Ni mara ngapi umewahi kutamani muujiza utokee na mara moja uwe tajiri mkubwa, na uwe na mafanikio na furaha tele? Hii ni ndoto ambayo inawatokea watu wengi katika maisha yao. Hijalishi hali uliyonayo sasa, iwe umeshapata mafanikio ya kukuridhisha au unasukuma maisha kiubishi, unapenda kuwa zaidia ya hapo ulipo sasa. Na ndio maana unapata mawazo haya ya kutokea kwa muujiza na kuweza kufikia utajiri, mafanikio na furaha.

Habari nzuri ni kwamba muujiza huu unaofikiria tayari unao na unaweza kuufanya ukawa kweli na ukafikia mafanikio makubwa sana. Muujiza huo sio wa uchawi au mwingine wowote unaofikiria. Muujiza huu unatokana na ujuzi, uzoefu, mawazo na kikubwa zaidi matendo. Hijalishi una ujuzi kiasi gani au umepata uzoefu mkubwa kiasi gani na hata mawazo yako yawe mazuri kiasi gani bila ya kufanya matendo hakuna muujiza wowote unaoweza kutokea kwenye maisha yako. Matendo ndio yatakufanya uweze kufikia mafanikio makubwa kupitia ujuzi, uzoefu na hata mawazo mazuri uliyonayo.

Fanya tathmini ya ulipo sasa.

Ni kiwango gani cha mafanikio ulichonacho sasa hivi unavyosoma hapa? Chukua muda leo hii baada ya kumaliza kusoma hapa na ujichunguze kwa makini kwa kujibu maswali haya kama umeajiriwa;

Je unafurahia kazi unayofanya? Je kazi unayofanya inakukosesha furaha au kufanya maisha yako yawe magumu zaidi?

Je uwezo wako unatumika vizuri katika sehemu ambayo unafanya kazi sasa? Je upo katika cheo kinachoendana na uwezo wako?

Je unakatishwa tamaa na mambo fulani yanayoendelea unapofanya kazi? Je umeachwa kwenye kuandishwa cheo? Je umenyimwa ongezeko la mshahara?

Kama unachofanya sasa hakikuvutii na hukifurahii na kila ukiangalia kesho au miaka mitano ijayo huoni tofauti yoyote na leo, huna haja ya kuendelea na maisha hayo, fanya kitu sasa. Fanya kitu leo hii ambacho kitakusaidia kubadili hali ya mambo. Hutokuja kupata nafasi ya kubadili maisha yako zaidi ya leo hii, kesho kila siku itaendelea kuwa kesho, kama utashindwa kufanya leo, kesho haitafika.

Mambo matatu muhimu ya kufanya ili kubadili hali ya maisha yako.

1. Gundua uwezo wako mkubwa.

Kumbuka una uwezo mkubwa sana ulioko ndani yako. Kama ukiweza kutumia uwezo huu unaweza kufikia mafanikio makubwa sana. Jiulize maswali yafuatayo; Je nianzishe biashara yangu? Je nijiajiri mwenyewe? Je nimechelewa sana kufanya mabadiliko? Unaweza kufanya mabadiliko sasa kwenye maisha yako. Hujachelewa bado, bila ya kujali umri wako, kama ukiamua na kuanza utekelezaji leo hujachelewa, ila ukisema kesho ndio umechelewa.

2. Jihamasishe mwenyewe.

Uwezo wa kuwahamasisha wengine ni kitu muhimu sana unachohitaji kuwa nacho iliuweze kufikia mafanikio makubwa. Shauku yako ndio itaweza kuwashawishi watu mbalimbali kuweza kushirikiana na wewe katika biashara unayofanya. Na ili uweze kuwashawishi wengine ni lazima uweze kujishawishi wewe kwanza, ni lazima uweze kujihamasisha na ni lazima uwe na hsuku kubwa juu ya kile unachofanya. Vitu hivi vitakufanya uweze kujiamini na kuweza kufikia mafanikio.

Kuingia kwenye biashara au kujiajiri ni hatua kubwa sana kwenye maisha na inaweza kukutisha. Lakini kama unaweza kujihamasisha na una shauku kubwa utaweza kujiamini na kuendelea kusonga mbele. Muhimu zaidi ni kuwa na mtizamo chanya muda wote ili kuweza kufikia mafanikio.

3. Jiridhishe kabla ya kufanya mabadiliko.

Kabla hujafanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako ni kuhimu kujiridhisha kwanza. Japo kujiridhisha sio dhamana kwamba utafanikiwa, itakusaidia kujiandaa na kuweza kukabiliana na changamoto zitakazotokea mbeleni. Kabla ya kuingia kwenye biashara hasa kama unatokea kwenye ajira ni vyema kuijua vizuri biashara unayokwenda kufanya na pia kujiandaa kwa sababu mwanzo huwa ni mgumu.

Pamoja na changamoto zote unazoweza kukutana nazo zisiwe kikwazo cha wewe kushindwa kufanya mabadiliko kwenye maisha yako na kuendelea kutumikia kazi ambayo haikufurahishi. Kufanya kazi ambayo haikufurahishi sio kwamba tu inakunyima furaha bali inakuweka katika hatari ya kupoteza afya yako.

Fanya kitu sasa.

Kama tulivyosema msingi mkuu wa miujiza yote ni matendo. Fanya kitu sasa mabacho kitabadili maisha yako ya mbele. Fanya tathmini ya kazi unayofanya, andika malengo yako na kisha weka mipango ya kuyafikia na uanze kuifanyia mipango hiyo kazi.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.