Kwa siku 30 zilizopita kila siku ulikuwa unapata makala moja ikielezea mbinu za kufikia mafanikio makubwa kwenye kile unachofanya. Tumejifunza njia za kufikia mafanikio, siri za kufikia mafanikio na utajiri, siri za mafanikio kwa wanawake, siri za mafanikio kwa wanafunzi na hata siri za afya bora ili kufikia mafanikio makubwa. Kama umezisoma makala hizi zote na kama umezingatia yale uliyojifunza sasa hivi wewe ni mtu tofauti kabisa na utafikia mafanikio makubwa sana.
Kama hukuweza kusoma makala zote tafadhali chukua muda wako kuzisoma zote kwa kubonyeza maandishi haya. SIKU 30 ZA MAFANIKIO.
Kumbuka mabadiliko utakayofanya sasa utaanza kuona matunda yake baadae kidogo. Hivyo usikate tamaa pale unapoanza kufanya mabadiliko halafu huoni matokeo makubwa kwenye maisha yako. Kama tulivyojifunza kwenye siku hizi 30 unahitaji kuwa na uvumilivu ili kufikia mafanikio makubwa.
FURAHA, FURAHA, FURAHA…..
Tutahitimisha siku hizi 30 za mafanikio kwa kuangalia kitu ambacho kila binadamu anapenda kuwa nacho ila wachache ndio wanakipata. Kitu hiki ni FURAHA. Furaha ndio hitaji kubwa la kila binadamu. Tunafanya kila tunachofanya ili kuwa na furaha kwenye maisha yetu.
Mahitaji makubwa ya kuwa na furaha ni;
1.Kuwa na kitu cha kufanya.
2. Kuwa na kitu cha kupenda.
3. Kuwa na kitu cha kutumaini.
Furaha sio kitu ambacho unapewa bali ni kitu ambacho tayari kipo ndani yako. Hiki ni kitu ambacho unakigundua wewe mwenyewe kutokana na maisha yako unayoishi. Furaha haitokani na vitu ambavyo unamiliki ila jinsi gani unavichukulia vitu hivyo unavyomiliki. Furaha inatokana na ile hali ya kujali na kushukuru kw akile ulichopata.
Kuna watu wanaomiliki mali nyingi ila hawana furaha na wakati huo huo kuna watu ambao hawana umiliki wa vitu vingi ila wana furaha kwenye maisha yako.
Hapa hatuzungumzii zile kauli kwamba matajiri wana hela ila hawana furaha na kwamba masikini hawana hela ila wanafuraha, huu ni uongo kabisa. Kuna matajiri wengi wenye hela na wanafuraha na kuna masikini wengi mno hawana hela na hawana furaha kabisa na maisha yako. Hivyo wewe ambaye tayari ni yajiri au unaelekea kwenye utajiri nataka uwe na furaha pia na hapa ndio utajifunza jinsi ya kupata furaha hiyo.
Furaha inatokana na wewe kujali na kushukuru kwa kile ambacho umekipata na unachomiliki. Furaha inatokana na wewe kutoa zaidi kwa ajili ya wengine. Na furaha inatokana na wewe kujikubali na kujua kwamba wewe mwenyewe ndio unawajibika kwa maisha yako na furaha yako. Kama unafikiri kuna mtu ambaye anaweza kukuletea furaha umepotoka, kama wakati huna hela hukuwa na furaha usifikiri utaipata ukishapata hela. Furaha inaanzia ndani yako.
Hisia zinazoharibu furaha.
Kuna hisia ambazo zinawanyima watu furaha au zinaharibu furaha ya watu. Hisia hizo ni;
1. hofu
2. hasira
3. chuki
4. majivuno
5. wivu.
Hisia zote hizi ziko chini ya uwezo wako na hivyo unaweza kuzidhibiti. Hakikisha unaondoa kabisa hisia hizo kwenye mawazo yako ili uweze kufurahia furaha ya kweli.
Vitu muhimu vya kuishi navyo.
Kuna jinsi ya kuishi ambayo itayafanya maisha yako kuwa na mpangilio mzuri na kuwa na furaha. Jinsi hii ya kuishi inatokana na mambo muhimu ambayo unatakiwa kuyafanya kwenye maisha yako. Mambo hayo ni;
1. kazi
2. sala
3. upendo
4. burudani.
Hivi ni vitu muhimu sana kwenye maisha yako, ni muhimu kufanya kazi ili kupata kipato na kuweza kuendesha maisha. Ni muhimu kufanya sala kulingana na imani yako ili kuweza kujijenga zaidi kiroho na kiimani. Ni muhimu kuwa na upendo kwa wengine ili nao wawe na upendo kwako. Na pia ni muhimu sana kupata burudani ambayo itakufurahisha na kukupumzisha.
Furaha pia inategemea uadilifu na uaminifu. Usipokuwamuaminifu huwezi kuwa na furaha. Ukiwadhulumu wengine hata kama utapata fedha nyingi kiasi gani bado huwezi kuzifurahia kwa sababu unajua hujazipata kihalali. Hivyo kuwa muaminifu na muadilifu ili kuweza kufurahia maisha yako.
Tumia haya yote uliyojifunza kwa siku hizi 30. Kama utayasoma mambo haya na kuachana nayo hakuna chochote kitakachotokea kwenye maisha yako. Ila kama utayasoma, kuyazingatia na kuyafanyia kazi kwenye maisha yako utaona mabadiliko makubwa na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
TUKO PAMOJA.