Kujiamini ni tabia ambayo kila mtu anaweza kujijengea kama anavyoweza kujijengea tabia nyingine. Katika makala zilizopita tuliona nini maana ya kujiamini na faida za kujiamini. Kwenye makala ya leo tutaangalia jinsi unavyoweza kujijengea tabia ya kujiamini.
Awali ya yote kujijengea kujiamini sio kitu ambacho kitatokea mara moja, bali itakuchukua muda na inahitaji wewe kujitoa. Kama kweli utadhamiria kujijengea tabia ya kujiamini hakuna kitakachoweza kukuzuia kujijengea tabia hiyo.
Zifuatazo ni hatua za kujijengea kujiamini;
1. Gundua vipaji vyako.
Kila mtu ana kipaji chake au ana kitu fulani ambacho anaweza kukifanya vizuri sana. Kwa kuwa na kitu hiki ambacho unaweza kukifanya vizuri sana na unapenda kukifanya kutakupatia kujiamini kwa sababu watu watapenda kazi unayofanya. Kama utajua unachopenda kufanya na kukifanya kwa viwango vya juu sana utapata mafanikio makubwa ambayo yatakuongeze akujiamini.
2. Furahia baadhi ya tabia nzuri ulizonazo.
Ukiacha vipaji, bado kuna tabia fulani ulizonazo ambazo ni nzuri kwako. Zijue tabia hizi na jisifu kwa kuwa nazo, kila mara unapojisikia hufai na kukosa kujiamini kumbuka tabia hizi nzuri ambazo unazo. Tabia hizo inaweza kuwa uwezo mzuri wa kusikiliza, uwezo wa kushawishi, uvumilivu n.k
3. Gundua udhaifu wako.
Sauti iliyopo kichwani mwako inakuambia nini? Ni vitu gani ambavyo unaogopa kufanya? Ni vitu gani unaona aibu kufanya au kuwa navyo? Vijue vitu hivi maana ndivyo vinakujengea kutokujiamini. Kwa kuvijua vitu hivi utajua matatizo ya kutokujiamini yanaanzia wapi na jinsi gani ya kuyaepuka au kuacha kuyapa kipaumbele.
4. Kubali makosa yako na songa mbele.
Hakuna aliye mkamilifu, kila mmoja wetu anakosea. Hata watu ambao wanajiamini sana nao wanakosea ila tofauti yao na wasiojiamini ni kwamba watu wanaojiamini hukubali makosa yao na kusonga mbele. Hawakai kujutia au kufikiria kwa nini makosa hayo yametokea kwao bali hujifunza kwenye makosa yao na kusonga mbele. Yakubali makosa yako, jifunze kupitia makosa hayo na songa mbele. Ukiweza kufanya hivi utajiongezea kujiamini kwa kiasi kikubwa.
5. Jijengee mtizamo chanya.
Kama ukiwa na mtizamo hasi wa kujiona wewe huwezi au hufai moja kwa moja utajiondolea kujiamini. Jijengee mtizamo chanya kwamba unaweza na kwamba wewe ni wa tofauti na wa pekee. Usisikilize maneno ya watu yanayokukatisha tamaa au yanayokuambia huwezi. Mara zote kuwa na mtizamo kwamba unaweza na utajijengea kujiamini.
6. Acha kujilinganisha na wengine.
Kama unataka kujijengea kujiamini acha kujilinganisha na watu wengine, kazana kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Usijilinganishe na rafiki zako, kaka au dada zako au mtu yeyote yule. Kumbuka katika hali yoyote ile kutakuwa na mtu ambaye ni tajiri kuliko wewe, mzuri kuliko wewe na mwenye ujuzi kuliko wewe. Hali kadhalika kuna ambao wamekosa vitu vingi ambavyo unavyo wewe. Kama ukijilinganisha na wale waliofanikiwa kuliko wewe huwezi kujiamini na hii itakupelekea kushindwa.
7. Pokea sifa kwa shukrani.
Utakapoanza kufanya kile unachopenda kufanya kwa ubora wa hali ya juu, kuna watu watakuona na kukusifia kwa kile unachofanya. Pokea sifa zao kwa kusema ASANTE na furahia kitendo hiko. Hii itakuongezea kujiamini na hata kutaka kufanya zaidi ili kutowaangusha wale wanaokuamini. Usipokee sifa kwa kusema ni kitu cha kawaida au sio kitu, chochote kile mtu anachokusifia nacho shukuru na furahi.
8. Igiza.
Kama umejaribu njia zote za kujijengea kujiamini ila bado hujaweza kujiamini igiza kama wewe ni mtu ambaye unajiamini. Kwa kuigiza tabia hii kidogo kidogo utaona unaanza kujiamini. Jifanye kwamba wewe ni mtu unayejiamini, ongea na watu kwa kujiamini na tembea au kaa kwa kujiamini. Kwa matendo haya utaanza kuona watu wakiheshimu na baadae kujijengea kujiamini. Usiwe mtu wa kujiweka nyuma na kuona aibu kusema mawazo yako, jifanye wewe ndio mtu mwenye mawazo bora na toa mawazo yako. Ukifanya hivi mara nyingi utajijengea kujiamini.
9. Wasaidie wengine.
Weka utaratibu wa kujitolea kuwasaidia wengine wanaoweza kuhitaji msaada unaoweza kutoa. Unaweza kuwa msaada wa mawazo, msaada wa muda na hata msaada wa fedha. Unapotoa msaada kwa watu wengine inakuongezea kujiamini na kujiona wewe ni mtu muhimu kwenye jamii yako. Fanya hivi mara kwa mara na utajijengea kujiamini.
10. Simamia misingi yako.
Kila mmoja wetu kwenye maisha ana misingi yake, kuna mambo ambayo utafanya na kuna mambo ambayo hutafanya hata ingekuwaje. Kama huna misingi ya aina hii utajikuta unafanya chochote kinachotokea mbele na hivyo huwezi kujiamini. Jiwekee misingi yako na isimamie na kuifuata katika wakati wowote ule. Inaweza kuwa vigumu lakini ukiweza kufanya hivi utajijengea kujiamini.
Hizo ndio baadhi ya hatua za kujijengea tabia ya kujiamini, zisome na anza kuzitumia kwenye maisha yako na utaona mabadiliko makubwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kuelekea kwenye mafanikio.
TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.
kaka assANTE JAMAN YALE MANENO YA MWSHO YAHUSIO KUJIAMIN TUWEKEE MKUU
LikeLike
Habari Godlove,
Maneno yapi hayo?
LikeLike
AHSANTE MUNGU AKUBARIKI
Mimi mwenyewe nilikuwa sipendi kusifiwa kwasababu naona kwamba nilitakiwa kufanya hivyo hivyo nimegundua kwamba nikishukuru kwa sifa nilizopewa kutanijengea nguvu ya kujiamini zaidi na kufanya vizuri zaidi ili nisiwaangushe walioona nafanya vizuri
LikeLike
Habari Daniel,
Anza sasa kuwashukuru na kupokea sifa unazopewa ili zikuwezeshe kufanya zaidi
LikeLike