Jamii nyingi zimekuwa zinamuweka mwanamke katika nafasi ya chini sana ya kuweza kufikia mafanikio. Ukiangalia nchi zote duniani, na hata makampuni makubwa sana duniani ni machache sana ambayo yanaongozwa na wanawake. Hata katika biashara za kawaida, viongozi wengi wa biashara ni wanaume.
Pamoja na harakati nyingi ambazo zimefanyika kuinua hali za wanawake bado sehemu kubwa za uongozi hazishikiliwi na wanawake. Hata ukichukua orodha ya matajiri wakubwa duniani, matajiri wakubwa Afrika na hata matajiri wakubwa Tanzania wachache sana ndio wanakuwa wanawake?
Je tatizo ni nini hapa? Je wanaume wana uwezo mkubwa kiliko wanawake? Leo tutajifunza mbinu ambazo mwanamke yeyote anaweza kuzitumia na akafikia mafanikio makubwa.
Kwanza kabisa mwanamke ana majukumu mengi kuliko mwanaume. Mwanamke anayefanya kazi ana majukumu matatu. Jukumu la kwanza kama mke, la pili kama mama wa familia na la tatu kama mfanyakazi. Kuweza kuendesha majukumu yote haya ili kuweza kufikia mafanikio makubwa inahitaji kujipanga vizuri.
Tatizo kubwa linalowauia wanawake kufika ngazi za juu licha ya kampeni nyingi kufanyika ni kukosa ile dhana ya mapambano. Ukiangalia katika malezi ya watoto wadogo, mtoto wa kiume ataanza kupambana na kushindana akiwa mdogo sana kwenye michezo na wenzake. Michezo kama mpira na mingine inamjengea mtoto uwezo wa kuendelea na mapambano hata anapokuwa mtu mzima. Malezi ya mtoto wakike yapo tofauti kidogo. Watoto wengi wakike michezo yao mikubwa huwa ni ya kuwa peke yao au kuwa na midoli, hivyo hukosa msingi huu mzuri wa mapambano.
Kwenye maisha kuna mapambano mengi sana, lakini wanawake wamekuwa rahisi sana kukata tamaa au kutodhubutu kujaribu. Udhubutu na kutokata tamaa ni vitu muhimu sana vinavyohitajika ili kufikia mafanikio.
Tatizo jingine kubwa kwa wanawake ni kutokuweka malengo na mipango. Kama kuna kitu ambacho tumeshazungumza sana mpaka sasa ni kuhusu malengo na mipango. Huu ni msingi muhimu kabisa wa kufikia mafanikio. Wanawake wengi hawaweki malengo na hata wakiweka huwa hayapo makini na huwa ya muda mfupi. Kwa mfano anaweza kusema malengo yangu ni kuwa namama bora wa familia, au kuwa na fedha za kutosha. Haya ni malengo mazuri lakini hayajakaa kwa umakini sana. Hivyo ni vyema wanawake wakaweka malengo makini, ya muda mfupi na muda mrefu na kujiwekea muda wa kuyafikia.
Je wanawake wanaweza kufikia mafanikio makubwa kwenye biashara?
Kinadharia hakuna tofauti kubwa kati ya uwezo wa mwanaume na uwezo wa mwanamke. Ila mfumo wa jamii umemfanya mwanamke kujiona wa chini au kushindwa kupambana katika mazingira ya kufanikiwa kibiashara. Wanawake wanaweza kufikia mafanikio makubwa sana kwenye biashara kama wanavyoweza kufikia wanaume. Lakini watakuwa na kazi ya kuondoa kwanza mawazo waliyowekewa kwamba hawawezi kama wanaume. Kuna mambo muhimu ambayo mwanamke anatakiwa kufanya ili kufikia mafanikio kwenye biashara;
1. Ni lazima mwanamke awe makini na biashara anayofanya, na sio afanye tu kwa sababu wengine wanafanya au kuonekana.
2. Ni lazima akazane kufanya kazi kwa bidii na maarifa na pia kujifunza zaidi kuhusiana na kile anachofanya na kupuuzia mitazamo ya jamii.
3. Ni lazima awe na shauku kubwa na pia awe na nguvu za kutosha ili kuweza kufanya kazi vizuri.
4. Ni lazima aweze kujiongoza na kujihamasisha ili kuweza kuondoa utegemezi na kuweza kuwa na ubunifu zaidi utakaomletea mafanikio makubwa.
5. Ni lazima awe na uvumilivu ili kuweza kuzivuka nyakati ngumu na vikwazo mbalimbali atakavyokutana navyo kwenye safari.
Nakutakia kila la kheri kwenye kufikia mafanikio makubwa.
TUKO PAMOJA.