Ni vyema kukumbuka kwamba pale tabia za mafanikio zinapokuwa zimejengwa zitaendelea kuwa na wewe mpaka utakapojenga tabia nyingine. Tabia za mafanikio utakazojifunza sasa ukiwa mwanafunzi zitakusaidia katika maisha yako ya elimu na hata maisha yako baada ya elimu.
Hizi hapa ni baadhi ya tabia za mafanikio kwako mwanafunzi.
1. Tengeneza taswira yako nzuri.
Wewe mwenyewe unajionaje? Unajiona kama mwanafunzi bora au mwanafunzi anayeshindwa? Mawazo yako, matendo yako na hata hisia zako zinaendana na jinsi unavyojichukulia wewe mwenyewe. Kama unajichukulia wewe kama mwanafunzi bora utafanya yale yatakayokufanya kuwa bora zaidi na hivyo utapata matokeo mazuri zaidi kwenye masomo yako. Kama unajiona wewe ni mwanafunzi wa kushindwa au usiyeweza utafanya mambo ya kushindwa na utaendelea kupata matokeo mabaya.
Tengeneza taswira yako kwamba wewe ni mwanafunzi bora, na mwenye mafanikio makubwa kwenye elimu. Jione wewe ukipata ufaulu mkubwa na kila siku ishi kama unavyojiona kwenye taswira yako. Kwa kufanya hivi utaona mabadiliko makubwa kwenye tabia yako na hata kwenye masomo yako.
2. Tengeneza na fuata ratiba yako.
Masomo yako chuoni au shuleni yanaenda kwa ratiba, unajua ni kwa nini? Kwa sababu bila ratiba hakuna kinachoweza kufanyika vizuri. Lakini cha kushangaza ni wanafunzo wachache sana ambao wana ratiba. Sasa anza kutengeneza ratiba yako ya kila siku kwa wiki nzima. Jua siku fulani utafanya nini kinachohusiana na masomo yako na kingine kisichohusiana na masomo yako. Hata ratiba ya kujisomea ni muhimu kujua siku fulani unasoma somo fulani. Katika ratiba hii panga ni muda gani utalala na ni muda gani utaamka. Pia weka muda utakaopumzika.
Ukiweza kutengeneza ratiba ambayo utaifuata kila siku utafikia mafanikio makubwa sana kwani hutapanick wakati wa mtihani kwa kuwa hukupata muda wa kusoma. Usipokuwa na ratiba kila kitu utasema unafanya kesho mpaka ratiba ya mtihani inapotoka na kujikuta huna maandalizi ya kutosha.
3. Epuka usumbufu kabla ya kuanza kusoma.
Utakapoweka ratiba yako ya kusoma, kabla ya muda wa kusoma utajikuta unapata usumbufu mkubwa sana. Kuna vitu vingi utaviona ni vyema ukavifanya kwanza kabla ya kuanza kusoma. Ukikubali kufanya vitu hivi hutaweza kusoma na hatimaye utashindwa kufuata ratiba yako. Kuna wakati kusoma kunaweza kuonekana ni kitu kisichovutia kabisa na wakati huu ndio unapata usumbufu mwingi sana kabla ya kusoma.
Usikubali usumbufu wa aina yoyote ukufanye ushindwe kufuata ratiba yako. Ukishapanga ratiba yako iheshimu na ifuate.
4. Jilazimishe kusoma.
Kama tulivyoona hapo juu unaweza kuwa na ratiba yako nzuri ya kusoma ila ukawa hujisikii kabisa kusoma. Wakati kama huu ni rahisi kusema nitasoma kesho na hatimaye kufanya mambo mengine ambayo hayana maana. Usikubali kuingia kwenye mtego huu, kama umeshapanga ratiba ifuate na hata kama hujisikii kabisa jilazimishe kusoma hata kama hutasoma vyote ulivyopanga. Kaa pale na fanya hata maswali au tafuta mwenzako wa kujadiliana nae kuhusu masomo hayo.
Ukiweza kujenga tabia hii ya kujilazimisha kusoma utafika wakati kusoma kwako kunakuwa kama kula. Yaani ukikaa tu unakuwa kwenye mood nzuri ya kusoma.
5. Weka mawazo yako yote kwenye kusoma.
Ukishakuwa na ratiba ya kusoma na ukaanza kusoma hakikisha mawazo yako yote unayaweka kwenye kile kitu unachosoma. Kama unasoma na mawazo yako yako sehemu nyingine unapoteza tu muda wako kwa sababu huwezi kuelewa vizuri. Kama unataka kuelewa sana kile unachosoma kwanza chagua muda ambao ni mzuri kwako kusoma. Kuna watu wanaweza kusoma vizuri usiku, wengine wanaweza kusoma vizuri mchana. Jua muda wako na tenga muda huo kwa ajili ya kusoma. Soma kwenye eneo ambalo halina kelele na ikiwezekana somea kwenye eneo moja kila siku, hii itakufanya kuzoea eneo hilo na hivyo akili yako kujijengea kwamba ikiwa kwenye eneo hilo kazi ni kusoma.
Pia ondoa usumbufu wa simu, redio, tv na vinginevyo. Kuna baadhi ya wanafunzi wanasema wanaelewa vizuri wakisoma na muziki, huu ni uongo labda uwe unafanya marudio.
Kuhusu simu, haijalishi wewe ni mwanafunzi wa sekondari au chuo kikuu au unasomea phd, kusoma ukiwa na simu yako mawazo yako yanakuwa hayajatulia. Unapokuwa katikati ya kusoma halafu ikaingia simu au meseji, ukishapokea simu ile unapoteza ule mlolongo wa kusoma na unapokuja kuanza tena unatumia nguvu nyingi sana. Hivyo zima au weka mbali simu yako wakati unasoma.
6. Kuna tabia nyingine muhimu sana za mafanikio ambazo tunaweza kuzieleza hapa kwa ufupi.
i. Penda kile unachosoma, penda shule/chuo na wapende walimu wako. Kama huwezi kupenda vitu hivyo vinavyohusiana na masomo yako itakuwa shida kwako.
ii. Jiandae vyema, kila siku inapoanza hakikisha umejiandaa kwa ajili ya masomo. Hakikisha una vifaa vyote unavyohitaji kwa ajili ya masomo yako.
iii. Hudhuria darasani, hii itakusaidia kuelewa zaidi yale unayofundishwa.
iv. Wahi mapema kwenye eneo unalotakiwa kuwepo, iwe ni darasani au sehemu nyingine.
v. Soma sana, yaani soma sana. Sio usome haraka bali soma kuelewa. Rudia tena kusoma mpaka uweze kumfundisha mtu mwingine bila ya mashaka. Kusoma ni kazi kama zilivyo kazi nyingine. Na njia pekee ya kufaulu masomo ni kusoma kwa juhudi na maarifa.
Hizo ndio tabia za mafanikio kwa wanafunzi. Kama ukiweza kujenga tabia hizo za mafanikio utaweza kupata ufaulu mkubwa kwenye masomo yako na baadae kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya masomo yako.
TUKO PAMOJA.