Fedha ndio damu ya biashara au ujasiriamali wa aina yoyote. Baada ya kuwa na wazo zuri la kijasiriamali kinachofuata ni utekelezaji ambao unahitaji fedha. Na kwa kuwa fedha hazipatikani kirahisi inawalazimu wajasiriamali wengi kuanza kidogo na kuendelea kukua kadiri siku zinavyozidi kwenda. Leo tutajadili umuhimu wa taasisi za fedha kama benki, saccoss, vicoba na hata taasisi nyingine zinazotoa mikopo ya kibiashara katika maendeleo ya mjasiriamali..

Taasisi za fedha ni muhimu sana kwenye maendeleo ya mjasiriamali. Kupitia taasisi hizi mjasiriamali anaweza kupata mkopo ambao unaweza kukuza biashara yake kwakiasi kikubwa sana. Kwa mkopo mjasiriamali anaweza kununua vitendea kazi vingi zaidi, kuboresha biadhaa au huduma anazotoa na hata kujitangaza zaidi. Mambo yote haya yataongeza wateja zaidi na hivyo kuleta faida kubwa kwenye biashara.

Japokuwa taasisi hizi hazitoi mkopo kwa watu wanaokwenda kuanza biashara kitu ambacho kimekuwa kikwazo kwa watu wengi, bado unaweza kuzitumia vizuri baadae ili kuweza kukua zaidi. Sababu kubwa inayozifanya taasisi hizi zisitoe mikopo kwa wanaokwenda kuanza biashara ni hatari kubwa ya biashara kushindwa. Biashara yoyote inayoanza ipo kwenye hatari kubwa ya kushindwa kutokana na changamoto mbalimbali na kukosa uzoefu wa kuendesha biashara kwa mfanyabiashara anayeanza. Hivyo kama ukipewa mkopo kwenda kuanza biashara unaweza kuwa mazigo kwako.

Kutokana na changamoto hii inakulazimu wewe mjasiriamali kuanza kidogo kwa fedha zako za akiba au unazoweza kupata kwa njia nyingine ambayo sio mkopo. Baada ya kuwa kwenye biashara kwa muda na kuonesha kuimudu biashara hapa ndipo unapoweza kupata fedha kutoka kwa taasisi hizi za kifedha. Kwa Tanzania taasisi nyingi zinatoa mikopo kwa biashara ambayo tayari imefanyika kwa zaidi ya miezi sita na pia kuna taasisi nyingine zinataka muda mrefu zaidi ya hapo.

Ni vigezo gani unatakiwa kuwa navyo ili kuweza kunufaika na taasisi hizi?

Huenda kigezo cha kwanza kwamba uwe kwenye biashara kwa zaidi ya miezi sita tayari unacho. Ila bado huna sifa ya kupewa mkopo wa kibiashara. Hii inatokana na wewe mjasiriamali kukosa vigezo muhimu unavyotakiwa kuwa navyo ili taasisi iweze kukuamini na kukupa mkopo. Baadhi ya vigezo hivyo ni;

1. Biashara iwe imesajiliwa. Wajasiriamali wengi wadogo wanafanya biashara zao kwa mazoea tu. Biashara nyingi ndogo ndogo Tanzania hazijasajiliwa katika mamlaka husika. Unahitaji kusajili biashara yako kwenye mamlaka ya mapato(TRA) na kupewa namba ya mlipa kodi. Pia unahitaji kusajili biashara yako katika halmashauri ya wilaya au manispaa unayofanyia biashara hizo na hapo kupewa leseni ya kufanya biashara. Pia kama uko makini zaidi na biashara yako unaweza kusajili jina la biashara yako kwenye mamlaka inayohusika na kusajili kampuni na biashara(BRELA) au hata unaweza kuisajili biashara yako kama kampuni. Unaweza kuona kufuata mlolongo wote huu unapoteza fedha nyingi ila ukweli ni kwamba utanufaika zaidi ya fedha utakazotumia kusajili biashara yako. Taasisi za fedha hazitoi mkopo kwa biashara ambayo haitambuliki popote.

2. Kuwa na taarifa ya fedha ya biashara yako. Ili taasisi iweze kukukopesha wewe fedha inahitaji kuona taarifa yako ya fedha ya kipindi kifupi kilichopita. Taarifa hiyo itaiaminisha taasisi kwamba mzunguko wako wa fedha ni mzuri na hivyo unaweza kurudisha mkopo utakaopewa. Ili kuweza kuwa na taarifa nzuri ya fedha unahitaji kufungua akaunti ya benki kwa ajili ya biashara yako, iwe ni akaunti ya biashara. Pia unahitaji kupeleka mapato yako kwenye akaunti yako ikiwezekana kila siku. Sio lazima fedha hizo uziweke kwenye akaunti hiyo kama akiba, unaweza kuweka na kuzitoa baada ya siku chache, hii itakusaidia wewe kuonesha uhai wa biashara yako kutokana na mzunguko huo wa fedha.

3. Unahitaji kuwa na dhamana. Ili kupata mkopo wa biashara unahitaji kuwa na dhamana ya kitu ambacho kinaweza kufidia mkopo wako kama utashindwa kuulipa. Biashara yenyewe kama ina rasilimali za kutosha inaweza kujidhamini yenyewe. Na pia baadhi ya taasisi zinaweza kukubali mtu mwingine akudhamini wewe, hivyo unahitaji kuwa mwaminifu kwa watu ili waweze kukusaidia kwa kukudhamini.

Tumia taasisi za fedha kukuza na kuboresha zaidi biashara yako. Jijengee mazingira yatakayokufanya uweze kukopesheka ili uweze kutumia mkopo huo kuendeleza biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.