Kitu kikubwa kitakachokufikisha kwenye mafanikio sio muda, juhudi au uwezo. Kitakachokuwezesha kufikia mafanikio makubwa ni msukumo wa ndani ambao unaendeshwa na uvumilivu. Msukumo huu na uvumilivu ndio unaokuwezesha kutumia muda, juhudi na hata uwezo wako mkubwa kufikia mafanikio makubwa. Kuna vikwazo vingi sana kwenye safari ya mafanikio, bila ya uvumilivu, haijalishi una juhudi au uwezo kiasi gani, utashindwa kufikia mafanikio.
Njaa ya mafanikio na kuhitaji sana kufikia mafanikio pamoja na uvumilivu ni vitu muhimu vitakavyokufanya uendelee na safari yako ya mafanikio hata pale unapokutana na changamoto au vikwazo.
Kabla ya kutumia uvumilivu ni lazima ujue ni nini hasa unataka kwenye maisha yako. Bila ya kujua kile unachokitaka, hata ukiwa na uvumilivu itakuwa ni kujitesa tu. Kama tulivyosema kwenye siku ya kwanza, jua ni nini unataka na kijue kwa undani, kisha weka malengo na mipango ya kufikia hicho unachotaka.
Tukiangalia masiaha ya watu wengi waliofanikiwa kwenye kada mbalimbali, wote wana kitu kimoja, UVUMILIVU. Watu hawa kuna kipindi walikutana na vikwazo vikubwa ambavyo viliwarudisha wengine nyuma ila wao waliweza kuvumilia na kuendelea.
Hakuna kitu chochote duniani kinachoweza kuchukua nafasi ya uvumilivu, kipaji hakiwezi, dunia imejaa watu wengi wenye vipaji ila hawana mafanikio. Elimu haiwezi, dunia imejaa wasomi wengi ambao hawajafikia mafanikio. Uvumilivu na kujua ni nini unataka ndio nguzo kuu ya kukufikisha wewe kwenye mafanikio.
Wakati unapokutana na changamoto au vikwazo, wakati unapokatishwa tamaa na wakati unapoona mambo hayaendi tena hapa ndio pa kukumbuka kwamba hakuna kitu kiinachoweza kuchukua nafasi ya uvumilivu. Endelea kuvumilia na kung’ang’ania na mwishowe utafikia mafanikio makubwa.
Uvumilivu ni mtazamo kwamba unaweza kufanya.
Ili uweze kuendelea na safari ya kufikia mafanikio makubwa ni lazima uwe na mtazamo wa kwamba unaweza kufanya. Kila jambo unalokutana nalo jua ya kwamba unaweza kulivuka na kuendelea mbele. Tatizo kubwa ni kwamba watu wengi wana mtazamo wa kinyume na huo. Mara zote wanafikiria hawawezi na pale wanapokutana na changamoto wanafikiria hawawezi kuzivuka. Watu wa kawaida wanakubali haraka sana kushindwa, lakini wewe usikubali endelea na mipango yako hata mambo yanapoonekana magumu, kama usipokata tamaa utafikia mafanikio.
Usikubali HAPANA kama jibu.
Mara nyingi kushindwa ni mafanikio yanayojaribu kuzaliwa kwa ukubwa zaidi na uvumilivu ndio utakaokuwezesha kufikia mafanikio hayo makubwa. Watu waliofikia mafanikio makubwa ni kwa sababu walikataa kupokea HAPANA kama jibu. Watu hawa waliambiwa hawawezi au haiwezekani ila wao hawakukubaliana na majibu haya na hatimaye wakafikia mafanikio makubwa.
Usikubali pale mtu anapokuambia haiwezekani au huwezi. Kama ndio malengo yako endelea kufanya bila ya kukata tamaa na utayafikia mafanikio makubwa.
Uvumilivu unafanya kazi pande zote.
Ukitumia uvumilivu kwenye kufanikiwa utafanikiwa na ukitumia uvumilivu kwenye kushindwa utashindwa. Kama utakuwa na uvumilivu kwamba unaweza kufikia mafanikio licha ya kujali hali unayopitia utayafikia. Kama utakuwa na uvumilivu wa mawazo kwamba huwezi kufikia mafanikio au utashindwa ni lazima utashindwa. Hivyo badala ya kung’ang’ania mawazo ya kwamba huwezi au utashindwa anza sasa kuwa na mawazo kwamba unaweza kufanya na kufikia mafanikio makubwa.
Uvuvmilivu ndio kitu kimoja chenye nguvu sana.
Kama huwezi kung’ang’ania na kuvumilia huwezi kufikia mafanikio makubwa kwenye eneo lolote lile. Kama utathubutu kuwa na uvumilivu utaweza kufikia mafanikio makubwa bila ya kujali elimu, kipaji, ushawishi, au hata fedha ulizonazo. Uvumilivu ndio kitu pekee kitakachokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa.
TUKO PAMOJA.