Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia malengo yetu.

Leo tutazungumzia changamoto ya kuanza biashara kwa mtaji wa kukopa.

Watu wengi sana wanapenda kufanya biashara au kujiajiri. Na kikwazo kikubwa cha watu hawa ni mtaji kama wanavyosema wenyewe, mimi huwa sikubali kauli hii kwa sababu mtaji ni kisingizio tu. Tatizo kubwa mpaka sasa hujaanza biashara ni kutokujua vizuri ile biashara unayotaka kufanya.

Kuna njia mbalimbali za kupata mtaji wa biashara. Unaweza kutumia fedha zako mwenyewe ulizoweka akiba, unaweza kupewa au kuchangiwa na watu wako wa karibu na pia unaweza kuomba mkopo wa kibiashara.

Je ni vyema kuanza biashara kwa mtaji wa kukopa? Kabla hatujajibu swali hili hebu tuone maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kuhusiana na hili;

Nilikosa kianzio yaani mtaji nikakimbilia mkopo ambao nimekamilisha taratibu nategemea kuupokea hivi karibuni ili nianze biashara ila umenitisha kwa mafundisho na ushauri yakuwa mpaka niwe na mtaji wangu mwenyewe nifanyeje?

Ni kweli kabisa ya kwamba haishauriwi kuanza biashara na mtaji wa kukopa hasa pale unapokopa kwenye taasisi za kifedha zinazohitaji marejesho haraka na riba kuwa kubwa kidogo. Ni kwa nini haishauriwi hivi?

1. Unapoanza biashara kuna mambo mengi ambayo unakuwa hujayajua bado na hivyo kukutana na changamoto nyingi sana mwanzoni. Kama umeanza na mtaji wa kukopa unaweza kujikuta unaingia kwenye matatizo.

2. Taasisi zinazotoa mikopo zinahitaji uanze kurejesha mkopo mapema. Unapochukua mkopo baada ya miezi michache watakutaka uanze kurejesha mkopo huo. Ni vigumu sana kwa biashara kuweza kusimama chini ya miezi sita na hivyo utajikuta unachukua mtaji na kurejesha, kitu ambacho kitazuia kukua.

3. Riba ya taasisi nyingi ni kubwa kidogo. Kama unachukua mkopo kwenda kuanza biashara, mwanzoni unaweza kuwa hupati faida kubwa sana au hupati faida kabisa. Wakati huo huo unatakiwa kurejesha mkopo ambao una riba kubwa kidogo. Kwa kufanya hivi utakuwa unazungusha tu fedha kwenye mikono yako.

Wakati sahihi wa kuchukua mkopo nu pale unapokuwa umeona biashara yako imeanza kutengeneza faida na hivyo kutaka kuikuza zaidi.

Ni kutokana na changamoto hizi ndio maana kuna sheria kwamba taasisi za kifedha zinakopesha watu mikopo ya kibiashara kwa wale ambao tayari wako kwenye biashara hiyo angalau miezi sita.

Sio kwamba hawawapendi hawa ambao wanaanza ila hawataki kuwaingiza kwenye matatizo ambayo yako wazi.

Ufanye nini kwa wewe ambaye tayari umeshaingia kwenye mkopo wa kuanzia biashara?

Kwanza kabisa inabidi ufikiri tofauti na wafanyabiashara wengine wanavyofikiri. Jua kwamba uko kwenye hali ya hatari na weka mipango yako vizuri ili usimezwe na hatari hiyo. Simamia vizuri sana biashara yako kuhakikisha unapunguza changamoto zinazoweza kukurudisha nyuma.

Pili, usitumie mtaji wote kwenye biashara hiyo, ingiza kama theluthi mbili na theluthi moja iache pembeni kwa ajili ya kuokoa ikiwa mambo yatakwenda ndivyo sivyo. Hakikisha unakuwa na kiasi hiki cha kukuinua pale utakapoanguka.

Tatu, jifunze zaidi kuhusu biahsara unayotaka kufanya, ijue nje ndani, jua changamoto zote za biashara hiyo na jua sababu za watu wengi kushindwa kwenye biashara hiyo. Pia jifunze na jipangie mbinu za ushindi ma uzifanyie kazi.

Tumia nafasi hiyo uliyoipata kama kitu cha kukusukuma mbele zaidi. Jua mkopo huo ulioupata ni hatari kwako na hivyo fanya biashara yako kwa ufanisi mkubwa ili kuepuka harati inayoweza kukupata.

Lengo langu sio wewe uongope kwa mkopo uliopata, ila uwe chachu kwako kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Unaweza kufikia mafanikio makubwa sana, amua na fanyia kazi maamuzi yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo432