Jinsi ambavyo mtu anakuwa na njaa kali ndivyo jinsi ambavyo akili yake inafikiria sana na pia anasikia sana harufu ya chakula. Tarkad mtoto wa Azure, alifikiria hivi. Na kwa siku mbili alikuwa hajapata chakula cha maana zaidi ya matunda aliyochuma kwenye bustani. Hakuweza kupata matunda mengine ya kula kwa sababu alifukuzwa na wanawake waliokuwa wanauza matunda yale.
Aliendelea kuzunguka mitaa ya Babeli huku akipita karibu na nyumba za chakula akiamini anaweza kukutana na mtu anayemfahamu na akamnunulia chakula au kumkopesha fedha. Kwa kustukizwa alijikuta uso kwa uso na mtu ambaye hakutamani kabisa kukutana nae. Alikuwa ni Debasir, mfanyabiashara wa ngamia wa babeli. Debasir alimfanya Tarkad ajisikie vibaya sana kwa sababu Tarkad alishindwa kumlipa fedha aliyokopeshwa.
Debasir alimwangalia na kumwambia afadhali nimekutana na wewe, nipe fedha zangu nilizokukopesha miezi mingi iliyopita. Tarkad alimwangalia kwa wasi wasi na kwa jibu kwa woga kwa kumwambia samahani sana,kwa leo sina fedha ya kukulipa. Debasir akamwambia basi tafuta fedha unilipe, kwa mwanaume kama wewe huwezi kushindwa kupata fedha. Tarkad alimjibu, mimi nina bahati mbaya ndio maana nashindwa kulipa madeni.
Debasir aliuliza kwa mshangao, una bahati mbaya! Unaweza kulaumu miungu kwa matatizo yako ila bahati mbaya inakwenda kwa watu ambao wanafikiria kukopa zaidi ya kulipa, Debasir aliendelea kumwambia. Debasir alimwambia Tarkad amfuate wakati anaenda kula kisha atampa hadithi moja itakayomfundisha. Tarkad alionekana mnyonge ila angalau alipata mtu wa kumkaribisha kwenye nyumba ya chakula.
Waliingia kwenye nyumba ya chakula na kukaa kwenye kona. Mhudumu alipokuja kuwahudumia, Debasir alimwambia niletee mguu wa mbuzi na mkate na mboga mboga na juisi kwa sababu nina njaa sana. Akamwambia usimsahau na rafiki yangu hapa, mletee jagi la maji, leta ya baridi maana kuna joto kali. Tarkad alihuzunika sana kwa sababu atakaa pale akimwangalia mtu anakula mguu wa mbuzi wakati yeye anakunywa maji tu. Lakini hakuwa na la kusema maana hakuwa na fedha. Debasir alikuw amuongeaji sana na kila mtu alikuwa anamjua.
Alimwambia Tarkad, nimesikia kutoka kwa msafiri aliyetoka Urfa kwamba kuna tajiri mmoja ambaye ana kipande chembamba sana cha jiwe ambacho mtu anaweza kuona kupitia kipande hiko cha jiwe. Analiweka jiwe hilo dirishani ili kuzuia mvua. Aliendelea kusema jiwe hilo ni la rangi ya njano na ukiangalia kupitia jiwe hilo unaoina dunia tofauti na ulivyoizoea. Alimuuliza Tarkad wewe unafikiriaje? Unafikiri mtu anaweza kuiona dunia tofauti na alivyoizoea? Nadhubutu kusema hivyo, alijibu Tarkad, huku macho na mawazo yake yakiwa kwa ile nyama ya mbuzi iliyokuwa mbele ya Debasir.
Debasir aliendelea kuongea na kusema ni kweli, mimi mwenyewe nimeiona dunia kwa rangi tofauti na ilivyo na hadithi ninayokwenda kukupa aitakufundisha ni jinsi gani ya kuiona dunia kwa rangi sahihi. Waliokuwa wamekaa jirani na meza yao walimsogelea Debasir maana walimjua kwa utoaji wake wa hadithi. Debasir aliendelea kula na Tarkad ahakupewa nafasi ya kuonja hata mkate uliodondoka chini.
Debasir alianza kwa kusema hadithi anayokwenda kutoa inahusiana na maisha yake ya ujana na jinsi alivyokuwa mfanyabiashara wa ngamia. Aliwauliza kama wanajua kwamba alishawahikuwa mtumwa Syria. Kulikuwa na minong’ono ya kushangaa ambapo Debasir aliacha kuongea na kuisikiliza kidogo.
Debasir aliendelea kusema, nilipokuwa kijana nilijifunza biashara ya baba yangu. Ilikuwa ni kazi ya kutengeneza viti vinavyotumika kukalia kwenye wanyama. Nilifanya nae kazi kwenye karakana yake na niliweza kupata kipato kidogo. Aliendelea kusema kwamba alioa na kipato hiko kidogo hakikuweza kumtosheleza yeye na mke wake. Alianz akupata tamaa ya vitu ambavyo hakuwa na uwezo navyo. Hivyo alianza kukopa akiahidi kulipa baadae. Alisema kwa kuwa kijana na kukosa uzoefu hakujua kwamba mtu anayetumia zaidi ya anachopata anajitengenezea matatizo yake mwenyewe. Alijitahidi kulipa madeni yake lakini baada ya muda aligundua kwamba kipato chake hakitoshelezi kulipa madeni na kupata hela ya kuishi. Waliokuwa wanamdai walianza kumfatilia kwa nguvu na maisha yake yalianz akuwa magumu sana. Anasema alikopa kwa marafiki zake na hakuweza kuwalipa pia. Baadae mke wake aliondoka na kurudi nyumbani kwao, aliamua kuondoka babeli na kuhamia mji mwingine ambapo angeweza kuanza upya.
Debasir aliendelea kusema kwamba kwa miaka miwili alifanya kazi kwenye misafara ya usafirishaji na baadae alijikuta akiwa mmoja wa majambazi ambao waliteka misafara ya usafirishaji. Aliendelea kusema kwamba hiyo sio tabia ambayo ingefaa kwa mtoto wa baba yake na hiyo ni kwa sababu alikuwa anaiona dunia kwa rangi ya tofauti. Anasema mara ya kwanza walifanikiwa kuteka msafara na kuiba. Mara ya pili hawakufanikiwa kuteka na kuiba badala yake walishambuliwa na kukamatwa. Walichukuliwa na kwenda kuuzwa kama watumwa.
Debasir alinunuliwa kwa fedha mbili na mfalme wa jangwani. Aliendelea kusema, watu wale wa jangwani ni wakali na wana roho mbaya sana. Alipelekwa mbele ya wake wa nne wa yule bwana aliyemnunua, mke wa kwanza aliyeitwa Sira alimchagua awe kijakazi wake kwa ajili ya kuendesha ngamia na kuwatumikia. Alianza kazi kwa kumuendesha Sira kuelekea kumuona mama yake aliyekuwa anaumwa. Wakiwa njiani alimshukuru Sira kwa kumchagua awe mtumwa wake. Alimwambia kwamba yeye sio mtumwa bali ametoka kwenye familia bora na ni maisha tu yamemfikisha pale. Sira alimwambia utasemaje kwamba wewe sio mtumwa wakati umekimbia matatizo babeli? Kama mtu sio mtumwa, hawezi kukubali kuwa mtumwa hata kama mazingira ni magumu kiasi gani.
Tutaendelea na sehemu hii ya uchambuzi kwenye makala ijayo…
Nakutakia kila la kheri katika kufikia uhuru wa kifedha.
TUPO PAMOJA.