Binadamu tunafanya mambo yetu kama vile tuna muda usioa na kikomo. Ukweli ni kwamba katika vitu ambavyo tunavyo kwa kiwango kidogo sana ni muda. Muda ni zawadi ambayo ipo kwa ukomo. Hakuna mtu yeyote anayeweza kuongeza hata sekunde moja kwenye siku hata angekuwa na uwezo au fedha nyingi kiasi gani. Muda ni mfupi sana na hii inaufanya uwe wa thamani sana.

Muda pekee ambao unaweza kufanya kitu chochote kwenye maisha yako ni sasa hivi. Kama unataka kufanya maisha yako yawe kama unavyotaka wewe, muda pekee wa kufanya hivyo ni sasa hivi, sio jioni ya leo na wala sio kesho au mwaka ujao, ni sasa hivi unavyosoma hapa.

Kila siku asubuhi ni nafasi mpya ya kuweza kuanza vizuri bila ya kujali jana ilikuwa siku mbaya kiasi gani au jana umefanya makosa mengi kiasi gani. Kila siku usiku ni nafasi ya kumaliza yale makosa na kushindwa kulikotokea kwenye siku hiyo na kulala na matumaini kwamba kesho itaanza siku nyingine mpya, na utakuwa na nafasi nyingine ya kufanya kwa ubora zaidi ukiwa tayari umejifunza na una uzoefu wa siku iliyopita. Njia bora ya wewe kuweza kupata kilicho bora kwenye maisha yako na kufikia mafanikio makubwa ni kuweza kuitumia kila siku, kila saa na kila dakika kwa ufanisi mkubwa.

Chochote kile ambacho unataka kitokee kwenye maisha yako, ni lazima uanze kukifanya sasa. Kama unataka kufikia mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya ni lazima leo ujifunze, ujiendeleze na pia ufanye kazi zitakazokupeleka kwenye mafanikio. Ni lazima ujifunze na kujihamasisha ili kuweza kuwa na shauku kubwa kwa kazi au biashara yako. Ni lazima ujiendeleze kwa kujifunza zaidi kwenye taaluma yako, kujua ugunduzi mpya na njia za kisasa zinazoboreshwa kila siku. Na pia ni lazima uwe tayari kufanya kazi yenye maana ili uweze kuzalisha majibu yenye thamani kwa watu wengine.

Ni leo hii ndio unaweza kuwa mfanyakazi mzuri, mfanyabiashara mzuri, mzazi mzuri, mume/mke mzuri, rafiki mzuri na hata kuwa kiongozi mzuri kwa watu wanaokuzunguka. Ni leo tu ndio unaweza kufanya yote haya, kesho haiwezi kufika kama hutoanza leo. Kama una ndoto ya kuwa na mafanikio na furaha ni lazima leo uanze kufanya yale yatakayokusogeza kwenye mafanikio na hata furaha.

Jinsi ya kupanga muda wa mwisho(deadline).

Katika malengo na mipango yoyote unayoweka kwenye maisha yako, ni lazima uwe na muda maalumu wa kukamilisha mambo uliyopanga. Mara nyingi tunajiwekea muda ambao ni mrefu sana na hivyo kujikuta hatutumii vizuri muda wetu, au tunajiwekea muda mfupi sana na kujikuta tunashindwa kukamilisha na baadae tunajiangusha wenyewe.

Njia nzuri ya kupanga muda wa mwisho wa kufanya jambo lolote na kuweza kulifikia kwa wakati husika unaweza kufanya yafuatayo. Gawa muda wako wote kwenye wiki, siku na saa utakazofanya kazi. Kisha gawa mipango yako katika kipindi hiko yaani jua wiki fulani utafanya nini na ndani ya hiyo wiki jua siku fulani utafanya nini na katika kila siku jua saa fulani utafanya nini. Hii itakuwa rahisi kwako kufanya jambo fulani kwa wakati wake na hivyo kukuwezesha kufikia malengo yako.

Mambo muhimu ya kufanya ili kuweza kuwa na matumizi mazuri ya muda.

Ili uweze kuwa na matumizi mazuri ya muda ni muhimu uweze kuwa na mpangilio mzuri wa muda wako na siku yako. Kama ukiweza kuwa na mpangilio huu na kuufata vizuri utaweza kuona thamani ya matumizi mazuri ya muda wako. Mambo hayo ni;

1. Siku ya kazi. Hii inamaanisha masaa ambayo umetenga kwa ajili ya kufanya kazi kwa siku. Inaweza kuwa saa moja, masaa mawili, au hata masaa kumi. Kama umeajiriwa tayari umeshapangiwa masaa yako ya kazi, na kama kuna kitu kingine unafanya nje ya ajira ni vyema kukipangia muda wake wa kufanya. Kama umejiajiri ni vyema pia ukajipangia ni muda gani unakuwa muda wa kazi kwako.

2. Pangilia muda wako wa uzalishaji. Kila mmoja wetu anamuda ambao akili yake inakuwa vizuri sana na anaweza kufanya kazi kwa utulivu na ubunifu mkubwa. Upangilie muda huu ili uweze kuutumia vizuri kufikia uzalishaji mkubwa na mafanikio makubwa pia.

3. Pitia mipango yako ya kila siku na ondoa chochote ambacho hakikuletei kukua, fedha, au ubora zaidi. Sio kila kitu ulichopanga kufanya kinaweza kuwa matumizi mazuri ya muda wako.

4. Pangilia mabadiliko. Jua kwamba kuna wakati unaweza kushindwa kufanya jambo ulilopangilia kufanya kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wako. Ni muhimu kuwa na jambo lingine la kufanya katika muda huo ili uepuke kupoteza muda.

5. Kuwa na mpango wa ziada. Jua kwamba kuna dharura zitatokea, unaweza kupanga miadi na mtu ikashindikana na mambo mengine ambayo yanaweza kukukwamisha. Jiandae kwa nyakati kama hizi ili usije kupoteza muda wako.

6. Fanya kazi za kawaida wakati ambao umechoka au unaweza kuwa unapoteza muda. Katika kazi au biashara zako kuna majukumu mengine ni ya kawaida sana na wakati wa kuyafanya haihitaji uwe umetulia au utumie ubunifu mkubwa. Yafanye majukumu haya wakati ambao umechoka au unaweza kuwa kwenye hali ya kupoteza muda.

Jifunze na kuwa na mpango mzuri wa matumizi mazuri ya muda wako ili uweze kufikia ndoto zako na kufikia mafanikio makubwa. Kumbuka binadamu wote tuna muda sawa, tofauti inakuja kwenye matumizi ya muda huu. Kuwa mjanja na kuwa bahili wa muda wako, utanufaika sana kwa hili.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.