Kuwa kwenye ujasiriamali au biashara ni jambo moja, kupata mafanikio kupitia ujasiriamali ni jambo jingine ambalo ni muhimu sana kwa kila mjasiriamali. Sio kazi ngumu sana kuanza biashara hasa pale unapokuwa huna kingine cha kutegemea isipokuwa kuingia kwenye biashara. Ila ni kazi ngumu kidogo kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara yako. Unaweza kudhibitisha hili kwa kuangalia biashara nyingi ambazo kila mwaka ziko vile vile hazikui wala kuzalisha biashara nyingine.

Kuna mambo mengi sana ambayo unaweza kufanya ili kuikuza biashara yako na hatimaye kupata mafanikio makubwa. Mambo mengine yanategemea vitu ambavyo huwezi kuvidhibiti kama hali ya uchumi au mfumuko wa bei. Leo tutajadili mambo matatu ambao yako chini ya uwezo wako na ambayo ukiyafanya utakuwa na uhakika wa kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara unayofanya au unayotaka kufanya kama bado hujaingia kwenye biashara.

1. Kuwa na uthubutu.

Hatua ya kwanza kabisa kwenye kuweza kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara na ujasiriamali ni kuwa na uthubutu. Ni muhimu sana uwe na ujasiri wa kujaribu mambo mapya ambayo yanaweza kuwa hayaoneshi uhakika wa mafanikio ila yanaweza kuleta mafanikio makubwa. Kwenye ujasiriamali kuna baadhi ya maamuzi unahitaji kuyafanya ila yanaonekana kuwa hatari sana. Na kama ukifanya maamuzi hayo unaweza kufanikiwa sana au pia unaweza kupoteza kiasi kikubwa sana. Kwa kuogopa kufanya maamuzi ya aina hii inawafanya wajasiriamali wengi kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Wachache ambao wana uthubutu na wenye ujasiri wananufaika sana na maamuzi ya aina hii.

2. Kuwa wa kwanza.

Kuna usemi mmoja unatumika kwenye biashara na unasema kwamba; ‘kama biashara unayofanya huwezi kuwa wa kwanza au wa pili unapoteza muda wako’. Ukweli ni kwamba ushindani ni mkubwa sana kwenye biashara na unapokuwa haupo kwenye ubora wa hali ya juu biashara yako itapata shida kubwa sana. Ni lazima uwe bora kuliko wengine wote wanaofanya kile unachofanya, ni lazima biashara yako iweze kutoa bidhaa au huduma ambazo mteja hawezi kuzipata sehemu nyingine, hapo ndipo utaweza kufikia mafanikio makubwa.

Hata kama unafanya biashara ya uchuuzi ambapo unauza bidhaa zile zile ambazo kila mtu anauza, ziuze kwa njia ya tofauti sana ambayo itaongeza ubora kwenye biashara yako. Unapokuwa bora na unapokuwa namba moja unaondokana na ushindani usio na maana na hivyo kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kama haufanyi kwa ubora maana yake ni kwamba unafanya kama kila mfanyabiashara mwingine anavyofanya na hivyo mtaanza kugombania wateja kwa njia ambazo zitawaumiza wote kwa mfano kupunguza bei.

3. Kuwa tofauti.

Kama huwezi kuwa tofauti usijisumbue kuingia au kuendelea na biashara yako. Hii ni kwa sababu kila siku utakuwa na msongo wa mawazo kutokana na mambo kuwa magumu. Katika biashara yoyote unayofanya au unayotaka kufanya angalia ni jinsi gani unaweza kujitofautisha na mtu mwingine anayefanya biashara kama hiyo. Hata kama mko eneo moja na wote mnauza bidhaa zinazofanana angalia vitu vitakavyokutofautisha wewe na wafanyabiashara wengine. Na vitu hivi view ni vile ambavyo vinawavutia wateja kuja kwenye biashara yako kuliko kwenda kwenye biashara ya watu wengine. Na utakapojitofautisha ndio utaweza kuwa wa kwanza katika biashara unayofanya.

Kuna njia nyingi sana za kujitofautisha, fikiria kwa biashara unayofanya na kwa wateja ulioko nao ni kitu gani ukifanya kitawaleta wateja wengi zaidi. Kitu hiko kiwe hakijafanyika na wengine au kama wanakifanya basi wewe unaweza kukiboresha zaidi. Ukifikiria kwa makini ni lazima utapata baadhi ya vitu ambavyo vitakutofautisha na wafanyabiashara wengine na hivyo kukuweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia mafanikio makubwa.

Fanya mambo hayo matatu kuboresha biashara yako ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Usifanye tena biashara kwa kuangalia wengine wanafanya nini kisha ukaiga. Hii itakuwa njia rahisi sana ya wewe kushindwa.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.