Karibu tena msomaji kwneye kipengele cha jinsi ya kujijengea tabia za mafanikio. Mwezi wa kumi na mwezi wa kumi na moja tulikuwa tunajadili jinsi ya kujijengea tabia ya kujiamini.
Katika makala zilizopita tumeona mambo mengi muhimu ya kuzingatia ili kuweza kujijengea tabia hii ya kujiamini. Pia tuliona umuhimu wa tabia ya kujiamini na uhusiano wake na kufikia mafanikio makubwa.
Leo nitakushirikisha kanuni ya kujijengea tabia ya kujiamini. Mwanzo kabisa wa makala hizi za kujiamini niliahidi kukutumia maneno ambayo unaweza kuwa unayasema kila siku na hii ikakuongezea kujiamini kwako. Maneno haya yanatoka kwenye kitabu Laws of Success kilichoandikwa na Napoleon Hill. Maneno haya utayachapa mahali na uwe unayasema kila siku mara mbili, asubuhi wakati unaamka na usiku kabla ya kulala. Kwa kufanya hivi utajijengea kujiamini kwa kiwango kikubwa sana.
Kanuni ya kujijengea kujiamini.
1. Najua kwamba ninao uwezo wa kufikia malengo yangu niliyojiwekea hivyo nahitaji kuwa mvumilivu nakuendelea kutekeleza mipango yangu kila siku.
2.Naelewa kwamba mawazo ninayokuwa nayo kwenye kichwa changu yanajionesha kwenye tabia ya nje ya mwili na yanaweza kubadilika na kuwa matendo ya kweli. Hivyo kila siku nitaifanya akili yangu iwe na mawazo yanayoendana na malengo na mipango yangu, kwa kutengeneza picha za akili na kuzibadili picha hizo kwenda kwenye uhalisia kwa kuifikiria kila siku. Nitatenga dakika 30 kila siku kwa ajili ya zoezi hili.
3. Najua kwamba kupitia kujijengea mawazo, mahitaji ambayo ninayataka kweli na ninayoyawaza kila mara yatajitokeza kwenye ulimwengu wa kawaida. Hivyo nitatenga dakika kumi kila siku kupitia na kujijengea mawazo yatakayoniwezesha kufikia mahitaji yangu.
4. Nimeandika kwa umakini kabisa maelezo ya malengo na mipango yangu kwa miaka mitano ijayo. Nimeweka gharama ya huduma zangu kwa kila mwaka kwa miaka hiyo mitano, gharama ninayotegemea kupokea na gharama hii itatokana na huduma nzuri nitakayoitoa.
5.Naelewa kwamba hakuna utajiri au nafasi inayoweza kudumu kama haikujengwa kwenye misingi ua ukweli na haki, hivyo sitajihusisha kwenye kazi au biashara ambayo haitawasaidia watu wengine. Nitafanikiwa kwa kuzivuta kwangu nguvu ninazotaka kutumia na kushirikiana na watu. Nitawashawishi wengine kunisaidia mimi kwa sababu nitawasaidia kwanza. Nitaacha kabisa chuki, husda, wivu, ubinafsi na mtizamo hasi kwa kutengeneza upendo kwa binadamu wote kwa sababu najua kwamba mtizamo hasi kwa watu wengine hauwezi kuniletea mimi mafanikio. Nitawashawishi wengine kuniamini na mimi nitawaamini pia.
Hivyo ndio vipengele vitano muhimu vya kanuni ya kujijengea kujiamini. Maelezo hayo yameandikwa kwa nafsi ya kwanza, yaani utayasoma kama vile unajiambia wewe mwenyewe. Yachape maandishi hayo kwenye karatasi na isome karatasi hiyo kila siku mara mbili, asubuhi kabisa unapoamka na usiku kabla ya kulala. Kwa kufanya hivyo utaijengea akili yako mtazamo mpya ambao utakuwezesha kuchukua hatua na kufikia mafanikio makubwa sana.
Naamini kwamba unaweza kufikia mafanikio makubwa sana kwa sababu uwezo unao na nia tayari tumejadili hapa. Imebaki wewe tu kuchukua hatua.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.