Katika nyakati hizi ujasiriamali umekuwa ukizungumziwa sana katika jamii zetu. Mafunzo memgi ya ujasiriamali yametolewa na watu wengi sana wamehamasika kuingia kwenye ujasiriamali. Vyombo vya habari navyo vimeupamba sana ujasiriamali. Wajasiriamali wanaoonekana kupata mafanikio makubwa wamekuwa wakitumiwa kama mifano kwenye sehemu mbalimbali. Kila siku tunasikia habari kwamba mtu alianza na mtaji kidogo sana lakini sasa anamiliki kampuni kubwa au hata viwanda. Kuna hadithi nyingi za watu walioanzia uchuuzi na sasa ni wamiliki wa makampuni makubwa.

Katika hadithi hizi nzuri na mafunzo ya ujasiriamali watu wengi hawapewei ukweli wenyewe kuhusu ujasiriamali. Tunaangalia watu waliofanikiwa kwenye ujasiriamali lakini hatujiulizi wale walioanza nao mbona wengi wameshindwa. Kuna watu wengi wamefanya ujasiriamali kwa muda mrefu ila hawajafikia mafanikio. Kutokuangalia ni nini kinazuia wengi kufikia mafanikio ndio inapelekea wajasiriamali wengi wapya nao kushindwa kufikia mafanikio waliyopanga.

Safari ya ujasiriamali ni safari ngumu na yenye changamoto nyingi sana. Ukifuatilia kwa undani maisha ya wajasiriamali waliofanikiwa sana utagundua kwamba walipitia nyakati ngumu sana na za kukatisha tama. Katika nyakati hizi wengi walishindwa kuendelea ila hao wachache waliofanikiwa walikubali kuvumilia na kutokukata tamaa. Wale walioshindwa kufikia mafanikio ndio waliokata tama na kushindwa kuendelea kutokana na changamoto mbalimbali.

Leo tutaangalia mambo matatu ambayo yatakupa ukweli halisi wa safari ya ujasiriamali na jinsi gani unaweza kujiandaa na mambo hayo.

1. Utafanya kazi sana.

Moja ya fikra za watu wanaotoka kwenye ajira na kuingia kwenye ujasiriamali ni kwamba wataacha kufanya kazi nyingi na wao kuwa ndio mabosi kwenye ujasiriamali wao. Huu ni uongo kabisa, kwenye ujasiriamali utafanya kazi muda mrefu kuliko ulivyokuwa unafanya kwenye ajira. Kama kazini ulikuwa unafanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni kwenye ujasiriamali utafanya kazi saa kumi na mbili asubuhi mpaka saa nne usiku, na wakati mwingine unaweza kufanya kazi mpaka usiku wa manane. Utalazimika kufanya kazi hata ukiwa nyumbani kwa sababu unaweza kupata simu inayohitaji wewe kuchukua hatua kama mmiliki wa biashara. Hivyo sahau kuhusu kupata muda wa kufanya unachotaka mwenyewe. Utatumia muda mwingi sana kwenye biashara zako wakati wa mwanzo wa biashara.

2. Utashindwa mara nyingi.

Hata ungejiandaa kiasi gani bado utakutana na changamoto ambazo zitakufanya ushindwe au urudi nyuma. Unaweza kujipanga vizuri na ukafanya kila kitu ila kikatokea kitu nje ya uwezo wako na kikakukwaza. Kitu pekee ambacho unaweza kuwa na uhakika nacho kwenye ujasiriamali ni kwamba kuna kushindwa. Kama ukiweza kutumia kushindwa huko kama njia ya kujifunza utajikuta unafanikiwa sana kupitia ujasiriamali. Ila ukikata tama baada ya kushindwa utakuwa umejiondoa kwenye safari ya kufikia mafanikio. Hivyo kufanikiwa ni njia nzuri ya wewe kujifunza njia za kufikia mafanikio.

3. Utavaa kofia nyingi kwa wakati mmoja.

Unapokuwa mjasiriamali hasa wakati wa mwanzo utahitaji kufanya kila idara ya biashara yako. Wewe utakua ndio mkurugenzi, wewe ndio mhasibu, wewe ndio afisa mauzo na masoko, wewe ndio muweka rekodi za biashara yako. Hata kama utaanza biashara kwa mtaji mkubwa bado ni muhimu wewe kujua kila eneo la biashara yako ili ujue ni wapi panahitaji nguvu kubwa ili kufikia mafanikio unayotarajia.

Safari ya ujasiriamali sio rahisi kama tunavyoiona kwenye mafundisho au taarifa mbali mbali. Kuna changamoto nyingi sana ambazo kama utakuwa hujajiandaa vizuri zitakukatisha tama na uone haiwezekani wewe kufikia mafanikio. Jifunze kuwa na uvumilivu na endelea na mipango yako hata mambo yanapokuwa magumu. Tumia makosa unayofanya na kushindwa kwako kama sehemu ya kujifunza ili kuwa bora zaidi baadae. Unaweza kufikia mafanikio makubwa kupitia ujasiriamali, jiandae na anza kufanya kazi kwa bidii na bila ya kukata tamaa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio kupitia ujasiriamali.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.