Tamaa ya bahati ni kitu kinachotokea kwa kila mtu. Hata watu wa babeli walitamani sana bahati. Kila mtu anapenda kukutana na bahati ambapo kwa juhudi kidogo aweze kufikia mafanikio makubwa. Je kuna njia yoyote ya kukutana na miungu inayotoa bahati ili ikupatie bahati? Je kuna njia yoyote ya kukaribisha bahati? Haya ni baadhi ya maswali ambayo watu wa babeli walikuwa wakijiuliza na kuyatafutia majibu.
Watu wa babeli walikuwa watu wa kuchunguza na kufikiri. Ni katika kufikiri huku walipata majibu mengi yaliyowafanya kuwa watu matajiri sana. Japokuwa wakati huo hawakuwa na shule au vyuo, walikuwa na kumbi mbalimbali ambapo walikutana na kujadiliana. Katika kumbi hizi za majadiliano kila mtu alikuwa sawa kwenye kutoa maoni yake. Mtumwa aliweza kupinga hoja za mwana mfalme bila ya kuogopa bali kutumia hoja.
Katika kumbi hizi za majadiliano za babeli kulikuwa na ukumbi mmoja maalumu ambao Arkad aliutumia kuendesha majadiliano mbalimbali. Kila siku jioni watu walikutana kwenye ukumbi huo na Arkad aliendesha mijadala mbalimbali ihusuyo fedha, utajiri na mafanikio.
Siku moja jioni wakati jua linazama ukumbi ulikuwa tayari umejaa watu waliohudhuria mjadala. Arkad aliwauliza, je tujadili nini jioni ya leo? Mtu mmoja alisimama na kusema kuna somo moja ambalo halijawahi kujadiliwa na angependa sana kusikia linajadiliwa. Aliendelea kusema kwamba siku hiyo alipata bahati ya kuokota mfuko uliokuwa na fedha ndani yake. Aliwaambia angependa kuwa na bahati zaidi ili aweze kupata fedha zaidi, hivyo aliomba mjadala uwe ni jinsi gani ya kuvuta bahati nzuri.
Arkad akasema, somo zuri sana limetolewa kwa ajili ya kujadili. Aliendelea kusema kwa baadhi ya watu bahati ni kitu kinachotokea tu kama ajali wakati kwa watu wengine wanaamini kuna muungu unaotoa bahati unaoitwa Ashtar. Aliwauliza wote je wako tayari kujadili kuhusu bahati? Wote aliitika ndio wapo tayari.
Arkad alisema kwa kuanza mjadala wetu tunaomba kusikia kwa wale ambao wamewahi kukutana na bahati, yaani bila ya juhudi zozote wakakutana na fedha ambazo zimewapa mafanikio. Kulikuwa na utulivu ambapo kila mmoja alimwangalia mwenzake lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza. Arkad aliwaambia hakuna hata mmoja? Basi bahati itakuwa ni kitu ambacho ni cha nadra sana. Aliwauliza kwa kuwa mle ndani hakuna mtu mwenye uzoefu wa bahati, ni wapi wanaweza kupata mtu mwenye uzoefu wa bahati.
Mtu mmoja alisimama na kusema sehemu nzuri ya kuzungumzia bahati ni kwenye michezo ya kubahatisha. Alisema ni katika michezo hii ambapo utakuta watu wanaomba miungu iwape bahati waweze kushinda. Arkad alimuuliza je wewe umewahi kubahatika kwenye michezo hiyo, je miungu uliyoiomba ilibadili mchezo na hatimaye wewe kushinda? Kijana mmoja aliingia kwenye majadiliano na kusema kwamba anafikiri hata hiyo miungu huwa haijui kama anacheza mchezo maana haijawahi kumsaidia.
Mtu mwingine aliendelea kusema kuhusu kuchez akama ri kwenye mashindano mbalimbali, je kuna watu wenye bahati ya kubashiri vizuri? Alisema kwamba inajulikana kabisa kwamba timu fulani ni bora, je kuiwekea kamari kunakufanya wewe uwe na bahati?
Arkad alisema miungu haipo kwa ajili ya kusaidia watu kushinda bahati na sibu au kushinda kamari bali ipo kwa ajili ya upendo na utu. Aliwaambia ipo kwa ajili ya kuwasiaida wale wenye mahitaji na kuwapa wale wanaostahili kulingana na juhudi zao.
Arkad aliendelea kuwaambia, kwenye kulima, kufanya biashara kwa uaminifu, na kwenye kila kazi ya mtu, kuna kila fursa ya kupata bahati kupitia juhudi na maarifa. Aliendelea kusema wakati mwingine mtu anaweza asipate faida kutokana na maamuzi mabovu aliyofanya, kubadilika kwa msimu au sababu zozote zilizo nje ya uwezo wake lakini kama mtu atakuwa mvumilivu ni lazima atapata faida baadae. Hii ni kwa sababu nafasi ya kupata faida ipo kwenye upande wake.
Arkad aliendelea kusema mtu anapocheza mchezo wa kubahatisha au kamari hali inabadilika. Faida haiwi upande wake bali upande wa mchezeshaji wa mchezo huo. Hivyo mtu anayecheza mchezo wa bahati ana nafasi tano za kupoteza na nafasi nne za kupata. Kwa vyovyote vile fedha anazoshinda mtu kwenye michezo hii ni ndogo ukilinganisha na anazopoteza. Na mtu pekee mwenye uhakika wa kufaidika na mchezo huu ni yule anayechezesha.
Mtu mmoja aliuliza lakini kuna watu ambao wanapata fedha nyingi sana kwenye michezo hii. Arkad alijibu ndio, lakini wanazifanyia nini fedha hizo? Alisema katika watu wengi anaowajua waliofanikiwa hakuna hata mmoja ambaye alianza kwa kupata fedha za bahati au kamari.
Tutaendelea na sehemu ya pili ya uchambuzi huu kwenye makala ijayo…
Nakutakia kila la kheri kwenye kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.