalamikia changamoto unazokutana nazo, hebu zichukulie kama sehemu ya kujifunza na kuonesha uwezo mkubwa ulioko ndani yako.

5. Utashindwa lakini sio mwisho wa safari. Katika wakati mmoja au mwingine katika safari yako ya maisha hata kama unafanya kitu ambacho unakipenda sana utakutana na vikwazo vikubwa vitakavyokufanya ushindwe. Ila kushindwa huko sio mwisho wa safari labda kama utaamua iwe hivyo. Kushindwa huku ni moja ya sehemu ya elimu muhimu itakayokusaidia wewe kufikia mafanikio makubwa. Kushindwa ni moja ya gharama unazotakiwa kulipwa ili kufikia mafanikio makubwa.

6. Usifuate kundi, kimbia mbio zako mwenyewe. Katika jambo lolote unalofanya, usijaribu kabisa kulifanya kwa kuiga au kwa sababu kila mtu anafanya, utakuwa umerahisisha njia ya wewe kushindwa vibaya. Fanya kila unachofanya kwa utofauti mkubwa na kwa mipango yako mwenyewe, ukifuata mkumbo kwa sababu wengine wanafanya hutaweza kwenda mbele zaidi yao. Unaweza kuwaangalia wengine kama sehemu ya kukupa changamoto ila kamwe usifanye kama wao wanavyofanya, kumbuka wewe una uwezo mkubwa na ni wa kipekee. Fanya unachofanya kwa utofauti mkubwa.

7. Mtazamo wako ndio kila kitu. Nikitaka nisiandike sana kuhusiana na hili nitasema hivi; KAMA UNAFIKIRI UNAWEZA AU UNAFIKIRI HUWEZI UKO SAHIHI KABISA. Yaani hakuna anayeweza kukufanya uweze au ushindwe isipokuwa wewe binafsi. Kushinda au kushindwa kunaanzia ndani ya fikra zako. Hivyo mara zote kuwa na mtizamo chanya juu yako mwenyewe na juu ya kile unachofanya. Hata kama mambo ni magumu kiasi gani, angalau endelea kuwa na mtizamo chanya, huu utakuwezesha kufikia mengi zaidi.

8. Utakatishwa tamaa, usiwasikilize. Utakapoanza kufanya kile unachopenda kufanya na utakapokuwa unakifanya kwa tofauti na wengine wanavyofanya watajitokeza watu wengi sana watakaokuambia HUWEZI au UTASHINDWA. Ili kutosumbuana na watu hawa wakubalie kisha wapuuzie, endelea kufanya mambo yako, kama unachokifanya ni halali kisheria na kijamii endelea kufanya, usigeuke nyuma. Wakati mwingine wanaokukatisha tamaa ni watu wako wa karibu kabisa na watakupa kila aina ya ushahidi kwamba kwa nini hutaweza. Wewe wapuuze kwa sababu hakuna anayekujua wewe zaidi ya wewe mwenyewe.

9. Uvumilivu ni muhimu. Kitakachokuvusha kwenye nyakati ngumu na kitakachokufanya uweze kusubiri mpaka mwisho ni uvumilivu. Ni lazima uwe na uvumilivu kwa sababu kuna changamoto nyingi sana na pia itakuchukua muda mrefu kufikia mafanikio.

10. Hakuna kitu cha bure, hakuna njia ya mkato. Katika dunia hii hakuna kitu cha bure, kwa kiingereza wanasema THERE IS NO FREE LUNCH. Ogopa sana mtu anayekuambia utapata hiki bure, kuna jinsi ambavyo unalipia bila ya wewe mwenyewe kujua. Hivyo usipende vitu vya bure au vitu rahisi vinaweza kuwa kikwazo kikubwa kwako kufikia mafanikio makubwa. Pia hakuna njia ya mkato unayoweza kutumia kufikia mafanikio makubwa bila ya kupata madhara. Ukikutana na mtu anakuambia kuna njia rahisi na ya haraka ya kupata fedha au utajiri kimbia haraka sana kumkwepa. Kwanzia kuwekwa misingi ya dunia, kwanzia utawala wa babeli mpaka wa roma fedha imekuwa ikipatikana kwa kufanya kazi ambayo ina thamani kwa watu wengine.

11. Nyongeza, JIUNGE NA KISIMA CHA MAARIFA. Fanya chochote unachoweza ujiunge na KISIMA, ndani ya kisima kila siku utakuwa unajifunza mambo mapya na mbinu mbalimbali za kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Tena jiunge kwa uanachama wa GOLD ili kupata kila kitu kilichopo kwneye KISIMA. Hii ni sehemu ambayo imejaa maarifa makubwa sana ambayo yatakufunza na kukuhamasisha kushukua hatua na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Gharama ya kujiunga kwa GOLD ni tsh elfu hamsini kwa mwaka, hii ni sawa na tsh 4200 kwa mwezi au sawa na tsh 140 kwa siku, yaani shilingi mia moja arobaini kwa siku na itakuwezesha kujifunza mambo ambayo yatakusaidia kufikia mafanikio makubwa. Naweza kusema kama umekosha tsh 140 ya kuwekeza kwenye maendeleo yako kwa siku una tatizo kubwa sana. Kupata utaratibu wa KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi. Na kama ungependa kujiunga ila huwezi kutoa fedha yote kwa wakati mmoja wasiliana nami kwa 0717396253 au email amakirita@gmail.co na tutaweka utaratibu mzuri utakaokuwezesha wewe kuendelea kujifunza huku ukiendelea kulipa.

Anza kutumia mambo haya sasa na utaona mafanikio makubwa sana siku zijazo. Isome makala hii mara kwa mara na ikiwezekana print na uwe nayo sehemu ambayo unaweza kuisoma kila unapohitaji kuhamasika au unapoona mambo hayawezekani.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa, najua unaweza, anza sasa.

TUKO PAMOJA NA HAKIKA TUTAKUTANA KILELENI.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo5