Mafanikio kwenye ujasiriamali sio bahati bali ni kitu kinachoweza kufanyiwa kazi na kila mjasiriamali. Kila mjasiriamali anaweza kufikia mafanikio makubwa kuliko aliyonayo sasa, kama atakuwa tayari kujifunza zaidi na kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi. Ukichunguza kwa makini wajasiriamali waliofanikiwa utaona ni watu wa kujifunza na wako makini na biashara zao. Pia wanafanya kazi kwa muda mrefu zaidi na wanafanya kwa juhudi na maarifa. Ukichunguza wajasiriamali walioshindwa au wanaosukuma tu siku unakuta ni watu ambao hawajui wanafanya nini kwenye ujasiriamali.

Leo nakushirikisha vitu vitatu muhimu kwa wewe mjasiriamali kujifunza. Kwa kujifunza vitu hivi utaboresha biashara yako na utaweza kufikia mafanikio makubwa sana.

1. Kuuza na kutafuta masoko.

Kama wewe ni mjasiriamali kuna kitu unauza. Unaweza kuwa unauza bidhaa, unauza huduma au hata unauza mawazo. Ili uweze kufanikiwa ni lazima uweze kuuza bidhaa au huduma yako kwa watu sahihi na kwa wingi zaidi. Ni muhimu kujifunza mbinu za kisasa za kuwavutia wateja mpaka waweze kununua bidhaa au huduma yako. Pia ni muhimu sana kujifunza kuhusiana na soko la bidhaa au huduma yako. Jua soko lako ni lipi na unaweza kulifikiaje au kulikuzaje. Pia jua ni soko lipi ambalo sio lako kwa sasa ila unaweza kulifanya kuwa lako kama ukifanya mabadiliko. Kila bidhaa au huduma ina soko lake, lijue vizuri soko ili uweze kulitawala.

2. Kanuni za mawasiliano.

Binadamu ni viumbe ambao tunawasiliana kwa njia mbalimbali. Tunaweza kuwasiliana kwa kuongea, maandishi na hata ishara za mwili. Mawasiliano bora ni nguzo muhimu sana kwako kama mjasiriamali. Utawasiliana na watu wengi sana kwenye biashara yako. Utawasiliana na wateja, utawasiliana na wafanyakazi wako, utawasiliana na wadau mbalimbali na pia utawasiliana na taasisi mbalimbali. Kupitia mawasiliano yako unaweza kuwa na ushawishi utakaokuwezesha kufanikiwa au ukakosa ushawishi na hivyo kukosa fursa nyingi.

Jifunze jinsi ya kufanya mawasiliano mazuri kwa kuongea, kuandika na hata kwa vitendo. Jifunze jinsi kutoa maelezo yako kuhusiana na biashara unayofanya yatakayomwezesha mtu kukuelewa na kutamani kufanya biashara na wewe. Mawasiliano mazuri yatakuwezesha kujenga uhusiano mzuri na wateja na hivyo kuwa na wateja wengi zaidi. Pia yatakuwezesha kupata ushirikiano kutoka kwa wadau na hata taasisi mbalimbali.

3. Kukubaliana.

Katika maisha yako ya kila siku na hata kwenye biashara zako kuna wakati utashindwa kuelewana au utakwaruzana na wadau mbalimbali ambao ni muhimu kwenye biashara yako. Wadau hao wanaweza kuwa wateja, wafanyakazi, washirika, au taasisi zinazohusiana na biashara yako kwa njia moja au nyingine. Katika wakati huu unahitaji kitu kimoja kikubwa sana nacho ni uwezo wa kukubaliana na kuondoa tofauti. Kama utakosa uwezo huu utajikuta unakosa wateja, unavunja uhusiano wa kibiashara na hata kufungiwa biashara yako. Jifunze jinsi ya kuweza kufikia makubaliano pale mnapokuwa mmetofautiana na mtu yeyote hasa kwenye biashara yako. Katika makubaliano wakati mwingine kuna vitu unaweza kupoteza, kuwa tayari kupoteza vitu fulani ili biashara yako ikue zaidi.

Wewe kama mjasiriamali haupo kwenye ulimwengu wako mwenyewe, unazungukwa na wajasiriamali wenzako, wateja na hata wadau wengine ambao ni muhimu kwenye biashara yako. Vitu hivi vitatu muhimu, kuuza na masoko(sales and marketing), kanuni za mawasiliano(communication skills) na kupatana(negotiation) vitakuwezesha kufikia mafanikio makubwa kupitia ujasiriamali.

Unaweza kujifunza vitu hivi kwa kusoma vitabu na kuna vitabu vingi sana vimeandikwa kuhusiana na mambo ya biashara na ujasiriamali. Pia unaweza kujifunza kwa kuendelea kusoma makala hizi za KONA YA MJASIRIAMALI na pia unaweza kuhudhuria semina na mafunzo mbalimbali. Kumbuka kujifunza ni sehemu ya safari yako ya mafanikio kwenye ujasiriamali. Tumia kila nafasi unayopata kujifunza zaidi.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio kwenye ujasiriamali.

TUKO PAMOJA.