TIBA YA KWANZA; Anza kunenepesha mfuko wako.

Arkad alianza mafunzo yake kwa kuwauliza wanafunzi wake maswali. Alimuuliza mmoja unafanya kazi gani? Akamjibu ni mwandishi na anawaandikia watu. Arkad alimjibu hata yeye alikuwa anafanya kazi hiyo na ndio ilimpatia fedha yake ya kwanza aliyowekeza. Alimwambia hata yeye anaweza kufanikiwa sana kwa kuanza na kazi hiyo.

Alimuuliza mwingine anafanya kazi gani akamjibu ni muuza busha, ananunua wanyama kwa watu na kuwachinja kisha kuuza nyama. Arkad alimwambia kwa kuwa anafanya kazi na anapata kipato basi anayo nafasi kubwa ya kufanikiwa. Arkad aliendelea kumuuliza kila mtu aliyekuwepo kwenye ukumbi ule kuhusu kazi anayofanya.

Baada ya zoezi hilo Arkad aliwaambia wote kwamba kila mtu kwenye ukumbi ule alikuwa na kazi anayofanya ambayo inamuingizia kipato. Na aliwaambia kuna njia nyingi sana za kutengeneza kipato. Na pia aliwauliza vipato hivi si vinaingia kwenye mifuko yao? Wote walikubali. Akawauliza tena je hawaoni ni sahihi kutumia vyanzo vyao vya mapato walivyonavyo kufikia utajiri? Wote walikubali kuwa ni sahihi kufanya hivyo.

Arkad aimgeukia mtu mmoja aliyesema anauza mayai akamuuliza, kama utachukua kikapo na kuweka mayai kumi kila siku asubuhi na jioni ukaondoa mayai tisa kutoka kwenye kikapu hiko ni nini kinatokea? Yule muuza mayai alimjibu kikapu kitajaa mayai kwa sababu unatoa mayai machache zaidi ya uliyoweka. Arkad aliwageukia wengine na kuwauliza kuna mtu ambaye mfuko wake umesinyaa? Wote wakajibu ndio. Arkad aliwaambia leo nawapa siri ya kwanza ya kunenepesha mifuko iliyosinyaa, kwa kila fedha kumi unazopata tumia tisa na moja weka kwenye mfuko wako. Baada ya muda mfuko wako utatuna na kukua zaidi. Aliwaambia hiyo ndio njia iliyompatia utajiri mkubwa yeye, aliwaambia sio kazi rahisi ila inawezekana.

Arkad aliwaambia wanafunzi wangu hiyo ndio tiba ya kwanza ya mifuko iliyosinyaa; kwa kila fedha kumi natumia tisa na kuhifadhi moja. Aliwaambia wajadiliane na kesho yake wangeendelea na tiba ya pili.

TIBA YA PILI; Dhibiti matumizi yako.

Arkad alianza siku ya pili kwa kuwaambia baadhi ya wanafunzi wamekuwa wanamuuliza unawezaje kuweka sehemu ya kumi ya kipato chako ikiwa kipato hicho hakitoshi hata kwa matumizi yake ya kawaida. Arkad aliwauliza tena, ni wangapi kati yenu jana walikuwa na mifuko iliyosinyaa? Wote walinyoosha mikono. Akawauliza inawezekanaje wote kuwa na kifuko iliyosinyaa ili hali kila mtu anafanya kazi tofauti na ana kipato tofauti?

Arkad aliwaambia kwamba atawapa siri kubwa sana kuhusu mapato na matumizi ya binadamu; Aliwaambia kile ambacho watu wanasema ni matumizi ya muhimu huwa yanakua jinsi kipato kinavyokua. Aliwaambia wasichanganye matumizi muhimu na tamaa, aliwaambia kila mtu ana tamaa ambazo hawezi kuziridhisha. Aliwaambia kama wanafikiri wakiwa na utajiri ndio wataridhisha furaha zao wanajidanganya. Kuna ukomo wa muda wako, kuna ukomo wa nguvu zako, kuna ukomo wa kiasi cha chakula unachoweza kula na hivyo pia kuna ukomo wa starehe unayoweza kupata, Arkad alisema. Aliwaambia kama magugu yaotavyo shambani ikiwa hakujapandwa, ndivyo tamaa zinavyokua kama zisipodhibitiwa.

Arkad aliwaambia wayajue matumizi yao vizuri kisha wajue ni yapi ya muhimu na yapi sio ya muhimu. Kisha yale ambayo sio ya muhimu waachane nayo. Aliwaambia waweke bajeti ambayo itawawezesha kuishi kwa sehemu ya tisa ya kipato chao. Waendelee kutumia bajeti hiyo na kuifanyia marekebisho kila inapobidi lakini isizidi sehemu ya tisa ya kipato chao.

Arkad aliwaambia hii ni tiba ya pili ya mifuko iliyosinyaa; weka bajeti ya matumizi yako, jua ni kiasi gani utatumia kwa chakula na kiasi gani kwa starehe, lakini bajeti hiyo isizidi sehemu ya tisa ya kipato chako.

TIBA YA TATU; Ifanye Akiba yako izae zaidi.

Arkad alianza siku ya tatu kwa kuwaambia kuwa baada ya kujijengea nidhamu ya kuweka sehemu ya kumi na pia kudhibiti matumizi, baada ya muda mifuko itaanza kutuna. Aliwaambia siku hiyo angewafundisha jinsi ya kufanya akiba yao kuzaa zaidi, maana kuweka tu akiba ni mwanzo, ili kufikia mafanikio ni lazima ikuzalie. Arkad aliendelea kuwaambia unawezaje kuifanya fedha yako ikufanyie kazi? Aliwaambia uwekezaji wake wa kwanza haukuwa wa bahati kwa sababu hakuwa amejifunza. Uwekezaji wa pili ulikuwa kumpa mtu anayekopesha fedha na kisha kumpatia riba na hivyo uwekezaji wake kukua zaidi.

Aliwaambia utajiri wa mtu haupo kwenye fedha anazobeba kwenye mfuko wake au akiba yake bali kwenye uzalishaji unaofanyika na fedha zake. Kwa njia hii kipato kinakuwa kikubwa hata kama mtu ataacha kufanya kazi. Aliwaambia kipato chake kimekuwa watumwa wake kwa sababu kinaendelea kumzalishia zaidi.

Aliwaambia fedha inaongezeka sana kama ikipewa muda. Aliwapa mfano wa mkulima mmoja alipata mtoto na akaamua kuwekeza kwa ajili ya mtoto wake huyo. Alichukua vipande kumi vya fedha na kumpatia mmkopesha fedha na kumwambia aviweke mpaka mwanae atakapokua. Walikubaliana kwamba riba itakuwa robo ya kiwango kilichopo kila baada ya miaka minne. Baada ya miaka 25 mkulima yule alienda kwa aliyempa fedha zile na kukuta zimekua na kufikia vipande thelathini na moja na nusu. Kwa kuwa mwanae hakuhitaji fedha hizo kwa kipindi hiko aliziacha ziendelee kukua zaidi. Alipofikisha miaka hamsini, mtoto yule alienda kwa mtu yule aliyepewa fedha na kukuta zimefika vipande 167. Kumbuka baba yake aliweka vipande kumi tu. Hii ndio nguvu ya riba inayokusanywa kwa muda. Kwa miaka hamsini uwekezaji umekua mara 17.

Arkad aliwaambia hii ndio tiba ya tatu; ifanye kila fedha yako ikufanyie kazi ili uweze kuzalisha utajiri zaidi na hivyo utatengeneza mfereji wa utajiri utakaoendelea kutiririsha utajiri hata kama hufanyi kazi.

Tutaendelea na tiba nyingine zilizobaki kwenye uchambuzi ujao. Tafadhali tushirikishe mambo matano uliyojifunza hapa kwenye uchambuzi huu.

Nakutakia kila la kheri kwenye kufikia uhuru wa kifedha,

TUPO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.

P.S Usisahau kutushirikisha mambo kumi uliyojifunza.