Ni kweli kwamba kuna nguvu kubwa sana ya uumbaji katika akili yako ya ndani(subconscious mind) ambayo inaweza kukuletea chochote unachotaka. Nguvu hii ni kubwa kama ile inayodhaniwa kuwa nguvu ya majini katika hadithi za Allannin, ambapo unasema kitu na kinatokea.

Leo tutajifunza jinsi unavyoweza kutumia nguvu hii kufikia mafanikio makubwa.

Ili uweze kutumia akili yako hii ya ndani kufikia mafanikio lazima uweze kuipa masharti ya vitu vile unavyotaka. Masharti haya utayaweka kwa njia ya mawazo unayoyarudia kila mara. Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita subconscious mind hupokea na kufanyia kazi mawazo yoyote yanayoingia yawe mazuri au mabaya.

Hivyo ili kuweza kufikia mafanikio makubwa kila siku na kila mara ingiza mawazo ya mafanikio unayotaka kwenye akili yako. Jinsi mawazo haya yanavyokaa na yanavyokuwa ya uhakika ndivyo yatakavyokutengenezea mazingira ya kufikia mafanikio hayo.

Mawazo yanayokufanya mpaka sasa unashindwa kufikia mafanikio.

Kuna mawazo mengi ambayo watu wengi huyaweka kwenye akili zao mara kwa mara. Kupitia mawazo haya watu wengi wameshindwa kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.  Hapa utaona mawazo hayo na jinsi ya kuyabadili na kuweka ambayo yatakufikiasha kwenye mafanikio.

1. Matajiri wanamiliki hela zote na hawaruhusu masikini kuwafikia wao. Haya ni mawazo ambayo wengi wanaamini na yanawafanya washindwe kufikia utajiri.

SULUHISHO; Sio kweli kwamba matajiri wanamiliki fedha zote, fedha zipo nyingi sana ni wewe kuweza kutengeneza thamani itakayowafanya watu wakupe wewe fedha. Weka mawazo haya kichwani kila siku.

2. Umri wangu ni mdogo sana kuweza kufikia utajiri. Wazee wameng’ang’ania nafasi zote hivyo vijana hatuna nafasi.

SULUHISHO; Sio kweli kwamba udogo wako unaweza kukuzuia kufikia mafanikio. Ndio wazee wanaweza kuwa wameshikilia nafasi lakini bado kuna fursa nyingi za wewe kuweza kufikia mafanikio. Zijue na uzitumie.

3. Nimezaliwa kwenye familia masikini, siwezi kuwa na mafanikio makubwa.

SULUHISHO; Kuzaliwa masikini hakutokani na kuzaliwa masikini bali uzembe wako katika maisha. Kuna watu wengi sana ambao wamefikia mafanikio makubwa sana ila wametoka familia masikini sana.

4. Sina elimu ya chuo kikuu hivyo siwezi kuwa tajiri.

SULUHISHO; Elimu ya chuo kikuu ni muhimu sana kwenye baadhi ya taaluma kama udaktari, uinjinia na kadhalika, ila fani nyingi sana hazihitaji elimu ya chuo kikuu bali kufanya kazi kwa juhudi na maarifa makubwa.

5. Umri umeenda sana kutaja kujaribu tena. Ningekuwa na nguvu kama vijana ningeweza kufanya makubwa sana.

SULUHISHO; Sio kweli kwamba umri wako ndio unaokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Kuna watu wengi wamefikia mafanikio makubwa kwa kuanza wakiwa na miaka 50, 60 na hata zaidi. Jua ni kitu gani unaweza kufanya na komaa nacho.

6. Kila kitu kimeshagunduliwa, kila biashara imeshafanywa, sina nafasi yoyote ya kuanza kitu kipya na kufanikiwa.

SULUHISHO; Vitu vilivyogunduliwa ni sehemu ndogo sana ya vitu vinavyoweza kugunduliwa. Kila siku wanasayansi wanakuja na ugunduzi mpya na unaotatua changamoto za binadamu. hivyo bado una nafasi kubwa sana ya kugundua kitu au kufanya biashara ya tofauti. Kama bado watu wana matatizo basi jua fursa bado zipo nyingi sana.

Itumie vizuri akili yako ya ndani ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Kila siku weka mawazo chanya na ya mafanikio kwenye akili yako na itakuweka kwenye mazingira hayo.

Unaweza kuandika sentesi ya kile unachokitana na kila siku kabla ya kulala ukaisoma na asubuhi unapoamka ukaisoma tena. Na unapoisoma weka hisia kali na sema kama vile tayari umeshapata kile unachotaka. Kwa mfano unaweza kuandika; “ninamiliki biashara yenye thamani ya bilioni moja, inayotoa huduma nzuri kwa watu na iliyotoa ajira kwa mamia ya watu” Kwa kutengeneza maelezo hayo vizuri huku ukiitaja biashara unayomiliki, na kuyasema kila siku na kabla ya kulala na baada ya kuamka akili yako ya ndani itakutengenezea mazingira ya kufikia biashara hiyo.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.