Moja ya mahitaji makubwa ya kila binadamu ni kukubalika kwa kile anachofanya. Tuna njaa kubwa sana ya kuona watu wakitukubali kutokana na mambo tunayofanya. Unapenda watu wakuone wewe ni mfanyakazi bora au kiongozi bora au mfanyabiashara bora.
Pamoja na watu wengi kupenda kukubalika kwa kile wanachofanya bado ni wachache sana ambao wanaweza kufikia hali hiyo. Je kufikiwa na wachache kwa hali hii ina maana kwamba kuna baadhi ya vitu unaweza kuwa bora sana na vingine haviwezekani?
Jibu ni hapana, kwenye kila kitu ambacho kinafanyika duniani mtu anaweza kuwa bora kuliko watu wengine wote duniani katika kukifanya. Namaanisha hata wewe unaweza kuwa bora sana kwenye hiko unachofanya au unachotarajia kufanya. Unachohitaji ni kuwa na mbinu za kukuwezesha kufikia ubora huo wa hali ya juu.
Kufikia ubora wa viwango vya kimataifa ni kitu ambacho unakifanya kila siku. Sio kitu cha kufanya mara moja halafu ndio unakuwa bora na kuendelea kubaki kwenye ubora. Bali ni kitu ambacho unakifanya kila siku na unakitengea muda kidogo.
Jinsi ya kufikia ubora wa hali ya juu.
Leo nakushirikisha mambo matatu muhimu ya kufanya ili uweze kufikia ubora wa hali ya juu sana.
1. Penda kile unachofanya.
Hii ndio njia ya kwanza na muhimu sana. Kama hupendi unachofanya sahau kabisa kuwa bora kwenye kitu hiko. Naposema kukipenda pia simaanishi ukipende kwa sababu kinakupatia fedha, bali kipende kwa sababu ndio kitu unachokithamini sana. Na kama unakithamini sana utakuwa tayari kukifanya kwa moyo mmoja bila ya kujali unapata fedha au la. Utakuwa tayari kukifanya kwa sababu unajua unaleta mabadiliko makubwa duniani.
Kupenda unachofanya ni hatua ya kwanza kabisa ya kufikia viwango vya hali ya juu kabisa.
2. Gawa hiko unachokipenda katika sehemu ndogo sana.
Baada ya kujua unachopenda kufanya, bado huwezi kufanya kila kitu katika nyanja hiyo. Kwa maana hii unachagua sehemu ndogo ambayo unaweza kuifanyia kazi na kubobea kwa hali ya juu. Usijaribu kufanya kila kitu, utaishia kuwa hovyo, chagua kufanya machache ambayo kwa kuwekeza nguvu zako unaweza kuleta mabadiliko makubwa.
3. Tenga dakika 20 kila siku kufanya jambo kuhusiana na eneo ulilochagua.
Baada ya kujua unachopenda kufanya na baada ya kugawa katika sehemu ndogo ambayo unaweza kuifanyia kazi vizuri sasa unahitaji kufanya jambo kila siku litakalokusogeza mbele katika jambo hilo ulilochagua. Unahitaji muda mchache sana kila siku ambao hautaharibu ratiba zako.
Tenga dakika 290 kila siku za kujifunz akuhusu jambo hilo, kulifanya na hata kulifuatilia kwa undani zaidi. Unaweza kufanya hata ika wa saa moja kwa siku. Kinachotakiwa ni angalau kila siku kufanya kitu kwenye jambo hilo, ukisema unachagua siku moja na kufanya mambo yanayohusika na jambo hilo kwa muda mrefu bado huwezi kunufaikia kama utakavyofanya kila siku kwa muda mfupi.
Jiandae kuwa bora sana kw akile unachofanya, inawezekana. Hakuna wa kukuzuia bali wewe mwenyewe.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia ubora wa hali ya juu sana.
TUPO PAMOJA.