Karibu tena msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA katika kipengele hiki cha tabia za mafanikio. Tunaendelea kujifunza tabia ya kujiamini na leo tutajifunza umuhimu au faida ya tabia ya kujiamini. Kujiamini binafsi ni tabia muhimu sana kwenye maisha yako, ni muhimu kuliko unavyofikiri wewe. Tabia hii ya kujiamini ndiyo itakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa katika jambo lolote unalolifanya.

Zifuatazo ni faida au umuhimu wa tabia ya kujiamini binafsi.

1. Kujiamini kutakufanya usikatishwe tamaa.

Kwa kujiamini binafsi itakufanya usikatishwe tamaa hasa pale unapokataliwa au unapokutana na vikwazo. Katika jambo lolote unalofanya unaweza kukutana na vikwazo mbalimbali. Kama hujiamini utaona huu ndio mwisho na huna chochote unachoweza kufanya. Ila kama unajiamini utajua kwamba hiki ni kikwazo ambacho hakina nguvu ya kukuzuia wewe kufikia malengo yako hivyo utaweza kukivuka.

2. Kujiamini kutakufanya uweze kuchukua hali za hatari(ku-take risk).

Katika maisha, kazi na hata biashara kuna wakati inakubidi uchukue maamuzi ambayo yanaweza kuwa hatari kwako(ku-take risk). Na maamuzi ya aina hii ndiyo yanayokuletea mafanikio makubwa kwenye maisha yako kama yakifanikiwa. Kama hujiamini utaogopa kuchukua maamuzi hayo na hivyo kushindwa kupata mafanikio. Kama unajiamini unaweza kuchukua maamuzi hayo kwa sababu unajua uwezo wako ni mkubwa na utapambana mpaka mwisho.

3. Kujiamini kutakufanya usiogope kupingwa.

Katika jambo lolote unalofanya au utakalofanya kuna watu watakupinga. Kuna watu watakuambia haiwezekani au huwezi na wengine watakuambia unapoteza muda wako au hujui ni nini unafanya. Kama hujiamini utaona watu hawa wako sahihi na hivyo kukubaliana na kile wanachosema. Mwishowe wewe ndio unashindwa kufikia mafanikio uliyojipangia. Kama unajiamini utapuuza maneno ya watu hawa kwa sababu unajua wao hawajui ni uwezo gani ambao unao.

4. Kujiamini kutakuondolea hofu.

Mara nyingi hofu unazozipata kwenye maisha yako zinatokana na wewe kuwa na wasiwasi kama kweli unaweza kukabiliana na changamoto uliyokutana nayo au utakayokutana nayo. Kama unajiamini na unajua unaweza kupambana na changamoto yoyote utakayokutana nayo hutaweza kupata hofu.

5. Kujiamini kutakufanya usijione mpweke.

Kama hujiamini na ukawa uko peke yako ni rahisi sana kujisikia upweke na kuona kama umetengwa. Ila kama unajiamini utauona muda ambao uko peke yako kama muda wa kutafakari maisha yako.

6. Kujiamini kutakufanya ujione una thamani.

Kama unajiamini utajiona una thamani bila ya kujali uko katika hali gani. Hata kama huna fedha au mali kwa kujiamini utajua kwamba kwa juhudi zako utaweza kutengeneza fedha na mali za kutosha. Ila kama hujiamini utajiona kama huna thamani hasa pale unapojiona wa chini. Hii itakufanya ujione wewe huna thamani ukijilinganisha na wale unaowaona wana mafanikio.

7. Kujiamini kutafanya watu wakupende.

Watu wanapenda watu ambao wanajiamini, kama utajiamini watu watafurahi kuwa karibu na wewe kwa sababu unawafanya na wao wajiamini. Pia watu wengine wanaweza kukufanya wewe kama shujaa wao kwa kuwa unajiamini. Ila kama hujiamini hata watu watakuwa wanakukimbia kwa sababu utakuwa unawapa na wao woga ambao unao wewe.

8. Kujiamini kutakuondolea msongo wa mawazo na pia kutakufanya usiwe na wivu kwa wale ambao unaona wamefanikiwa kuliko wewe.

Hizo ndio faida za wewe kujiamini. Faida zote hizo zinahusiana moja kwa moja na mafanikio na hivyo hakuna mafanikio kama hakuna kujiamini.

Endelea kujifunza kuhusu tabia hii ya kujiamini na kwenye makala zijazo tutajifunza ni jinsi gani ya kujijengea tabia ya kujiamini.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio.

TUPO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.