Karibu tena msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA katika kipengele hiki cha jinsi ya kujijengea tabia za mafanikio. Kwa zaidi ya miezi sita sasa tumekuwa tukijadili jinsi ya kujijengea tabia ambazo zitatuwezesha kufikia mafanikio. Moja ya sababu kubwa kwa nini watu wengi hawafanikiwi licha ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa ni baadhi ya tabia walizonazo ambazo zinawazuia kufanikiwa. Kwa mfano unaweza kufanya kazi kwa bidii na maarifa na ukapata kipato kizuri ila kwa vile una tabia mbovu kwenye matumizi ya hela kila siku ukawa unashindwa kufikia mafanikio.

Mpaka sasa tumeshajadili tabia muhimu sana kama matumizi ya fedha, kutunza muda, kujijengea tabia ya kujisomea, kujijengea nidhamu binafsi na hata kujijengea kujiamini. Rudia makala hizi mara kwa mara hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA ili uweze kuzifanya tabia hizi nzuri za mafanikio kuwa sehemu ya maisha yako.

Mwezi huu wa kumi na mbili tutajadili tabia ya kuahirisha mambo na jinsi tunavyoweza kuondokana nayo ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Katika kitu kimoja ambacho ni adui mkubwa wa mafanikio ni tabia ya kuahirisha mambo. Kwa wiki tano za mwezi huu wa kumi na mbili tutajadili yafuatayo.

1. Maana ya kuahirisha mambo na kwa nini watu wanaahirisha mambo.

2. Hasara za tabia ya kuahirisha mambo.

3. Jinsi ya kuondoa tabia ya kuahirisha mambo.

4. Vitu vinavyochochea tabia ya kuahirisha mambo na jinsi ya kuviepuka.

5. Uhusiano wa mafanikio na tabia ya kuahirisha mambo.

Nini maana ya kuahirisha mambo?

Kuahirisha mambo kwa kiingereza wanaita procrastination, ni tabia ambayo inamfanya mtu kusogeza mbele mambo ambayo angetakiwa kufanya sasa. Mambo haya yanayosogezwa mbele ni mambo muhimu na ambayo mtu angetakiwa kiyafanya sasa ili aweze kutekeleza majukumu yake au kufikia malengo yake. Na hata pale mtu anapopeleka mambo haya mbele, kwa wakati huu anakuwa hafanyi mambo ambayo ni muhimu kama yale aliyoyasogeza mbele.

Tabia ya kusogeza mambo mbele ni tabia ambayo inamuathiri kila mtu. Hata uwe mtu wa kutunza muda kiasi gani, kuna wakati utajikuta unakwepa baadhi ya majukumu yako au kuyasogeza mbele. Hivyo ni muhimu sana kujifunza kuhusu tabia hii ili kujua jinsi gani ya kuondokana nayo.

Tabia ya kuahirisha mambo ni kikwazo kikubwa sana kwenye kufikia mafanikio makubwa. Sababu kubwa mpaka sasa bado hujaweza kufikia malengo na mipango yako kwa asilimia kubwa ni tabia ya kuahirisha baadhi ya mambo ya msingi unayotakiwa kufanya.

Ni wakati gani ambapo unaahirisha mambo?

Unaweza kuwa unaahirisha mambo ila wewe mwenyewe ukawa hujui kwamba unafanya hivyo. Hii inatokana na kwamba tabia hii ya kuahirisha mambo imeshakuwa sehemu ya maisha yetu na hivyo tunaona ni kitu cha kawaida. Hapa nakupa baadhi ya mifano ya kuahirisha mambo inayotokea kwenye maisha yetu ya kila siku.

1. Mfanyakazi anakuwa na ripoti za kuandaa ila kila anapoanza kufanya kazi anaona kitu kingine kizuri cha kufanya, mfano kupanga vitu vizuri au kuinuka kwenye kiti na kwenda kuuliza kitu kwa mtu mwingine. Hii yote ni tabia ya kuahirisha mambo na ripoti hiyo haitamalizika kwa muda.

2. Unakuwa na majukumu yako uliyojipangia kufanya kwa siku ila kila baada ya muda mfupi unaingia kwenye mitandao hasa mitandao ya kijamii na email. Kila unaposema kwa sasa hutaingia kwenye mitandao hiyo unaona kama kuna kitu kinakupita hivyo unaoenda kuchungulia na unapotelea huko moja kwa moja.

3. Unataka kuanza biashara au ujasiriamali lakini kila siku unajipa sababu kwamba bado hujapata wazo zuri la biashara, bado hujapata mtaji wa kutosha. Hizi zote ni njia unazotumia kuahirisha mambo.

4. Mwanafunzi anajua kabisa anatakiwa asome ili aweze kufanya vizuri kwenye masomo yake ila anaona bado ana muda mrefu mpaka mtihani ufike. Baadae anstuka mtihani huu hapa na hajasoma vile anavyotakiwa kusoma. Hii inatokana na tabia ya kuahirisha mambo.

Kwa nini watu wanahirisha mambo?

Zamani jibu la haraka ilikuwa ni kwamba kuahirisha mambo ni uvivu. Ila sasa watu wamesomea na kufanyia utafiti tabia hii na wanasaikolojia wanakubali kwamba tabia ya kuahirisha mambo ni tabia ambayo watu wamejijengea kwa muda mrefu. Mtu anaweza kuwa mchapakazi mzuri ila bado akajikuta na tabia hii ya kuahirisha mambo.

Zifuatazo ni baadhi ya sababu kwa nini watu wanapenda kuahirisha mambo, ikiwemo na wewe;

1. Kutokujua jinsi ya kufanya jambo.

Moja ya sababu kwa nini watu wanahirisha mambo ni kukosa utaalamu wa kufanya jambo husika. Au kutokujua ni jinsi gani wanaweza kufanya jambo hilo. Na hivyo badala ya kujifunza jinsi ya kulifanya wanatafuta kitu rahisi zaidi cha kufanya.

2. Kukosa mapenzi na kitu unachofanya.

Sababu nyingine inayowafanya watu kuahirisha kufanya jambo ni kukosa mapenzi na jambo hilo. Kwa mfano kama unafanya kazi ambayo huipendi ni rahisi sana kwako kuahirisha baadhi ya majukumu yako. Lakini kama unapenda unachofanya unakuwa na shauku kubwa sana ya kukifanya.

3. Kukosa hamasa.

Unahitaji hamasa ili kuweza kufanya jambo lolote. Hamasa hiyo inaweza kutoka ndani yako mwenyewe au nje yako. Ndio maana watu wanaweza kufanya kitu ambacho hawapendi kufanya ila kwa kuwa wanapewa sifa au wanapewa fedha. Kukosa hamasa ni moja ya sababu kubwa sana zinazowafanya watu kuahirisha mambo.

4. Kuogopa kushindwa.

Unapofanya jambo jipya kama kuanza biashara au ujasiriamali mara nyingi unakuwa huna uhakika wa kufanikiwa. Nafasi ya kushindwa inaonekana ni kubwa kuliko ya kufanikiwa. Kuwepo kwa hali hii ya kushindwa kunawafanya watu wengi kuahirisha kuanza kufanya jambo kwaa kuepuka kushindwa. Hii ndio sababu kubwa inayiwafanya watu wengi kushindwa kuingia kwenye biashara.

5. Kuogopa kufanikiwa.

Usishangae, ndio unaahirisha kufanya jambo kwa sababu unaogopa kufanikiwa. Sasa hivi unaona unaishai maisha ambayo ni sawa kwako, na kama ukifanikiwa zaidi ya hapo watu wengi wataanza kukuangalia kwa jicho la tofauti. Wengine watakuona wewe ni mwizi au fisadi, wengine watategemea uwagawie fedha na kadhalika. Hali hizi zinawafanya baadhi ya watu waogope kufanikiwa na hivyo kujikuta wanaahirisha mambo.

6. Kuogopa kukataliwa.

Mara nyingi watu wanaahirisha kufanya mambo kwa sababu wanaogopa kukataliwa. Kwa mfano mtu anaweza kuwa anahitaji msaada kutoka kwa wengine ili aweze kukamilisha majukumu yake. Kwa sababu anafikiri akiwaambia watamkatalia mtu huyo anaahirisha majukumu hayo moja kw amoja.

Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazokufanya uahirishe kufanya mambo ya msingi na hivyo kupoteza muda mwingi na kushindwa kufikia mafanikio makubwa.

ZOEZI LA KUFANYA.

Kaa chini na utafakari ni jinsi gani ambavyo umekuwa unaahirisha ammbo ya msingi kwenye maisha yako. Pia orodhesha ni mambo gani ambayo umeahirisha mpaka sasa na ni sababu zipi ulizotumia na unazoendelea kutumia.

Tukutane wiki ijayo kwenye muendelezo.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.