Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD.

Leo tunaendelea kujifunza hatua kumi za kufuata ili kuanza safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha.

8. Hatua ya nane; ASSET zinanunua vitu vya anasa.

Robert anasema ni vigumu sana kuwekeza kwenye assets kwa sababu kuna vishawishi vingi sana vya watu kununua vitu vya anasa. Vitu kama magari mazuri na nyumba nzuri za kifahari zinawafanya wengi kuwa na matumizi makubwa kuliko uwekezaji na mbaya zaidi wanakopa ili kupata vitu hivyo. Robert anasema hata yeye anapenda kununua vitu vya anasa ila havinunui kwa mkopo. Anasema kama anataka kununua gari zuri, anaangalia ni sehemu gani akiwekeza fedha zake ili ziweze kumpatia faida ambayo itamwezesha kununua gari hilo. Badala ya kuchukua mkopo na hivyo kuwa na madeni zaidi anatengeneza uwekezaji ambao utamlipa zaidi. Robert anasema watu wengi wanakopa fedha kununua vitu wanavyotaka, ni kitu rahisi kwa muda mfupi ila kwa muda mrefu ni kitu kigumu sana. Uwekezaji ili kununua vitu vya anasa ni kitu kigumu mwanzoni ila kwa muda mrefu ni kitu kizuri sana. Njia rahisi baadae inakuwa ngumu na njia ngumu baadae inakuwa rahisi. Fedha ni nguvu kubwa sana, ukiweza kuitumia vizuri utapata uhuru mkubwa.

9. Hatua ya tisa; uhitaji wa mashujaa.

Robert anasema alipokuwa mdogo alikuwa anapenda mchezo wa baseball. Na hivyo alijifunza mambo mengi sana kuhusu wale ambao wamefanikiwa kwenye mchezo huo. Alijifunza ni jinsi gani wanacheza, ni kiasi gani wanalipwa na ni maisha gani wanaishi. Na hata alipokuwa anacheza mchezo huo hakujiona kama yeye mwenyewe bali watu wale ambao walikuwa mashujaa wake. Robert anasema hii ni njia nzuri sana ya kujifunza ambayo tunaipoteza tunapokuwa watu wazima.

Robert anasema hata baada kukua amekuwa na mashujaa wengine kwenye maswala ya biashara na uwekezaji. Amekuwa akijifunza kuhusu Warren Buffet, Donald Trump na wengine wengi. Anasema anasoma kila kitu ambacho Warren Buffet amewekeza. Na anasoma vitabu vya wafanya biashara wengi ambao wamefikia mafanikio makubwa. Robert anasema kw akuwa na mashujaa mtu anasukumwa kutumia uwezo wake mkubwa kufikia mafanikio makubwa. Mashujaa wanafanya mambo yaonekane rahisi na yanawezekana, kama wao wameweza na wewe unaweza pia na hivyo kuweka juhudi zaidi.

10. Hatua ya kumi; Fundisha na utapokea(toa na utapokea).

Robert anasema baba zake wote walikuwa wanafundisha. Rich dad alimfundisha kuhusu ulimwengu wa fedha na biashara wakati Poor dad alimfundisha kuhusu ujuzi wa kawaida. Rich dad alimfundisha Robert kwamba kama unataka kitu, toa kitu hiko na utakipata kwa wingi sana. Kama unataka fedha, toa kwanza fedha na utazipata nyingi sana. Anasema Rich dad alipotaka fedha zaidi alitoa fedha kama msaada kwa wasiojiweza na hii ilimfanya kupata fedha nyingi sana.

Robert anasema kama ni wazo moja analoweza kukupa ni toa na utapokea. Anasema kwake inafanya kazi kila mara, kama anataka kitu anakitoa kwanza na baadae anakipata kwa wingi mno. Anasema sheria ya kutoa na kupokea iko sahihi na inafanya kazi.

Rich dad alimwambia Robert kwamba watu masikini wana tamaa ya fedha kuliko watu matajiri. Anasema watu matajiri kuna kitu wanakitoa kwenye jamii zao lakini watu masikini mara nyingi hawana cha kutoa na ndio maana hawapati zaidi. Robert anatumia mfano kwamba kama utaweka kuni au mkaa na kuziambia nipe moto na mimi nitakupa kuni zaidi hakuna kitakachotokea. Ila kama utazipa kuni hizo moto kidogo zitakupatia moto mwingi sana, hivyo kumbuka toa na utapokea. Linapokuja swala la fedha, upendo, na hata biashara, toa kwanza kile unachotaka na utapata zaidi.

CHUKUA HATUA.

Kila mmoja wetu amepewa zawadi kubwa mbili, akili na muda. Ni juu yako kuhusu jinsi unavyoweza kutumia zawadi hizi mbili kufikia mafanikio. Kila fedha inayopita kwenye mkono wako una uchaguzi wa kuitumia kufikia mafanikio au kuendelea kuwa na maisha magumu. Una uchaguzi wa kuitumia hovyo na kuendelea kuwa masikini au kuiwekeza na kuanza kupata faida na kuelekea kwenye uhuru wa kifedha. Hatua ya kwanza kuwekeza ni kuwekeza kwenye akili yako, kujifunza zaidi kuhusu kile unachofanya, unachotaka kufanya au unachotaka kuwekeza.

Kila siku na kila shilingi unayopata unaamua kuwa tajiri au unaamua kuendelea kuwa masikini. Huu ni uchaguzi ambao umekuwa unafanya kila siku. Endelea kujifunza na kuwekeza ili kufikia uhuru wa kifedha. Chagua kutumia elimu hii na kuifunzisha kwa watoto wako ili nao wakue wakielewa vizuri elimu ya fedha. Usipofanya wewe hakuna atakayefanya, maisha yako na ya watoto wako yatategemea maamuzi utakayofanya leo na sio kesho au siku zijazo.

Huu ndio mwisho wa uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD. Kwa takribani miezi miwili tumejifunza mengi sana katika uchambuzi wa kitabu hiki. Kama utayatumia haya uliyojifunza utaanza kuelekea kwenye uhuru wa kifedha. Kumbuka kuwa masikini au kuwa tajiri ni uchaguzi wako mwenyewe.

Fanya uchaguzi sahihi sasa na ishi nao ili uweze kufikia uhuru wa kifedha. Kama ulikosa makala yoyote kati ya makala hizi unaweza kuzisoma zote hapa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia uhuru wa kifedha kwako mwenyewe na kwa familia yako kwa ujumla.

Wiki ijayo tutaanza uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON ni kitabu kizuri sana kuhudhu fedha, kuzipata, kuzitunza na kuziwekeza zaidi. Kama Robert alivyosema kwenye kitabu chake, hiki ni moja ya vitabu vilivyomfundisha kuhusu mambo ya fedha.

TUKO PAMOJA.