Kuna njia nyingi za kupata mafanikio makubwa kwenye maisha. Mafanikio yanaweza kupatikana na yeyote ambaye anatumia njia zilizothibitishwa za kuweza kufikia mafanikio makubwa. Ni lazima mawazo yanayoingia kwenye akili yako yawe ya kitajiri ndio uweze kufikia utajiri.
Kumbuka duniani kuna rasilimali nyingi sana za kumfanya kila mtu kuweza kufikia mafanikio makubwa. Rasilimali ya kwanza na kubwa kabisa ni akili yako mwenyewe. Kwa kutumia akili yako unaweza kufanya mambo makubwa sana. Vitu vyote tunavyoviona leo, kwanzia magari, ndege, kompyuta, simu, na vingine vingi vilianzia kwenye mawazo ya binadamu. Watu hawa waliweza kuyafanyia kazi mawazo yao na hatimaye leo tunaona vitu hivi vizuri.
Tumia njia hizi zilizodhibitishwa za kufikia mafanikio na utajiri.
1. Unataka nini kwenye maisha.
Kama unakumbuka kwenye siku ya kwanza kabisa ya siku hizi 30, tulisema cha kwanza kabisa ni kujua ni kitu gani unataka kwenye maisha. Kama unafuatilia vizuri mafundisho haya tayari utakuwa umeshaandika ni vitu gani unavyotaka kwenye maisha. Kama bado, naweza kukuhakikishia kwamba umepoteza siku 18, na hata hizi zinazokuja hutajifunza kitu cha kukubadilisha. Hivyo nakuambia tena chukua kalamu na kitabu chako kisha andika chini kila kitu unachotaka kwenye maisha yako. Andika ni kiasi gani cha fedha unataka, ni nyumba au gari gani unataka, bi kazi au biashara gani unataka na kadhalika.
2. Ujuzi/maarifa.
Kuna vitu vitatu unavyotakiwa kuwa navyo ili kufikia mafanikio; ujuzi/maarifa, uaminifu, na fani.
Bila ya ujuzi au uzoefu huwezi kukamilisha jambo lolote. Lazima ujue jinsi ya kufanya kitu fulani. Lazima uweze kuzalisha kitu ambacho kina thamani kwa watu wengine na wanaweza kulipa fedha ili kukipata. Na pia kuwa na ujuzi bila ya kuutumia ni kazi bure. Hivyo ni lazima uweze kutumia ujuzi ulionao ili kuweza kufikia mafanikioa makubwa.
3. Dhumuni kubwa na zuri.
Ili lengo lolote litimie ni lazima kuwe na dhumuni zuri na kubwa ambalo linakusukuma utimize lengo hilo. Haijalishi unataka fedha kiasi gani, ila kama fedha hizo unazitaka kwa mema na kwa ajili ya kuwasaidia wengine ni lazima utazipata. Ila kama utataka kupata fedha hizo ili kuwakomoa wengine hutaweza kuzipata. Ni muhimu sana kuwa na dhumuni kubwa na zuri la kwa nini unataka unachotaka.
4. Taswira.
Ni lazima uweze kupata taswira ya mambo yale ambayo unayataka. Kila siku pata muda wa kupitia taswira hiyo. Pata taswira umeshapata fedha unazotaka na una kila unachotaka. Pata taswira unasimamia biashara unayotaka, pata taswira umekaa kwenye gari unayotaka au kwenye nyumba unayotaka. Kwa kujenga taswira hii mara kwa mara unajisogeza kwenye mazingira ya kupata kile unachotaka.
5. Tengeneza mwongozo wa mafanikio.
Ni lazima utengeneze mwongozo wako wa mafanikio ili uweze kujua ni wapi unapoelekea. Katika mwongozo huo weka vitu vyote ambavyo unataka na jinsi ambavyo unataka kuwa. Weka imani kubwa kwenye vitu hivyo na ufuate mwongozo huo kila siku.
6. Fikiria makubwa.
Kile unachofikiria ndio unachokipata, fikiri kidogo utapata kidogo, fikiri kikubwa na utapata kikubwa. Hii ni sheria ambayo inafanya kazi kwa kila mtu anayeweza kuitumia.
Tumia kanuni hizi za mafanikio ambazo zimefanya kazi kwa watu wengi na zinaweza kufanya kazi kwako pia. Amini kwenye yale unayotaka na kwenye uwezo wako binafsi na utaona mabadiliko makubwa sana na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.