FEDHA: Hiki Ndicho Kitu Kinachosababisha Pesa Unayotafuta Isikae Mkononi Mwako.

Pesa ni sehemu ya maisha yetu, tena maisha ya kila siku. Ni mara chache sana kwa siku kupita bila mtu kutumia pesa au kufikiria kupata pesa na jinsi ya kuitumia. Kutokana na umuhimu huu wa pesa katika maisha yetu, kila mtu hujikuta yupo katika harakati za kutafuta pesa kwa namna moja au nyingine mpaka ipatikane.

Kila kukicha shughuli karibu zote unazoziona zinaendelea mara nyingi zinahusiana pesa. Kila mtu wazo la pesa limekuwa liko mbele zaidi na kuwaza afanye nini ili apate pesa zaidi za kuongoza maisha yake baadae. Kwa sababu ya pesa binadamu hujikuta anafanya kila kinachowezekana kwake ili mradi tu apate pesa.
Pamoja na jitihada zote hizo za kutafuta pesa, hata hivyo kuna wakati pesa hiyo inapopatikana huwa haitulii mkononi. Hiki huwa ni kitu cha ajabu kidogo na kinawashangaza wengi kwanini pesa haikai mikononi mwao. Utakuta leo umepata kiasi Fulani cha pesa ambacho ni kikubwa lakini baada ya siku chache tu unajikuta huna hiyo pesa.
Hali hii inapotekea, wengi huwa wanajiuliza sana na kuanza kutafuta mchawi anayesababisha pesa kupotea. Wengi kwa kutojua hujikuta wakiamini wamelogwa au wana mikosi ndiyo inayosababisha pesa isikae na kutulia mikononi mwao. Hiki huwa ni kipindi kigumu kwa wengi, ambacho husababisha wengine wakate tamaa na kuamua kuishi maisha ya bora liende.
  
Kama katika maisha yako umepitia au upo katika kipindi hiki cha pesa kutokukaa mikononi mwako, nataka nikupe moyo na uhakika hujalogwa, huna mkosi wala balaa ila kuna kitu kinachosababisha pesa isikae mkononi mwako. Hiki ni kitu ambacho hukijui, ingawa leo nataka wewe ukijue ili uweze kutimiza ndoto zako ambazo zimekwama kwa muda mrefu sasa kwa sababu ya pesa.
Kitu pekee kinachosababisha pesa yako isiweze kutulia ni kwamba wewe haupo katika kiwango cha mtikisiko sawa na fedha. Pengine unajiuliza huu mtikisiko ni nini? Najua hiki ni kitu kigeni kwako ambacho kinahitaji ufafanuzi kiasi ili uweze kunielewa ni kwa namna gani haupo katika kiwango cha mtikisiko na fedha?
Kwa kawaida kila kitu katika maumbile huwa kina tabia ya kutikisika (movements) wakiwemo binadamu na fedha. Vitu vinavyoshabihiana huitika kwa vile vya mwelekeo wake, hii ikiwa na maana kwamba vitu hivyo hutikisika kwenye kiwango cha masafa ya aina moja. 
Sasa ni vipi wewe unaweza kuwa katika kiwango cha mtikisiko sawa na fedha ili uweze kuvuta pesa zaidi na hatimaye kuwa tajiri? Hebu kwanza tutazame kile tunachokijua kuhusu kutikisika. Wakati tunapokuwa na matumaini, watu wenye matumaini na matukio ya matumaini huja upande wetu, kwani wakati huo kiwango chetu cha mtikisiko huwa kinawiana na kiwango cha watu hao.( Soma Kanuni Ya kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha)
Wakati tunapokuwa na hisia za kukata tamaa, tunavutia matukio na watu wenye kukatisha tamaa upande wetu, kwani wakati huo tunakuwa kwenye eneo la viwango vya chini vya mtikisiko, ambavyo vinawiana na vya hao wengine.
Hivyo siku zote , vitu vinavyofanana huvutika upande wa vitu vinavyofanana navyo, hii ni kanuni ya maumbile isiyokwepeka. Hisia zetu huathiri viwango vyetu vya kutikisika, hivyo tunajihisi tusio na furaha na tulio na simanzi, ni kwa jinsi tutakavyohisi kwa namna hiyo, ndivyo viwango vyetu vya kutikisika vitakavyozidi kuwa chini.
Ili kuweza kuwa katika kiwango cha mtikisiko kama zilivyo fedha na kuondokana na tatizo la pesa kutotulia mkononi, tunahitaji kutazama sana kile kinachofanywa na fedha kwenye hisia zetu, kwa sababu ni namna tunavyoishi ndani yetu ndiko kunakoathiri kiwango chetu cha mtikisiko.
Inawezekana mtu ukawa hutengenezi pesa nyingi, lakini ni vema kukiri kwamba, unapopata hizo pesa hata kama ni kidogo ujisikie vizuri. Acha kuwa na simanzi unavyokuwa na simanzi unakuwa na mtikisiko mdogo hatimaye unaosababisha hata pesa kidogo ulizonazo zitoweke mikononi mwako.
Kumbuka unapokuwa na hisia za furaha unakuwa upo katika kiwango cha juu cha mtikisiko kinachosababisha uvute pesa na fursa nyingi. Na unapokuwa na hisia nyingi za huzuni, simanzi, kuwa na wasiwasi kuhusu pesa unakuwa unajiweka katika mtikisiko wa chini hali inayosababisha uendelee kukosa pesa katika maisha yako.
Wakati unapoendelea kuwa na hali ya furaha na kuepuka mawazo ya kukata tamaa, utajikuta unavuta mtikisiko wa juu, hali itakayopelekea uzidi kuvuta mambo mengi mazuri ikiwemo na pesa. Unaweza ukazidi kuongeza mtikisiko wako kwa kutumia mbinu ya kujifikiria akilini mwako kama unayepata kiwango kikubwa cha fedha na ujaribu kuzama kwenye hisia hizo.
Kwa kadri utakavyoweza kufanya hivi na kuegemeza hisia zako kikamilifu kwenye hili, ndivyo utakavyo kuwa unakaribia kutikisa kwenye kiwango ambacho fedha hutikisika na utakuwa umeachana na tatizo la pesa kutokaa mikononi mwako.
Chukua hatua juu ya maisha yako, hivyo ndivyo unavyoweza kuwa katika kiwango cha mtikisiko sawa na fedha. Ili kupata maarifa kama haya zaidi yatakayokuweka huru kifedha hakikisha unajiunga na KISIMA CHA MAARIFA bila kukosa, kumbuka kuanzia wiki ijayo ndani ya KISIMA CHA MAARIFA tutaanza uchambuzi wa kitabu RICHEST MAN IN BABYLON. 
Nakutakia ushindi katika safari yako ya uhuru wa kifedha.
DAIMA TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU- 0767048035/ingwangwalu@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: