Kanuni ambayo huwezi kuipinga na hata ukijaribu kuipinga, haiwezi kufutika, ni ile ya kwamba, kile ambacho mawazo yanaweza kukifikiri, yanaweza kukiumba pia. Hii ni kanuni inayoyafanya kazi katika maisha yako kila siku na kuleta matokeo yoyote yale kwa kile unachokifikiria na kukizingatia sana kila wakati uwe unakitaka au hukitaki .  Ni kwa vipi kanuni hii inafanya kazi?
 

Chochote ambacho mawazo yako ya kawaida yanakiona, yanakiamini na kukihisi, huchukuliwa na kupelekwa kwenye mawazo ya kina, ambayo ndiyo yanayowezesha mambo yote kuwa au kufanyika. Hata sala zetu huwa zinafanyiwa kazi kwenye mawazo ya kina.
Mawazo ya kina yanapopokea taarifa kutoka kwenye kufikiri kwako, huanza kufanyia kazi kile unachofikiri katika hali halisi. Mawazo ya kina kwa kawaida huwa hayajali yamepokea taarifa ya namna gani, yanachojua ni kufanyia kazi taarifa iliyopekelewa iwe mbaya au nzuri. Ni mawazo ambayo hayana akili, hayahoji kitu bali yanafanyia kazi taarifa tu unazozipeleka kwenye ubongo wako.
Kwa hiyo, unapofikiria unaweza, utaweza kweli na itafanyika, pia kama unafikiria huwezi kufanya kitu katika maisha yako na kuleta mabadiliko ni kweli kabisa hautaweza, hivyo ndivyo itakavyokuwa. Lakini, kwa bahati mbaya kufikiri kwa kuamini tu peke yake hakutoshi, bila kufanyia kazi unachofikiria na kukiamini.

  
 

Ni lazima ufanyie kazi unachokifikiria ili uweze kuleta matokeo makubwa na kuvuna utajiri wa kutosha kupitia ubongo wako. Unaweza ukaona kama ajabu vile, lakini hili halina ubishi mawazo yako ya kina yana nguvu kubwa sana ya kuzalisha chochote unachokitaka. Kila mmoja wetu angejua namna ya kuyatumia vizuri mawazo haya dunia isingekuwa hapa ilipo.
Kwa kupitia mawazo haya ya kina unaweza ukavuta mafanikio unayoyataka iwe pesa, fursa au ‘bahati’ kama wengi wanavyofikiri, ili mradi tu ujue namna gani unavyoweza kuyatumia mawazo hayo na kukuletea mafanikio makubwa katika maisha yako. Unaweza ukawa unajiuliza utatumia vipi ubongo wako au mawazo ya kina kukuletea mafanikio unayoyataka?
Hicho ni kitu rahisi sana, ili uweze kujenga utajiri unaoutaka kupitia ubongo wako kitu muhimu unachotakiwa kufanya na kikakuletea matunda ya haraka ni kuielekeza akili yako kwa mambo unayoyataka yakutokee kwenye maisha yako na si vinginevyo. Ukiweza kufanya zoezi hili dogo tu utapa kile unachokihitaji katika maisha yako. 
( Unaweza Ukasoma Pia Kanuni Ya Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako )
Je, katika maisha yako unaielekeza akili yako kwenye mambo gani? Ni jambo la muhimu sana kujua jinsi unavyoitumia akili yako. Ukweli ni kwamba, unapojifunza mbinu sahihi za kuitumia akili yako, unakuwa upo kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko ambavyo unavyofikiri.
Iwapo utaielekeza na kuifundisha akili yako itazame na kufanikisha malengo yako uliyojiwekea, basi ni wazi kabisa kwamba utajiweka mahali ambapo mafanikio yanapatikana kwako. Kinyume chake ni kupoteza fursa zote za mafanikio zilizoko mbele yako.
Ili kufanikisha hili, Unapaswa kuhakikisha kwamba, akili yako inatazama matokeo ya jumla na ya mwisho yanayohusiana na malengo yako uliyojiwekea. Kama lengo lako ni kutengeneza kiasi cha shilingi laki saba ndani ya wiki mbili, hakikisha hizo pesa uwe unaziona kama vile tayari unazo.
Pia kama lengo lako ni kujenga nyumba hakikisha hiyo nyumba unaiona kwenye ubongo wako na uwe unapiga picha kama unaishi vile kwenye nyumba hiyo na kuna kila kitu unachokihitaji ndani yake. Hayo ndiyo matokeo ya jumla yanayohusiana na malengo yako, unaweza ukaona kama ujinga hivi lakini ndio kanuni inafanya kazi. 
Unapotazama matokeo ya jumla kuna kuwa kunakufanya uchukue hatua muhimu na madhubuti za kuhakikisha kwamba, unakamilisha malengo na majukumu uliyojiwekea. Na vilevile unaposhindwa kuyatazama matokeo hayo ya mwisho, inakuwa ni rahisi kwako kuyumba na kuacha kutekeleza malengo yako pale unapokabiliana na changamoto.
Ni wazi kabisa kuwa, iwapo utashindwa kuielekeza akili yako vizuri kwa mambo unayoyataka, mawazo yako hayo ya kina hayataweza kukutengenezea fursa au utajiri unaoutaka katika maisha yako. Matokeo yake utajikuta umeishia mahali ambapo hupataki katika maisha na kujikuta ni mtu wa kulaumu.
Ni vizuri kuifundisha akili yako, ili iweze kukupeleka kule unakotaka kwenda kimaisha. Akili yako inaweza ikafananishwa na dereva wa gari. Hivyo, unao wajibu wa kuipa maelekezo sahihi na hatimaye mawazo yako ya kina yatafuata maelekezo hayo kwa kuibua na kutengeneza fursa mbalimbali za mafanikio kwako.
Kama utafikiri kwa usahihi na kuielekeza akili yako kwenye malengo yako, huna sababu ya kutokuwa tajiri. Kikubwa, jifunze kumudu mawazo yako kwa kuwaza tu, yale unayotaka yakutokee katika maisha yako na siyo yale ambaye huyataki. 
Acha fikra za kuamini eti kwamba kuwa maskini ni kuandikiwa, hakuna kitu kama hicho hizo ni fikra zinazokurudisha na kukwamisha sana. Kila mtu ana uwezo wa kuwa tajiri kama akitaka na kukubali kulipia gharama. 
Unatakiwa kuwa na dira ya mawazo sahihi ambayo unatakiwa uifate kila siku ili ufanikiwe. Unastahili kuwa tajiri acha kujiambia huwezi tena, kufanikiwa kwako ni lazima.  Acha kulia njaa kila siku na kulaumu, unaoutajiri mkubwa katika maisha yako sema hujijui tu.
Kama ni kupewa umepewa kila kitu ambacho kipo kwenye mawazo yako cha kukutoa sehemu moja na kukupeleka sehemu nyingine unayotaka. Kitu cha msingi, elewa namna ya kuyatumia hayo mawazo yako kukupatia chochote unachokihitaji. 
Hivyo ndivyo unavyoweza kutumia ubongo wako kukupatia utajiri unaoutaka. Nakitakia ushindi katika safari yako ya mafanikio, hakikisha  unaendelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza mambo mengi mazuri kwa faida ya maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU-  0767048035/ingwangwalu@gmail.com