Karibu tena msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA kwenye kipengele hiki cha KUJIJENGEA TABIA ZA MAFANIKIO. Kwa miezi mitano iliyopita tumejifunza jinsi ya kujijengea tabia muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Tabia tulizojifunza mpaka sasa ni; tabia ya kujisomea, tabia ya kutumia vizuri muda, tabia ya kutunza na kutumia vizuri fedha na tabia ya kujijengea nidhamu binafsi. Hizi zote ni tabia muhimu sana ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Kama huwezi kutumia muda wako vizuri sahau kuhusu mafanikio, muda ndio fedha mpya. Kama hupendi kujisomea nakujifunza zaidi unaweza tu kusahau kuhusu kufikia mafanikio makubwa.

Kama huna tabia nzuri kwenye kutunza na matumizi mazuri ya fedha zako hujui unakoelekea hasa inapokuja kwenye mafanikio. Na kama huna nidhamu binafsi, tafadhali sana usitafure mafanikio makubwa maana utakuwa hatari kwako mwenyewe na kwa wanaokuzunguka.

Sasa tunaingia kwneye kujifunza tabia nyingine muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Tabia hii ni kujiamini na kujithamini. Hii ni tabia muhimu sana itakayokuwezesha kupata mafanikio makubwa na pia kukuwezesha kudumu kwenye mafanikio hayo. Na ukosefu wa tabia hii ndio unafanya watu wengi wanashindwa kuyafikia mafanikio. Kutokujiamini ndio kunafanya watu wengi wanashindwa kwenye biashara. Kutokujiamini ndio kunafanya watu wengi kushindwa kuondoka kwenye ajira zinazowatesa na kwenda kujiajiri.

Ni kutokujiamini ambako kunafanya mtu ashindwe kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yake ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kutokana na umuhimu wa tabia hii na jinsi ukosefu wake umekuwa na madhara makubwa kwenye maisha ya watu wengi, tutajifunza tabia hii kwa miezi miwili. Hivyo kwa mwezi huu wa kumi na mwezi wa kumi na moja kila siku ya jumanne utapata makala moja ya kujifunza kuhusu tabia hii. Utajifunza umuhimu wa tabia hii, jinsi ya kuitengeneza na jinsi ya kuishi nayo. Na pia tutaona uhusiano kati ya tabia ya kujiamini na mafanikio makubwa.

Nini maana ya KUJIAMINI?

Kujiamini ni pale ambapo mtu anajua ya kwamba anao uwezo wa kufanya jambo au kitu fulani. Kujiamini kunatokana na mtu kujua anao uwezo mkubwa na kujua anaweza kutumia uwezo huo kufanya kile anachotaka kufanya.

Nini maana ya KUJITHAMINI?

Kujithamini haya ni maoni yako juu yako wewe mwenyewe. Hivi ni vile unavyojichukulia wewe kama mtu, kazi unazofanya na hata uhusiano wako na watu wengine. Kujithamini pia kunatokana na vile unavyofikiria watu wengine wanakuchukuliaje.

Ni kipi kinaanza kati ya kujiamini na kufanikiwa?

Watu wenye mafanikio makubwa wanajiamini na kujithamini. Je ni kipi kinaanza kati ya kujiamini na kufanikiwa? Hivi ni vitu viwili ambavyo vinategemeana sana. Ukijiamini utafikia mafanikio makubwa. Na ukiwa na mafanikio makubwa utajiamini.

Ukijiamini utafikia mafanikio makubwa kwa sababu kujiamini kwako kutakuwezesha kufanya mambo ambayo wengine wanaogopa kuyafanya. Kujiamini kwako kutakuwezesha kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako na kutumia mazingira yanayokuzunguka kufikia mafanikio. Kujiamini ndio kutakuwezesha kuwa na uvumilivu na kuvuka nyakati ngumu ili kufikia mafanikio.

Ukifanikiwa utajiaminizaidi kwa sababu utakuwa na uhakika wa kuwa njia fulani uliyowahi kutumia ilileta mafanikio. Jinsi unavyofanikiwa ndivyo unavyoongeza kujiamini na ndio unavyozidi kufanikiwa zaidi. Hii ndio maana wenye mafanikio wanaendelea kufanikiwa na wasiokuwa nayo wanaendelea kuteseka.

Watu wanaokosa kujiamini huwa na woga kwenye kila eneo la maisha yao. Kutokujiamini ni sumu mbaya sana ambayo imekunyima fursa nyingi sana za kufikia mafanikio makubwa.

Twende pamoja katika safari hii ya kujijengea tabia ya kujiamini ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Mwisho wa makala hizi utapatiwa kanuni ya kujiamini ambayo utaprint na kusaini kisha utakuwa unaisema kila siku asubuhi. Hii itakuwezesha kujenga tabia hii zaidi na pia kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.

TUKO PAMOJA.