Haiba ya mtu inatokana na tabia na sifa za mtu huyo. Binadamu wote katika vipindi tofauti vya maisha yao hutengeneza tabia mbalimbali za kufikiri, kuhisi na hata kutenda. Baadhi ya tabia hizi hutengenezwa kwa kujua, nyingine hutengenezwa kwa kutokujua. Jumla ya tabia zote alizonazo mtu ndio zinatupatia haiba ya mtu inayomfanya kuwa tofauti na watu wengine na pia kutengeneza uhusiano wake na watu wengine.

Haiba nzuri inatengenezwa na tabia ambazo zinawafanya watu kukubaliana na wewe. Haiba mbovu hutengenezwa na tabia ambazo huwafanya watu kutokukubaliana na wewe.

Kuwa na haiba nzuri inayowavutia watu wengi ni moja ya mahitaji ya wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa. Haiba nzuri itakupa nguvu itakayokuwezesha kuwa na ushawishi na hata kuwa kiongozi mzuri.

Jinsi ya kutengeneza haiba inayoendana na wakati.

Kwa kuwa haiba ni kitu muhimu sana kwako hapa tutajifunza hatua muhimu za kufuata ili kuweza kutengeneza haiba nzuri itakayokuletea mafanikio na utajiri.

1. Onesha kupendezwa au kujali watu wengine. Kwa kufanya hivi watu nao watakupenda na kukujali.

2. Kubali na toa sifa kwa uwezo na mafanikio ya watu wengine. Shukuru kwa kila jambo ambalo mtu amefanya kwa ajili yako.

3. Tengeneza sauti ya chini na yenye utulivu. Sauti kali na ya kuropoka huwafanya watu wasivutiwe na wewe.

4. Kuwa na mpango wa kukua zaidi, kujifunza zaidi na kufanikisha kitu chenye maana kwako na kwa watu wengine. Jinsi unavyojua zaidi na kufanya zaidi inakujengea heshima kubwa na hivyo kuwa na haiba nzuri.

5. Kuwa na hitaji la kuweza kujitegemea hasa katika kufikiri. Ni muhimu uweze kuwa na mawazo yako binafsi yasioingiliwa au kuathiriwa na mawazo ya watu wengine. Kutegemea wengine kwa kila kitu inakufanya wewe kutokujiamini na hatimaye kuharibu haiba yako.

Pamoja na hayo kuna mambo mengine muhimu unayotakiwa kufanya ili kuwa na afya njema na kuweza kutengeneza haiba nzuri. Mambo hayo ni;

1. Kula vizuri. Kile unachokula ndio kinachokutengeneza wewe. Ukila vyakula vya hovyo hovyo utaishia kuwa mtu wa hovyo hovyo. Ukila vyakula vizuri(mlo kamili) utakuwa na afya njema na hivyo kuwa na haiba nzuri.

2. Pata muda wa kupumzika. Mwili wako unahitaji muda wa kutosha wa kupumzika ili akili yako nayo ipumzike. Kwa kukosa mapumziko kwa muda mrefu hata uwezo wako wa kufikiri unaathirika na hivyo kushindwa kufanya maamuzi mazuri.

3. Jumuika na watu wengine. Hudhuria matukio mbalimbali ambayo watu mbalimbali wanahudhuria, inaweza kuwa mikutano, sherehe, kazi za kujitolea au hata matembezi ya kutoa misaada. Katika sehemu hizi unajifunza mambo mengi na pia unapata nafasi ya kuonesha haiba unayotengeneza.

Kuwa na haiba nzuri ili uweze kukubalika na wengi na uweze kuwashawishi ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.