Hata uwe na mipango mikubwa na mizuri kiasi gani ya kufikia mafanikio, kama hutakuwa na afya nzuri ni vigumu sana kuweza kufikia mafanikio makubwa. Na kama kwenye safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio utaisahau afya yako, hata ukifanikiwa halafu afya yako ikawa mbaya hutaweza kuyafurahia mafanikio yako.
Ili kuweza kufikia na kufurahia mafanikio yako ni muhimu sana kujali afya yako. Ili kujenga afya bora ni muhimu kuangalia sehemu zifuatazo.
1. Akili.
Ili kuweza kufikia mafanikio makubwa unahitaji kuwa na afya ya akili. Na ili kuwa na afya ya akili ni muhimu kuweka mawazo mazuri kwenye akili yako na kujijengea shauku ya kufikia mafanikio. Magonjwa, kukata tamaa na hata vikwazo vingine vyote vinaanzia kwenye akili. Hivyo linda afya yako ya akili ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.
2. Tunza nguvu za mwili wako.
Ukweli ni kwamba ulianza kuzeeka siku ulipozaliwa. Yaani kila siku inayoisha unazidi kupunguza siku zako za kuishi duniani. Na jinsi umri unavyokwenda ndivyo nguvu nazo zinakwisha. Ni vyema kutunza nguvu zako na kujua matumizi sahihi ili uweze kufikia mafanikio. Kama tulivyoona kwenye makala za nyuma, huwezi kufanya kila kitu. Na pia unaweza ukafanya mambo mengi na ukachoka sana ila ukakuta yana faida kidogo sana kwako. Hivyo jua ni kitu gani kinatumia nguvu zako na kiwe kina manufaa kwako.
3. Pumzika.
Mwili wako unahitaji kupumzika ili uweze kufanya kazi vizuri. Wakati huu wa mapumziko ndio mwili wako unapata nafasi ya kurudisha vitu vilivyotumika na kuisha. Ufanisi wako unaongezeka sana kama ukipata muda wa kutosha wa kupumzika.
4. Kunywa maji.
Mwili wako unahitaji sana maji kuliko kitu kingine chochote. Sehemu kubwa ya mwili wako ni maji na unapokosa maji ni kama unauchosha mwili wako. Kunywa maji ya kutosha kila siku ili uweze kuwa kwenye ufanisi wa hali ya juu.
5. Chakula.
Sio kila kitu unachokula ni kizuri kwa afya yako. Na kwa bahati mbaya sana sehemu kubwa ya vyakula unavyokula vinakuua taratibu. Vyakula hivyo vinakutengenezea sumu na vingine vinakuletea maradhi. Kula mlo kamili wenye virutubisho vyote muhimu. Kwa mtu mzima epuka mafuta mengi na pia epuka wanga mwingi. Ukitumia vyakula hivyo kwa wingi vinakwenda kutengeneza mafuta kwenye mwili na hivyo kuwa na uzito mkubwa na baadae shinikizo la damu au magonjwa ya moyo.
6. Fanya mazoezi.
Hiki ni kitu muhimu sana ili kuendelea kuwa na afya bora. Vyakula vingi tunavyokula havitumiki na mwili hivyo usipofanya mazoezi vyakula hivi huhifadhiwa na hatimaye kuleta madhara. Pia mazoezi yanaufanya mwili uwe mchangamfu na kuimarisha kinga ya mwili hivyo kuimarisha mwili kujikinga na magonjwa.
7. Epuka na tatua msongo wa mawazo.
Msongo wa mawazo ni tatizo ambalo tunakutana nalo mara kwa mara. Kwenye kazi zetu, biashara na hata maisha ya kawaida, kuna wakati tunakutana na changamoto ambazo hutuletea msongo wa mawazo. Ni lazima uwe na njia nzuri za kuepuka msongo wa mawazo au kukabiliana nao pale unapotokea. Fungua hiyo link hapo juu kujifunza zaidi kuhusu msongo wa mawazo.
Haya ndio mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu afya yako. Anza kuyafanya mambo haya kila siku ili kuweza kuimarisha afya yako na kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya mafanikio.
TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.