Ukiacha uwezo na nguvu za kawaida ambazo tunazo, kila mtu ana nguvu kubwa sana kupitia mawazo yake. Una nguvu zenye uwezo mkubwa wa kiakili ambazo zinaweza kukufikisha kwenye mafanikio makubwa. Kwa kifupi kila mtu ni ‘genius’ yaani una akili nyingi sana ambazo hujaweza kuzitumia bado.

Ubongo wa binadamu una seli za fahamu zaidi ya milioni kumi. Seli hizi zimeungana na kila moja na hivyo kutengeneza miunganiko zaidi ya bilioni moja. Ni katika miunganiko hii ambapo hutokea mawazo makubwa ya uvumbuzi na mafanikio makubwa.

Watu wengi hatujaweza kutumia hata robo ya uwezo mkubwa ulioko ndani yetu. Hata wanasayansi walioonekana kuwa na akili sana wametumia chini ya asilimia ishirini ya uwezo huu. Mtu wa kawaida anatumia chini ya asilimia tano.

Siri moja muhimu ya kuweza kutumia uwezo huu mkubwa.

Kuna siri moja muhimu sana ambayo kama ukiijua na kuanza kuitumia utaanza kutumia uwezo huu mkubwa na hakuna jambo lolote ambalo litakuhsindwa kwenye maisha yako. Siri hii ni rahisi sana na unaweza kuanz akuitumia kesho.

Amka asubuhi na mapema na kitu cha kwanza kufanya chukua kalamu na karatasi, juu ya karatasi andika tatizo linalokuzuia wewe kufikia mafanikio au linalokusumbua kwenye kazi yako, biashara yako au maisha yako ya kifamilia. Au tatizo hilo liwe linawasumbua watu na hakuna anayefikiria kulitatua. Baada ya kuandika tatizo hilo, kaa na ufikirie na uandike majibu ishirini ni jinsi gani unaweza kutatua tatizo hilo. Hakikisha unakaa na kujilazimisha kufikiri mpaka upate majibu ishirini.

Ukiweza kufanya hivi kila siku kwa wiki moja utakuwa na mawazo zaidi ya mia moja kwa mwaka zaidi ya mawazo elfu tano. Katika mawazo haya elfu tano kuna baadhi yatakuwa bora sana na kama ukiweza kuyatumia hakuna atakayeweza kukuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Kwa nini ufanye zoezi hili asubuhi na sio jioni? Kwa sababu asubuhi akili inakuwa imepumzika na pia hakuna usumbufu wa aina yoyote, watu wanakuwa wamelala na hutegemei kupokea simu muda huo.

Kwa nini mawazo ishirini na isiwe matano au kumi? Mawazo matano ni rahisi sana utayapata kwa dakika moja au mbili. Kumi ni rahisi pia kwa dakika tano mpaka kumi utakuwa umeshayapata. Ila mawazo ishirini sio rahisi kuyapata na hii itakufanya uipe akili yako kazi ya ziada ya kufikiri zaidi na jinsi unavyoilazimisha kufikiri zaidi ndio unavyoweza kufikia uwezo wako mkubwa sana.

Nakusisitiza sana ufanye hili kila siku. Tena leo kanunue notebook mpya yenye mistari ushirini kwenye upande mmoja halafu hii iwe kwa kazi hiyo tu ya kuandika mawazo. Fanya hivi kila siku na ninakuhakikishia maisha yako, kazi na hata biashara vitabadilika na kuelekea kwenye mafanikio.

PS.

Tumeanza kufanya zoezi hili kwa wanachama walioko kwenye group la wasap KUAMKA ASUBUHI NA KUJISOMEA na nafikiri baadhi wameanza kuona uzuri wa kitu hiki. Nakushauri na wewe uanze kufanya hivi, hutoi hela yoyote na wala hupotezi muda wowote. Kwa njia hii utajijua zaidi na kujua mzizi wa matatizo mbalimbali yanayokukabili.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.