Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.

Kwenye uchambuzi uliopita tuliona jinsi ambavyo RICH DAD alimfundisha Robert na Mike kwamba nyumba ya kuishi sio mali inayozalisha(ASSET) bali ni mali isiyozalisha(LIABILITY). Robert alifafanua ni jinsi gani watu masikini wanavyoaminishwa kwamba kwa kuwa na nyumba una mali inayozalisha. Pia alieleza ni jinsi gani matajiri wanazidi kuwa matajiri kwa kuwekeza kwenye mali zinazozalisha na masikini kuendelea kuwa masikini kwa kuwekeza kwenye gharama na mali zisizozalisha.

Maamuzi ya kununua au kujenga nyumba ya gharama badala ya kuwekeza kwenye mali inayozalisha yanaweza kuwa na madhara yafuatayo;

1. Kupoteza muda.

Kwa kutumia fedha yako kujenga au kulipia nyumba unapoteza muda ambao kama ungewekeza kwenye mali inayozalisha ingekuwa imeongezeka thamani zaidi.

2. Kupoteza mtaji.

Kama umeshaweka fedha zako kwenye nyumba unakosa fursa ya kuweza kuzitumia kama mtaji wa biashara au kuwekeza sehemu nyingine.

3. Kukosa elimu.

Kwa kutumia fedha kujenga au kulipia nyumba kunamfanya mtu akose fedha ya kuwekeza na hivyo kutokupata uzoefu kuhusu uwekezaji. Kwa kukosa uzoefu huu wanakuwa hawajui lolote kuhusu uwekezaji na hivyo kukosa fursa nyingi kwenye maisha yao.

Robert anasema wale wanaotumia fedha zao kulipia gharama badala ya kuwekeza wanakosa nafasi adimu ya kuwa “sophisticated investors ” yaani wawekezaji wa kisasa. Anasema uwekezaji bora huuzwa kwa wawekezaji wa kisasa na wao ndio huwauzia wale wanaoogopa kuchukua mazingira ya hatari.

Robert anasema maisha ya baba yake(POOR DAD) ni mfano halisi wa mtu anayeishi kwenye mbio za panya. Matumizi yanaongezeka kadiri mapato yanavyoongezeka na hivyo anashindwa kuwekeza kwenye mali zinazozalisha. Mwishowe anajikuta kwenye madeni makubwa na hivyo maisha yake yanakuwa ya kulipa madeni.

Anasema maisha ya RICH DAD ni mfano halisi wa mtu aliyejipanga kufikia uhuru wa kifedha. Anawekeza kwenye mali zinazozalisha badala ya kuongeza matumizi. Na hii humuwezesha kupata kipato cha ziada kupitia uwekezaji na kipato hiko kuwekezwa tena na hivyo uwekezaji kukua zaidi. Kwa njia hii TAJIRI ANAENDELEA KUWA TAJIRI. Watu wa daraja la kati wanajikuta kwenye matatizo ya fedha kila mara kwa sababu chanzo chao pekee cha fedha ni mshahara na mshahara unavyoongezeka kodo nazo zinaongezeka na matumizi pia yanaongezeka na hivyo wanajikuta kwenye mbio za panya.

Njia ya kwanza ya mtu kuanza kuelekea kwenye utajiri ni kujua tofauti ya ASSETS na LIABILITIES na kuwekeza zaidi kwenye assets ili kuweza kuendelea kuzalisha mapato zaidi. Pia ni lazima kupunguza matumizi na kununua mali zisizozalisha ili kupata fedha nyingi za kuwekeza zaidi.

Robert anasema kwamba dhana ya kuchukulia kwamba nyumba ya kuishi ni uwekezaji unaozalisha na falsafa kwamba ongezeko la kipato unaweza kuongeza matumizi ha hata kuwa na nyumba kubwa zaidi ndio chanzo cha matatizo makubwa ya kifedha kwenye jamii zetu. Ongezeko la matumizi linafanya familia nyingi kuingia kwenye madeni ambayo yanawaingiza kwenye matatizo makubwa. Haya ni maisha ya hatari sana ambayo yanasababishwa na ukosefu wa elimu ya fedha.

Kwa waajiriwa ambao wanaona nyumba yao ndio uwekezaji mkubwa wanawafanyia watu wengine kazi bila ya wao kujua. Kwanza wanamfanyia kazi aliyewaajiri. Hapa wanafanya kazi ambayo inamfaidisha sana mwajiri wao ila yeye anawalipa sehemu ndogo. Pili wanaifanyia kazi serikali maana kila wanapopokea mshahara serikali inakata kodi kwanza. Hivyo hata mtu akifanya kazi kwa nguvu zaidi anazidi kuongeza kodi anayolipa serikalini. Na tatu wanafanyia kazi benki, hapa watu hawa wanakuwa na mikopo mingi hivyo wanapopata mshahara wanakatwa malipo ya mikopo hiyo. Kumbuka mikopo hii ina riba na wakati mwingine inakuwa riba kubwa.

Robert anasema kwa kufanya kazi kwa nguvu zaidi unazidi kunufaisha hawa watatu unaowafanyia kazi, mwajiri wako, serikali na benki au taasisi za fedha.

Robert anasema ili kufikia uhuru wa kifedha unahitaji kufikia utajiri ambapo hata usipofanya kazi bado maisha yako yanaweza kuendelea bila ya kutetereka. Na unaweza kufikia utajiri huu kama utakuwa umewekeza vya kutosha. Ila kama unategemea mshahara tu kama chanzo chako cha mapato huwezi kufikia utajiri huu.

Kitu kikubwa cha kukumbuka ni kwamba Matajiri wananunua ASSETS, masikini wanalipia gharama na daraja la kati wananunua LIABILITIES wakiamini ni ASSETS.

Tunajifunza nini hapa?

1. Kuwekeza kwenye nyumba ambayo haizalishi kunakupotezea muda, fedha na pia kunakukosesha elimu.

2. Matajiri wanaendelea kuwa matajiri kwa kuwekeza zaidi kwenye mali zinazozalisha.

3. Masikini wanaendelea kuwa masikini kwa kuwekeza kwenye gharama na mali ziasizozalisha.

4. Sophisticated investors(wawekezaji wa kisasa) ndio wanaofaidika zaidi kwenye uwekezaji.

5. Ni muhimu kujua tofauti ya ASSETS na LIABILITIES na kuwekeza zaidi kwenye ASSETS ili kuweza kufikia kwenye uhuru wa kifedha.

6. Kuna sehemu tatu unazofanyia kazi, mwajiri wako, serikali na benki au taasisi za fedha.

7. Jinsi unavyozidi kufanya kazi zaidi, kama huna elimu ya fedha ndio unavyozidi kuwanufaisha wengine.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.

TUKO PAMOJA.