Kila mmoja wetu anakubali kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo. Na hata maandiko yameeleza kwamba asiyefanya kazi na asile. Hivyo ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kufanya kazi kwa maendeleo yake binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Katika moja ya makala tuliwahi kujadili kwamba kama unataka kufanikiwa usifanye kazi (bonyeza hapo kusoma). Kikubwa tulichojifunza kwenye makala hiyo ni kwamba ni muhimu sana kupenda kazi unayoifanya, vinginevyo itakuwa vigumu sana kufikia mafanikio makubwa.

Sasa leo naandika barua hii kwako mfanyakazi ambaye jumatatu kama ya leo unaiona ni siku mbaya sana kwenye maisha yako. Naandika barua hii kwako mfanyakazi ambaye umefanya kazi kwa miaka mitano, kumi, na hata ishirini lakini bado huoni mafanikio yoyote.

Naandika barua hii kwako mfanyakazi ambaye unaiona kazi yako kama mtego ambao ukitaka kuondoka unaona utakosa mengi na ukiendelea kuwepo unakosa mengi zaidi. Na naandika  barua hii kwako mfanyakazi ambaye uko njia panda hujui kama uache kazi hiyo au uendelee na kazi hiyo.

KUCHOKA

Kuna maswali muhimu ambayo unapaswa kujiuliza ili kujua kama kazi uliyonayo sasa itakufikiasha kwenye mafanikio au la.

Maswali sita muhimu ya kujiuliza.

Jiulize maswali haya kama bado umeajiriwa na yatakupa picha ya kazi unayofanya sasa na malengo yako ya mbeleni. Jibu ndio au hapana kwenye kila swali halafu baadae utajua ni hatua gani ya kuchukua.

1. Je kazi yako ya sasa inakuridhisha?

Je ni kazi ambayo inakupa amani ya moyo, unajisikia vizuri unapoifanya na unaridhika na kile unacholipwa kulingana na mchango unaotoa kwa mwajiri wako?

2. Je kuna nafasi ya wewe kupandishwa cheo?

Kwa hali ilivyo kwenye sehemu yako ya ajira kuna nafasi ya wewe kupanda cheo zaidi ya hapo ulipo sasa. Na nafasi hiyo ni ya uhakika kiasi gani?

3. Je kama ukipandishwa cheo itakusaidia kufikia malengo yako?

Kama ikatokea kwamba umepandishwa cheo, je nafasi hiyo itakuwezesha kufikia malengo yako kwenye maisha? Au itaendelea kuwa sehemu ya matatizo kwako?

4. Je utaweza kupata kazi unayopendelea zaidi kama utaendelea kufanya kazi unayofanya sasa?

Kama utaendelea kufanya kazi hiyo je itakuwezesha kupata kazi nyingine ambayo unaipenda zaidi?

5. Je kazi yako inakupa nafasi ya kuonesha uwezo mkubwa ulioko ndani yako?

Kwa nafasi unayofanyia kazi unapata nafasi ya kuonesha uwezo mkubwa ulio ndani yako? Au unabanwa na kujikuta unafanya kazi zisizo na kiwango kikubwa na hivyo kupunguza uwezo wako?

6. Je unafurahia kazi unayoifanya?

Unapoamka asubuhi una shauku kubwa ya kwenda kwenye kazi yako? Je unapotoa bidhaa au huduma unayotakiwa kutoa unakuwa na shauku ya kufanya hivyo? Je masaa yako ya kazi unaona ni kama sehemu ya kujifunza na kuonesha uwezo wako zaidi au unatamani yaishe haraka na uondoke kazini?

Jibu maswali hayo kwa usahihi bila ya kujionea aibu au kufanya unafiki. Kama umejibu hapana kwenye swali lolote hapo juu anza kufikiria jinsi ya kuondoka kwenye kazi hiyo unayofanya kwa sababu kuendelea kuifanya kutafanya maisha yako yawe magumu. Kutafanya maisha yako yaendelee kuwa magumu kwa sababu kazi yako utaiona ngumu na mbaya kila siku na nafasi ya wewe kufikia malengo yako itakuwa ngumu. Kumbuka kama kazi yako inakupa msongo wa mawazo sio nzuri kwa afya yako.

Unataka kujua ni maandalizi gani ya kufanya kabla hujaacha kazi yako hiyo? Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo utajifunza mengi zaidi. Ukiwa kwenye KISIMA unaweza kuanza kusoma makala hii; Mambo kumi muhimu unayotakiwa kujua kabla ya kuacha kazi na kwenda kujiajiri.(kama tayari ni mwanachama unaweza kufungua na kusoma)

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo432