Mamilioni ya watu wanaenda na maisha bila ya kujua yanawapeleka wapi. Watu hawa wanafanya kile ambacho kinafanywa na kila mtu au kinachoonekana ni cha kawaida kufanya. Hawa ni watu ambao wanaamini kuna bahati na wao hawajapata bahati hiyo ndio maana maisha yao hayajawa vizuri.

Sasa wewe ondoka kwenye kundi hili la watu, wewe sio wa kusubiri bahati ikujie, bali wewe ni wa kutengeneza bahati yako mwenyewe. Kumbuka tulisema bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa.

Kuna mambo manne muhimu unayotakiwa kufanya ili kutengeneza bahati yako;

1. Weka malengo.

2. Kuwa na mipango ya kufikia malengo hayo na ya kila siku.

3. Tafuta fursa.

4. Tumia fursa kufikia mafanikio makubwa.

Jinsi ya kuweka malengo ya maisha yako.

Kila mtu ana vitu fulani ambavyo anapenda kufanya au angependa kuwa navyo kwenye maisha yake. Na mara nyingi vitu hivi vinagharimu fedha. Inawezekana unapenda kusafiri sehemu mbalimbali duniani, au unataka kuanzisha biashara yako au unataka kuwa na uwekezaji mkubwa vyote hivi unahitaji kuwa na fedha. Na fedha hizi sio za wizi au utapeli, bali fedha ulizotafuta kwa jasho lako.

Hivyo bila ya kujali ni malengo gani unayo kwenye maisha, moja ya malengo yako lazima liwe kupata kiasi fulani cha fedha. Ni lazima ujiwekee malengo kwamba kwa mwaka unahitaji kuingiza kiasi gani cha fedha ili uweze kufikia malengo unayotaka kwenye maisha yako.

Weka lengo hili la kupata kiasi fulani cha fedha kuwa lengo la maisha yako na mengine yote yatafuatia. Kujifunza zaidi jinsi ya kuweka malengo soma makala za malengo hapa.

Tafuta fursa, haitakutafuta wewe.

Mara nyingi watu husema sijapata fursa yoyote ya kuniwezesha kufikia mafanikio. Waulize je umetafuta fursa kwa kiwango gani? Wanaishia kukosa majibu. Fursa haitakufata wewe hapo ulipo ili uweze kuitumia ni lazima wewe utafute fursa kulingana na malengo na mipango yako kwenye maisha yako.

Kutafuta fursa ndio ufunguo wa kufikia mafanikio. Mafanikio yako kwenye maisha yatatokana na jinsi unavyoweza kutafuta na kutumia fursa. Kama ulipata fursa ukaichezea au kuharibu huo sio mwisho wa dunia, endelea kutafuta fursa nyingine.

Jinsi ya kujenga wazo kufikia mafanikio makubwa.

Hata uwe na mawazo mazuri kiasi gani hayawezi kuwa na thamani yoyote kama hayatafanyiwa kazi. Kuna maelfu ya mawazo ambayo yanapita kwenye kichwa chako kila siku ambayo yanaweza kukufanya wewe kuwa tajiri mkubwa sana kama yakiweza kutumika.

Kuna hatua tatu za kuendeleza wazo lako ili kufikia mafanikio makubwa.

1. Andika wazo lako kwenye karatasi na kisha andika orodha ya njia zote ambazo wazo hilo linaweza kutumia kukuletea faida.

2. Pitia njia hizo ulizoorodhesha na kisha ondoa zile ambazo zinahitaji muda mwingi au fedha nyingi kwa sasa, au ambazo haziwezi kuleta faida kubwa.

3. Anza kufanyia kazi njia hizo ulizoona zinaweza kukuletea faida kwa sasa. Endelea kutengeneza mawazo zaidi kwa ajili ya kuboresha.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.