Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ni matumaini yangu unaendelea vizuri katika harakati zako za kutafuta mafanikio na uhuru wako wa kifedha. Katika kona yetu ya Ujasiriamali na biashara, tutajifunza Mbinu ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia, ili kujenga mafanikio katika biashara. Mbinu hizi ni baadhi katika mbinu nyingi za kijasiriamali ili kujenga mafanikio.

1. Fanya biashara uipendayo

Kama wewe ni mjasiriamali mpya ni muhimu kufanya biashara ya kile kitu unachokipenda. Usiingie kwenye biashara kwa kufanya kile ambacho umeona tu wengine wanafanya, usifuate mkumbo! Kama wewe umefanya kazi kwa muda mrefu katika mambo ya ufundi na una kiu kubwa ya kuwa mjasiriamali, ni vema ukafikiria ni kitu gani katika tasnia hiyo ya ufundi, unaweza ukaifanya wewe mwenyewe binafsi vizuri zaidi. Kwanini usifikirie kuanzisha kitu chako ambacho una uzoefu nacho mzuri zaidi na kuona kwa namna gani siku za baadaye utaweza kujitegemea? Ikiwa wewe ni mjasiriamali wa muda mrefu, basi inakupasa kujenga ari ya kupenda hicho ambacho unakifanya. Baadhi ya wajasiriamali wamevunjika moyo kwa kuona hawapati matokeo mazuri kwa yale wanayofanya. Tambua kuwa mafanikio katika biashara si swala la kulala na kuamka, bali ni kitu ambacho kinachoweza kuchukua muda na uhitaji uvumilivu. Jifunze toka kwa wajasiriamali waliofanikiwa na utagundua kwamba mafanikio yao yalichukua muda.

2. Kuwa mbunifu

Ili kupata mafanikio katika biashara, ni muhimu kwa wajasiriamali kujenga upekee katika bidhaa au huduma wanazotoa. Tafuta namna ya kujitofautisha na washindani wako. Wajasiriamali wengi wamefanya mambo ambayo tu wameona wengine wanafanya. Wengi wameingia katika biashara kwa kuiga toka kwa wenzao yale wanayofanya. Yafaa mjasiriamali kuwa mbunifu na kuacha kuiga kila unachokiona toka kwa wenzako. Ni muhimu kwa wajasiriamali kuwa na upekee wa bidhaa au huduma, kwani ni njia nzuri zaidi ya kudhibiti soko. Elewa biashara katika zama hizi zina ushindani wa hali ya juu na changamoto ni nyingi. Sasa ili kukabiliana na changamoto hizo unapaswa kujitofautisha.

3. Watambue wateja wako.

Wateja ni msingi wa kuendelea kwa biashara yoyote kwa sababu bila wateja wa kuwauzia bidhaa hakuna biashara itakayoendelea. Kwa namna yoyote unayoweza kuwaita wateja wako, elewa tu kuwa ni watu muhimu sana katika biashara yako. Bila wao hakuna utakachofanya hata kama una bidhaa bora kiasi gani, unauza kwa bei gani, uko wapi na unatumia mbinu gani katika biashara. Jenga uhusiano mzuri na wateja wako. Hakikisha wateja wanapata kile wanachohitaji na epuka kuwa sehemu ya maudhi kwa wateja, Jiulize katika biashara yako umewahi kufanya nini katika kuwathamini na kuwajali wateja wako. Kama wateja wanaona unawajali na kuwathamini basi nao pia watakujali kwa kuendelea kufanya bishara na wewe kwa muda mrefu zaidi na watazidi kukuamini.

Zaidi ya kuendelea kuwa na wewe, wateja walioridhika na wewe watakuwa chanzo kizuri cha kutangaza biashara yako, kwani watawaambia wengine. Kitendo cha kuwaambia wengine kitakuwa mwanzo mzuri wa wewe kujenga msingi wa wateja bila gharama.

4. Tengeneza mtandao.

Pamoja na kuwa na namna bora ya kuwashika wateja wako ni muhimu kujenga mtandao mzuri na wengine Kuwa mtu wa kujichanganya na wengine, usione washindani wako kama maadui. Tunapozungumzia kujenga mtandao maana yake ni kutafuta namna bora ambayo itakufanya wewe na biashara yako, mfahamike bila gharama kubwa.

5. Jitengenezee soko lako maalumu.

Kama ungependa biashara yako ifahamike kati ya biashara nyingine ni muhimu kuwa na soko lako maalum linaloeleweka. Hii ni njia ya pekee ya kukutofautisha na washindani wako. Kumbuka kuwa kuna fursa nyingi sana za biashara ambazo watu wanaweza kuzitumia, tatizo lililopo ni lile la watu kufanya mambo kimazoea. Lakini kama watu wangefanyia kazi fursa hizi ingetoa nafasi kwa wao kupata mafanikio.

6. Jenga mazingira ya kupata faida endelevu.

Ikiwa unafanya aidha biashara ya huduma au bidhaa, ni muhimu kutathmini bei ya bidhaa uliyopanga ili kupata faida endelevu. Jiulize je bei uliyopanga inaendana na uhalisia katika soko?. Hili la upangaji wa bei za bidhaa ni jambo la msingi kulifikiria kwani ni hapa ambapo tunaweza kujenga faida endelevu. Usifikiri kupanga bei ya chini ndio njia ya kuvutia wateja au kupanga bei ya juu ni kufukuza wateja, la muhimu ni kucheza na soko.Endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa mambo mazuri ya kujielimisha na kujihamasisha na kuwa bora zaidi jiunge na KISIMA CHA MAARIFA.

TUNAKUTAKIA MAFANIKIO MEMA KATIKA UJASIRIAMALI NA BIASHARA YAKO NA TUPO PAMOJA.

Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika, Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika kujifunza zaidi.

kitabu-kava-tangazo4323