Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.

Katika masomo sita ambayo Robert alisema amefundishwa na atatufundisha kuhusu kufikia uhuru wa kifedha, somo la tatu ni kujua biashara yako vizuri.

Robert anasema watu wengi wanafanya biashara ila hawajui ni aina gani ya biashara wanayofanya au hawaijui vizuri biashara hiyo. Anasema matatizo ya fedha yanatokana na watu kuwafanyia wengine kazi kwa muda mrefu bila ya kufikiria hatima ya maisha yao itakuwaje. Anasema mfumo wa elimu unaandaa vijana kuwa waajiriwa zaidi ya kufikia uhuru wa kifedha. Anasema maisha yao yanaishia kutegemea chanzo kimoja cha mapato ambacho ni mshahara.

Anasema watu wengi wanajifunza taaluma mbalimbali na wanapoajiriwa wanafanyia kazi taaluma zao. Tatizo kubwa linakuja pale watu wanapofikiri kwamba taaluma zao ndio wanazifanyia kazi, kumbe wanafanya kazi nyingine tofauti na taaluma zao. Robert anatumia mfano mmoja kwamba anamuuliza mtu ni shughuli gani unafanya, anamjibu ni Banker anamuuliza tena je unamiliki benki? Anajibu hapana, nafanya kazi kwenye benki. Robert anasema pamoja na taaluma yako unahitaji kuwa kwenye biashara. Unahitaji kujua biashara ambayo itakuwezesha kuwekeza kwenye ASSETS ili uweze kufikia uhuru wa kifedha.

Anasema watu wengi wanaogopa kuchukua risk na hivyo kujikuta wakitegemea ajira tu na hatimaye kuendelea kuwa na maisha magumu. Anasema watu wengi hugundua nyumba sio ASSET pale wanapoacha au kuachishwa kazi na hivyo kujikuta hawana kipato na huku nyumba au mali nyingine isiyozalisha ikiendelea kuchukua gharama. Anasema katika wakati huu ndio watu huanza kuuza mali hizi zisizozalisha na cha kushangaza bei wanayouzia inakuwa ndogo sana kuliko bei waliyonunulia.

Robert anashauri hata kama bado umeajiriwa uchague ni biashara gani unataka kuwepo na uijue vizuri biashara hiyo. Anashauri uanze kuwekeza kwa kununua mali zinazozalisha badala ya kununua mali zisizozalisha. Anasema kwa mfano ukinunua gari leo milioni kumi, hata kama utaliuza baada ya mwezi mmoja hutaweza kuliuza kwa milioni kumi, itakuwa chini ya hapo.

Je ni assets gani unaweza kuanza kununua?

Robert anasema kwa ushauri wake kuna baadhi ya ASSETS ambazo anashauri mtu aanze kuzinunua;

1. Biashara ambayo haihitaji uwepo wako moja kwa moja. Biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo pale kila wakati.

2. Kuwekeza kwenye kununua hisa, vipande, na ina nyingine za dhamana za fedha.

3. Uwekezaji kwenye nyumba za kupangisha au kuuza.

Hizi ni sehemu ambazo mtu anaweza kuwekeza kwa kuanza kidogo kidogo na akaanza safari ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha.

Robert anasema alipokuwa mdogo POOR DAD alimshauri kutafuta kazi inayolipa vizuri wakati RICH DAD alimshauri kuanza kuwekeza mapema ili kupata uhuru wa kifedha. Alimwambia kama unachowekeza hukipendi hutajisumbua kukijua zaidi. Robert anasema alikuwa anapenda sana majengo na hivyo alifikiria kuwekeza kwenye nyumba za kupanga na kuuza. Pia alipenda makampuni na hivyo kuwekeza kwenye hisa.

Robert anasema hata wakati alipokuwa ameajiriwa aliendelea na kazi yake huku akiendelea na biashara yake ya uwekezaji. Alikuwa makini kwenye uwekezaji wake na kuendelea kujifunza zaidi. Robert anashauri kujenga na kuimarisha ASSET zako, anasema fedha yoyote inayoingia kwenye uwekezaji wako usikubali iondoke huko, ifanye iwe inakufanyia wewe kazi. Anasema watu masikini wanatumia fedha zao vibaya kwa kununua vitu vya kifahari ili waonekane ni matajiri na hivyo kushindwa kuwekeza kwenye mali zianzozalisha. Baadae wanajikuta kwenye madeni makubwa na hivyo kuwa kwenye mbio za panya. Matajiri wananunua vitu vya kifahari kwa fedha zilizozalishwa na uwekezaji wakati masikini wananunua vitu vya kifahari kwa fedha za jasho lao wenyewe.

Robert anasema yeye na mke wake walipokuwa wana fedha nyingi zinazotokana na uwekezaji wao wa nyumba aliweza kununua gari aina ya mercedes. Anasema haikuwa tabu kwao kwa sababu uwekezaji wao ndio umenunua nyumba, japo ilibidi kusubiri mpaka ukue. Anasema mtu anaponunua vitu vya kifahari kwa fedha zake mwenyewe anajiingiza kwenye matatizo makubwa sana kifedha.

Robert anasema unapoweza kuijua biashara uliyowekeza na kuweza kuikuza mpaka ikazalisha kiasi cha kuweza kuishi bila ya kufanya kazi moja kwa moja unakuwa umejifunza siri kubwa sana ya kufikia uhuru wa kifedha.

Tunajifunza nini hapa?

1. Kazi unayoifanya sio biashara yako, ni taaluma yako.

2. Lisha ya kuwa na kazi ni vyema ukawa na uwekezaji ambao hauhitaji muda wako sana.

3. Unaweza kuwekeza kwenye biashara, hisa, vipande na hata nyumba na baadae ukakua zaidi.

4. Masikini wananunua vitu vya anasa kwa fedha za jasho lao hivyo kuingia kwenye matatizo makubwa ya kifedha.

5. Matajiri hununua vitu vya anasa kwa fedha inayozalishwa kutokana na uwekezaji na hivyo kuendelea kuwa matajiri zaidi.

6. Ijue biashara unayofanya au unayotaka kuifanya na jifunze zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.

TUKO PAMOJA.