Katika historia ya dunia haijawahi kutokea wakati mzuri wa kuwa mjasiriamali kama ilivyo sasa. Tunaishi kwenye zama ambazo mtu yeyote anaweza kuingia kwenye ujasiriamali na kupata mafanikio makubwa sana. Katika karne ya 19 na karne ya 20, ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali ilibidi mtu awe na uwezo wa kujenga na kumiliki viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali. Au ilibidi mtu awe na umiliki wa sehemu kubwa sana ya ardhi ili kufanya kilimo kikubwa. Lakini katika karne hii ya 21, mambo yamebadilika sana. Unaweza kuingia kwenye ujasiriamali bila ya kumiliki kiwanda au hata hekari moja ya ardhi na ukapata mafanikio makubwa sana. Katika karne hii unaweza kuanza biashara bila ya mtaji mkubwa na baada ya muda ukafikia mafanikio makubwa sana. Huu ni wakati mzuri sana wa kuingia kwenye ujasiriamali na kufikia mafanikio.
Kwa nini wakati huu ni mzuri na bora zaidi.
Zama hizi tunazoishi ni bora na nzuri zaidi kuingia kwneye ujasiriamali kuliko zilizopita. Kuna sababu nyingi zinafanya zama hizi kuwa bora kwa wajasiriamali, baadhi ya sababu hizo ni;
1. Kukua kwa mtandao wa intaneti.
Mtandao wa intaneti umeathiri karibu kila aina ya biashara. Hivi sasa mtu anaweza kuanza na kufanikiwa kupitia ujasiriamali kwa kutumia mtandao wa intaneti. Kwa mfano waanzilishi na wamiliki wa mitandao kama facebook, google na hata jamii forums kwa hapa kwetu Tanzania wameweza kufanikiwa sana kupitia mtandao wa intaneti.
Pia mtandao wa inntanet umefanya upatikanaji wa taarifa kuwa rahisi zaidi kuliko kipindi chochote kile. Sasa hivi kama unataka taarifa yoyote ile inapatikana kwa urahisi sana kwenye mtandao wa intaneti. Unaweza kutumia mitandao ya kijamii kama sehemu yako ya kutangaza bidhaa au huduma zako na ukapata wateja wengi sana.
2. Muingiliano wa jamii na mataifa umeongezeka.
Kitu kingine kinachofanya ujasiriamali kuwa rahisi sana kipindi hiki ni muingiliano mkubwa baina ya jamii na mataifa mbalimbali. Sasa hivi mtu mmoja mwenye biashara yake ndogo anaweza kutafuta masoko hata nje ya nchi bila ya kupitia michakato mingi. Pia soko limekuwa kubwa sana na hivyo mtu yeyote kupata nafasi ya kuweza kufanikiwa kupitia ujasiriamali.
3. Matatizo ya watu yanaongezeka.
Kila siku matatizo ya watu yanaongezeka na kuongezeka kwa matatizo haya kunatengeneza biashara kwa watakaoweza kutatua matatizo hayo. Mahitaji makubwa ya watu kadiri maendeleo yanavyoongezeka yamekuwa nafasi nzuri sana ya kufanikiwa kupitia ujasiriamali. Kwa mfano matatizo ya kiafya yamekuwa mengi sana katika zama hizi hivyo kutoa nafasi kwa wajasiriamali wanaouza bidhaa au huduma za kutibu, kukinga au kuimarisha afya. Pia hitaji la watu kuenda na kazi ya mabadiliko limetengeneza nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye ujasiriamali. Hitaji la watu kuwasiliana kila kona ya dunia limewezesha mitandao ya kijamii kuku asana. Hitaji la watu kupata taarifa kila inapotoke imewezesha tovuti au blogu mbalimbali zinazotoa taarifa kufanikiwa sana.
4. Huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi.
Zamani kidogo ili kupata msaada wa kifedha kwa ajili ya kukuza biashara ilikuwa ni kazi kubwa sana na ilichukua mchakato mrefu mno. Ila zama hizi kuna upatikanaji mkubwa sana wa msaada wa kifedna kwa ajili ya kukuza biashara. Kuna mikopo kutoka benki, taasisi binafsi, vikundi vya kukopa na kuweka akiba na hata mifuko mbalimbali ya fedha. Pia mtu anaweza kuanzisha kampuni na baadae kuifanya ya umma na hivyo kuuza hisa na kuweza kukusanya mtaji mkubwa sana.
Hakujawahi kutokea wakati bora kama huu kuingia kwenye ujasiriamali. Unasubiri nini mpaka sasa? Kama umewahi kufikiria kwamba ujasiriamali ni njia itakayokuwezesha kufikia mafanikio ingia sasa kwenye ujasiriamali. Nakutakia kila la kheri.
TUKO PAMOJA.