Ukiangalia katika jamii nyingi watu waliosoma sana wanaishia kuwa na maisha ya kawaida huku wakikosa na uhuru wa kifedha. Na katika jamii nyingi watu wengi ambao wana uhuru wa kifedha hawana elimu kubwa. Ni kitu ambacho kimekuwepo kwa muda mrefu na kinatokea dunia nzima. Je unajua nini kinasababisha hali hii? Leo tutajadili hapa ili uweze kuchukua hatua kama upo kwenye moja ya makundi haya mawili.

Kwanza kabisa tunaposema uhuru wa kifedha tunamaanisha hata mtu asipofanya kazi moja kwa moja bado ana kipato kinachomtosheleza kuendelea na maisha yake ya kila siku bila kuathiri kitu chochote.

Ukiangalia wasomi wengi wanaweza kuonekana wana fedha za kuwatosha, ila wanapoacha kazi au kustaafu ndio unaona wazi wazi kwamba hawakuwa na uhuru wa kifedha kwani maisha yanabadilika sana.

wahitimu

Sababu zinazowafanya wasomi kushindwa kufikia uhuru wa kifedha zipo wazi ila sio wengi ambao wanazijua na jinsi ya kuziepuka.

1. Wasomi wanatumia muda mwingi kwenye elimu.

Ukilinganisha wasomi na wale ambao sio wasomi sana, wasomi wanatumia muda mwingi sana kwenye elimu. Tuchukue mfano wa vijana wawili ambao wamemaliza kidato cha nne mwaka mmoja, mmoja akaingia kwenye ulimwengu wa kazi au biashara na mwingine akaendelea na elimu. Aliyeendelea na elimu ana miaka 2 ya sekondari, miaka 3 ya shahada ya kwanza, miaka 2 ya shahada ya udhamili n.k. Kwa vyovyote vile huyu msomi atakua nyuma kiuzalishaji zaidi ya miaka 5 ukilinganisha na yule ambaye hakuendelea na shule.

2. Wasomi wanakosa elimu muhimu ya fedha.

Mfumo mzima wa elimu hakuna sehemu ambapo kunafundisha kitu chochote kinachohusiana na fedha binafsi. Kutokana na ukosefu wa alimu hii wasomi wanajikuta wana usimamizi mbovu wa fedha zao.

3. Wasomi wanatumia muda mwingi kwenye kazi zao.

Baadhi ya kazi za wasomi zinawahitaji kutumia muda mwingi sana na hivyo kukosa muda wa kufuatilia mambo yao ya fedha na hata uwekezaji. Kwa mfano daktari anajikuta ana kazi nyingi sana za kuokoa maisha ya watu na hivyo kusahau upande wake wa maisha ya kifedha. Injinia anaweza kuwa anasafiri sana kusimamia miradi mbalimbali na hivyo kushindwa kutuliza akili yake na kufanya uwekezaji mzuri.

4. Wasomi wana matumizi makubwa sana.

Pamoja na kwamba baadhi ya wasomi wanapata mishahara mikubwa na bado wana marupu rupu, matumizi yao ni makubwa sana. Hii inatokana na wao kutaka kuishi maisha ambayo jamii imeyajenga kwa wasomi. Kwa matumizi haya makubwa hata kama angekuwa na uwekezaji mdogo hauwezi kuhimili matumizi yake pale ambapo atakuwa hafanyi kazi.

5. Wasomi wanajiona wanajua kila kitu.

Wasomi wengi hata ambao ni maprofesa wana uelewa mdogo sana kuhusu mambo ya fedha na uwekezaji, lakini hutawaona wakijifunza kuhusu mambo hayo. Wakiona kuna semina zinaendesha kuhusiana na mambo hayo wanajisemea kwamba wanajua yote hayo, ukiwaambia wasome kitabu au kujifunza kwa njia nyingine watakuambia vitu hivyo wanavijua au hawana muda huo. Wanaweza kufikiria wanajua vitu hivyo ila ukwelini kwamba hawana uelewa mzuri kuhusu mambo ya fedha na uwekezaji.

Ufanye nini wewe msomi ili kuondoka kwenye mtego huo?

Kwanza kabisa kama utaendelea kukaa kwenye huo mtego, kazi ikiisha leo muda wa maisha yako unaweza ukahesabika. kuna sababu kubwa sana kwa nini wastaafu wengi huwa wanakufa ndani miaka mitano baada ya kustaafu(Soma; Hivi ndivyo unavyokufa na miaka 35 na kuzikwa na miaka 65)

Ili kuepuka hali hiyo unaweza kuanzia hapa;

1. Amua kwaba unakwenda kufikia uhuru wa kifedha na weka malengo na mipango ya kufikia hatua hiyo.

2. Anza kubadili tabia ambazo zinakuzuia kufikia uhuru wa kifedha, anza na kupunguza matumizi yasiyo ya msingi.

3. Tenga saa moja kila siku kwa ajili ya kufuatilia maisha yako ya kifedha na uwekezaji pia. Hata kama upo bize kiasi gani usipuuze eneo hili la maisha yako. Unaweza kupata saa moja kwa kuamka mapema zaidi ya unavyoamka kila siku.

4. Kubali kwamba huna uelewa mkubwa kuhusu mambo ya fedha na uwekezaji na kubali kujifunza kupitia njiambalimbali.

5. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kupitia KISIMA utajifunza mambo mengi sana kuhusu maendeleo na mafanikio. Kupata maelezo zaidi ya JINSI YA KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA bonyeza maandishi hayo. Jiunge leo na baadae utaishukuru nafsi yako kwa maamuzi sahihi uliyofanya.

Kila mmoja wetu anao uwezo wa kufikia uhuru wa kifedha kama atajifunza jinsi ya kufanya hivyo.Jifunze sasa na yafanyie kazi yale unayojifunza na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia uhuru wa kifedha.

TUPO PAMOJA.

kitabu-kava-tangazo432