Wengi wetu huwa tunajikuta ni watu wa kuumia sana na kujuta hasa mambo yetu yanapokataa na kwenda kinyume tulivyotarajia. Hiki huwa ni kipindi kigumu sana kwa wengi, ambacho huwafanya wengi wahisi kama vile maisha hawana tena, wakati uwezo wa kubadili hali hiyo unakuwa upo.
 

Unapokutana na hali hii inakuwa ni muhimu sana kwako wewe ukumbuke vitu muhimu vitakavyoweza kukusaidia kusonga mbele na safari ya mafanikio uliyonayo la sivyo unaweza ukajikuta unakata tamaa katika maisha yako.
(SomaVitu muhimu unavyotakiwa kukumbuka wakati mambo yako yanapokwenda hovyo )
Na ili kufanikiwa tena katika kipindi hiki kigumu kwako vipo vitu ambavyo hutakiwi wewe kuvifanya kabisa la sivyo, utajikuta unaharibu vitu vingi sana kama utachukua hatua ya kufanya vitu hivi katika kipindi ambacho mambo yako yanakwenda vibaya. Unatakiwa kuwa makini na mtulivu kutofanya vitu hivi kwani kila kitu kinawezekana kubadilika katika maisha yako endapo utatulia.
Vifuatavyo ni vitu muhimu usivyotakiwa kuvifanya wakati mambo yako yanapokwenda vibaya:-
1. Acha kukata tamaa.
Hiki ni kipindi ambacho kutakiwi kukata tamaa. Matatizo uliyonayo hayamanishi sasa huo ndio mwisho wa  Dunia au kila kitu ndo basi katika maisha yako. Unao uwezo wa kubadilisha maisha yako tena kwani zipo fursa nyingi sana ambazo zipo na zinaweza kukufanikisha tena. Anza kuweka mipango yako upya kwa ajili ya baadae badala ya kukata tamaa na kutulia tu. 
Tambua hakuna njia rahisi ya kuelekea kwenye mafanikio. Unatakiwa kujikaza, kuwa na roho ya ujasiri na kujiamini zaidi ili kufanikiwa. Ukikata tamaa maisha yako hakuna tena wa kuyaokoa hapo ndio utakuwa mwisho wako. Upo kwenye mapito tu hujakosea wala kuchelewa katika maisha yako, jipe moyo na songa mbele. 
2. Acha kuficha sana ukweli wa tatizo ulilonalo.
Watu wengi wanapokuwa katika kipindi cha matatizo mara nyingi huwa ni watu wa kujificha na kushindwa kuomba msaada hata wa mawazo kwa watu ambao wana uwezo wa kuwasaidia kabisa.
Kama upo katika wakati mgumu ambao mambo yako unaona yanaenda hovyo hiki ni kipindi ambacho unatakiwa upate msaada mzuri wa ushauri lakini kwa watu ambao wako makini na maisha sio kila mtu. Tafuta mtu ambaye ana uwezo wa kukupa mwanga wa nini cha kufanya katika kipindi chote ambacho upo kwenye wakati mgumu.
3. Acha kufikiria sana juu ya tatizo lililokupata.
Watu wengi wana kawaida ya kufikiri sana juu ya matatizo yao yaliyowapata badala ya kukaa chini kutafuta njia mpya ya kutatua tatizo. Kama una tabia hii nakupa ushauri achana nayo maana itakufanya ushindwe kusonga mbele zaidi.
Ni muhimu kutambua kuwa sisi tulivyo sasa ni matokeo ya mawazo yetu tuliyoyawaza katika  kipindi cha nyuma. Hiyo ina maana kuwa kama utaendelea kuwaza tatizo lako kitakachokupata ni kwamba utaendelea kuwa na matatizo katika maisha yako siku zote. Hauna uwezo wa kubadilisha jana iliyopita, weka mikakati mipya ya kufanikiwa zaidi.
4. Acha kutafuta sana taarifa hasi.
Unapokuwa katika kipindi cha matatizo uliyonayo, hii ni kipindi muhimu kwako ambacho unatakiwa uepuke kutafuta taarifa hasi zaidi. Jifunze sana kutafuta taarifa chanya, taarifa sahihi zitakazo kusaidia kutatua tatizo lako linalokukabili.
Acha kutafuta mchawi nje ya wewe mwenyewe, kumbuka kuna wakati sisi wenyewe tunakuwa tunahusika sana na matatizo yetu kuliko watu wa nje kama ambavyo tunakuwa tunafikiri. Jiulize mwenyewe unahusika kwa kiasi gani na tatizo ulilonalo.
5. Acha kutafuta majibu ya tatizo lako kwa pamoja.
Ni kweli unaweza ukawa upo kwenye matatizo, lakini jifunze kutotafuta majibu yote kwa mara moja juu ya tatizo lako. Kama utafanya hivyo hii itakufanya uwaze sana na kuna uwezekano mkubwa unaweza kushindwa kupata majibu sahihi.
Sikwambii uache kabisa kutafuta majibu ya tatizo ulilonalo hapana, jipe muda wa kutafuta au kushughulikia tatizo lako kwa usahihi. Hii itakusaidia kujua vizuri kama ni uzembe umetokea wapi, kama ni hasara imepotokea wapi? Utafanikiwa kwa hili endapo utajipa muda wa kutatua tatizo lako kwa polepole.
6. Acha kuogopa sana.
Haijalishi ni kitu gani au tatizo gani ulilonalo, habari njema kwako ni kwamba una uwezo wa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yako. Kama uwezo huu wa kufanya mabadiliko unao acha kuogopa sana anza kufanya mambo yako kwa upya tena. Jipange na endelea kufata mipango na malengo yako kama kawaida.
Kuogopa sana eti kwa sababu mambo yako hayaendi vizuri hiyo haitakusaidia kitu zaidi ya kukurudisha nyuma. Watu wote wenye mafanikio wanatabia moja muhimu sana hawaogopi wala hawachoki kujituma. Hakikisha unafata ndoto zako bila woga utafanikiwa.
Hivyo ndivyo vitu muhimu kwako usivyotakiwa kufanya wakati mambo yako yanapokwenda vibaya. Nakutakia mafanikio mema katika safari yako ya maisha. Ansante kwa kutembelea mandao huu wa AMKA MTANZANIA na karibu sana.
DAIMA TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0767048035/ingwangwalu@gmail.com