Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON. Na hii ni sehemu ya pili ya uchambuzi wa sheria tano za fedha. Katika sehemu ya kwanza tuliona Arkad akimpatia mwanae fedha na busara ya sheria tano za fedha.
Baada ya kuwaambia watu wale sheria tano alizopewa na baba yake Nomasir aliendelea kumwambia baba yake kwamba amemwambia matatizo yote yaliyomkuta. Akasema hakuna matatizo yasiyokuwa na mwisho na matatizo yake yalifikia mwisho pale alipoweza kupata ajira ya kusimamia watumwa waliokuwa wakifanya kazi ya kujenga ukuta wa mji.
Alisema kwa kufaidika na sheria ya kwanza ya fedha, aliweka akiba sehemu ndogo ya kila fedha aliyopata mpaka akaanza kuona anakuwa na kiasi kikubwa cha fedha. Alisema ni kazi inayokwenda taratibu na inahitaji uvumilivu na ilimhitaji kuwa na matumizi madogo sana. Siku moja mmoja wa wamiliki wa watumwa alimfuata na kumwambia wewe ni kijana ambaye umekuwa na matumizi madogo sana kulingana na kipato chako. Je umeweka fedha zako sehemu ambayo zinazalisha?
Nomasir alimjibu kwamba anafanya hivyo ili kukusanya fedha na kumthibitishia baba yake kwamba anao uwezo wa kudhibiti fedha. Kuhusu kuwekeza fedha zake sehemu inayozalisha alimwambia hajafanya hivyo kwa sababu anakumbuka jinsi alivyotapeliwa mara nyingi. Bwana yule alimwambia kama ataweza kumwamini atamuonesha njia nzuri za kuwekeza fedha zake na zimzalishie fedha zaidi.
Yule bwana alimwambia baada ya mwaka mmoja kazi ya kujenga ukuta ule unaozunguka mji itakuwa imeisha na watahitajika kujenga mageti ya chuma ya kulinda mji ule. Ili kujenga mageti hayo, chuma nyingi zitahitajika, ila mpaka sasa mfalme hajafikiria kuhusu kupatikana kwa chuma hizo. Hivyo alimwambia mpango ni kwamba wao wakusanyane watumie fedha zao kutuma wafanyabiashara wawanunulie chuma kutoka miji ya mbali na wazihifandhi. Wakati ukuta unakamilika na mfalme atakaposema watafute chuma za kujenga mageti watatoa chuma hizo na kuziuza kwa bei kubwa.
Nomasir anasema aliona fursa ile kama nafasi ya kutumia sheria ya tatu ya fedha. Na alikubaliwa kuingia kwenye kundi lile na wakafanya kama walivyopanga. Anasema lilikuwa kundi la watu wenye busara na walikuwa na mipango mizuri ya fedha ambayo ilipitiwa vizuri kabla ya kutumia fedha kwenye mipango hiyo. Aliendelea kusema kwa kushirikiana na watu wale aliendelea kupata busara zaidi kuhusu uwekezaji mzuri na fedha zake ziliongezeka mwaka baada ya mwaka na aliweza kupata fedha nyingi sana kushinda zile alizopoteza.
Alimwambia baba yake kwamba kupitia sheria zile tano za fedha amepata busara kubwa sana iliyomwezesha kutoka kwenye umasikini na ujinga wa fedha mpaka kwenye utajiri na busara kubwa ya fedha. Aliacha kuongea na kuwaita watumwa wake waliokuwa nyuma. Walikuja na mifuko mikubwa mitatu na mifuko yote ilikuwa imejaa fedha. Alimwambia baba yake kwamba haya ndio mavuno ya busara zako ulizonipatia kwenye sheria tano za fedha. Alisema bila ya busara fedha hupotea haraka sana. Baba yake aliweka mikono kwenye kichwa chake na kumwambia mwanangu umejifunza somo zuri na sasa najisikia fahari kuwa na mtoto kama wewe.
Kalabab aliishia hapo katika kuelezea hadithi hiyo. Aliwauliza watu wale waliokuwa wanamsikiliza ni nani kati yenu ambaye anaweza kwenda kwa baba yake na kumwambia ampe fedha na kisha atazifanyia kazi na ziongezeke zaidi? Alisema watu wengi wanakuwa na visingizio kwamba wamesafiri nchi za mbali na kufanya kazi nyingi lakini bado wameshindwa kupata fedha nyingi. Aliwaambia watu wanaweza kuwa na fedha nyingi sana kama watazijua sheria tano za fedha na kuishi nazo kila siku kwa kuzifanyia kazi.
Tujikumbushe tena sheria tano za fedha ambazo kila mmoja wetu inabidi aanze kuziishi sasa;
Sheria tano za fedha.
1. Fedha huja na kuongezeka kwa mtu ambaye anaweka pembeni sio chini ya sehemu ya kumi ya kipato chake kama akiba.
2. Fedha hufanya kazi kwa bidii kwa mtu mwenye akili anayeweza kuiwekeza sehemu inayozalisha.
3. Fedha huendelea kubaki kwa mtu anayeilinda na kuiwekeza kwa kufuata ushauri wa watu wenye busara.
4. Fedha hukimbia kwa mtu ambaye anaiwekeza kwenye eneo ambalo halijui au hafuati ushauri wa watu wenye busara.
5. Fedha hukimbia kwa mtu ambaye anailazimisha izalishe sehemu ambayo haiwezi kuzalisha au anayefuata ushauri wa watu matapeli.
Tutumie sheria hizi tano ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia uhuru wa kifedha.
TUPO PAMOJA.
Ahsante ubarikiwe
LikeLike
Asante na wewe pia.
Karibu sana, TUPO PAMOJA.
LikeLike
kiongoz mungu na azid kukupa maono zaid na zaid mkuu.
LikeLike
Asante na karibu sana,
TUPO PAMOJA.
LikeLike