Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON.

Sharru Nada alikuwa mfanya biashara ambaye alipenda sana kuvaa vitu vya thamani na mavazi ya kitajiri. Kwa muonekano wa nje alionekana ni mtu wa kujiweza ila kwa ndani alikuwa na matatizo makubwa.

Alikuwa akiongoza msafara wake wa kibiashara kutoka Damascus kwenda Babeli. Japokuwa njia ilikuwa na vitishi vikubwa yeye hakuhofia chochote. Kulikuwa na watekaji nyara katika njia hiyo ila yeye alikuwa na ulinzi wa kutosha.

Katika msafara huu aliongozana na kijana aliyekuwa naitwa Hadan Gula. Huyu alikuwa mjukuu wa rafiki yake ambaye alifanya nae biashara kwa muda mrefu. Alijisikia ana deni la kumlipa rafiki yake huyo na hivyo kumsaidia mjukuu wake. Alitamani kufanya kitu kumsaidia kijana huyo lakini ilikuwa vigumu kwake kutokana na jinsi kijana yule alivyokuwa.

Alikuwa anamwangalia kijana yule ambaye alikuwa maevaa bangili na hereni na kujisemea kwamba anafikiri mapambo ni ya wanaume. Aliendelea kujisemea kwamba kijana yule alifanana sana na babu yake ila babu yake hakuwa na tabia kama za kijana yule. Alimchukua kwenye msafara ule ili aweze kumsaidia kuondokana na matatizo aliyoyapata baada ya kurithi mali za babu yake yeye na baba yake.

Hadan Gula alimuuliza Sharru Nada, kwa nini unafanya kazi sana na kila siku unakuwa kwenye misafara ya kibishara, huna muda wa kupumzika na kufurahia maisha? Aliendelea kumwambia kwamba kama yeye ndio angekuwa na utajiri wake huo angeishi kama mtoto wa mfalme. Asingehangaika na misafara ya kuchosha na angevaa vitu vizuri na vya thamani kubwa.

Sharru Nada alimjibu kwa kumwambia babu yako hakuvaa vito hivyo vya thamani na akamwambia je hataacha muda wa kufanya kazi? Hadam Gula alimjibu kazi ni kwa ajili ya watumwa. Sharru Nada alikaa kimya na kuendelea na safari huku akitafakari mtazamo wa kijana yule. Mbeleni alimuonesha eneo lenye kijani sana kwa mbali na kumwambia ule ndio mji wa babeli na mnara mkubwa unaouona ni mnara wa babeli. Hadan Gula alimwambia kwa hiyo ile ndio babeli? Mji tajiri kuliko yote duniani? Aliendelea kusema kwamba babeli ndipo babu yake alipatia utajiri na kama wangeendelea kuishi pale asingekuwa kwenye hali ngumu aliyonayo sasa. Aliendelea kusema angetamani roho ya babu yake iendelee kuwepo ili yeye na baba yake wawe katika hali nzuri, maana waliachiwa urithi ila wote umepotea kutokana na kutokujua siri na kutunza na kukuza utajiri.

Sharru Nada hakujibu chochote, waliendelea na safari na walipita pembeni ya shamba kubwa. Katika shamba hilo aliwaona watu ambao aliwakuta wakifanya kazi hapo miaka 40 iliyopita. Alifikiri ni watu tofauti ila alipoangalia kwa makini alikumbuka ni watu wale wale. Alifikiria jinsi ambavyo miaka 40 iliyopita alivyotamani kazi za watu wale na kama angepewa nafasi ya kubadilishana nao angefurahi sana kupata kazi ile. Lakini sasa miaka 40 imepita ameweza kutengeneza utajiri mkubwa sana. Alimwambia Hadan Gula kwamba watu hawa wamekuwa kwenye shamba hili kwa miaka 40 na wanafanya kazi ile ile, inaonesha ni jinsi gani mawazo yao hayajabadilika kwa miaka 40.

Mawazo mengi yalimjia kichwani kwake kwa miaka 40 iliyopita na jinsi mambo yalivyobadilika na picha ya rafiki yake ilimjia tena kichwani. Ila kila alipomwangalia mjukuu wake alikosa matumaini atamsaidiaje. Maana kama ni kazi anazo za kutosha ila kijana yule anajiona sio mtu wa kufanya kazi ngumu na anapenda vitu vya thamani. Baada ya muda alipata mpango kwenye mawazo yake, ulikuw ampango mgumu lakini kwa kuwa huwa anafanya maamuzi magumu alikubaliana nao.

Alimuuliza Hadan Gula, je ungependa kujua jinsi gani mimi na babu yako tulikuwa washirika kwenye biashara? Hadan alimjibu kwa nini usiniambie umewezaje kutengeneza utajiri? Hiko ndio nataka kusikia. Sharru Nada alipuuzia jibu hilo na kuanz akumpatia historia yao. Alimwambia walianza kama wafanyakazi kwenye shamba lile na walikuwa wakifanya kazi ngumu kuliko wale waliowaona pale. Alimwambia yeye pamoja na babu yake na watu wengine wengi walikuwa watumwa na walifanyishwa kazi gumu sana. Hadan alishangaa sana kusikia kwamba walikuwa watumwa maana babu yake hakuwahi kumwambia historia hiyo. Alimjibu kwamba babu yake alikuwa mtu mpole sana na asiyekuwa na maneno mengi.

Hadan Gula alimwambia niambie ilikuwaje mpaka mkawa watumwa. Sharru Nada alimjibu kwamba mtu yeyote anaweza kujikuta amekuwa mtumwa. Alimwambia yeye alijikuta utumwani baada ya kaka yake kuua mtu na hivyo yeye kuchukuliwa na mke wa yule aliyeuawa mpaka watakapoweza kulipa fidia. Waliposhindwa kulipa fidia mwanamke yule alikasiriaka na kumuuza kama mtumwa. Hadan Gula alisema huo ni uonevu mkubwa sana, alimwambia amweleze waliwezaje kuwa huru tena. Sharru Nada alimwambia tutafika huko wacha tuendelee na hadithi kwanza.

Sharru Nada aliendelea kueleza kwamba wakati wakiwa kwenye msafara wa kupelekwa babeli kama watumwa walisikia habari nyingi sana njiani kwamba watumwa babeli wanafanya kazi nyingi sana mpaka wanakufa. Maneno yale yalimtisha sana na usiku kucha hakuweza kulala. Alimfata mlinzi aliyekuwa analind amsafara ule na kumuuliza kama wakifika babeli watauzwa kama watumwa. Mlinzi yule alimuuliza kwa nini unataka kujua? Sharru alimsihi sana kwmaba yeye bado ni kijana na anataka kuishi na sio kufa kama mtumwa, hivyo nataka kujua kama naweza kupata bwana mzuri. Mlinzi yule alimshauri kwamba watakapofika kuuzwa akitoke amnunuaji amwambie kwamba yeye anafanya kazi kwa nguvu, na asilete ubishi maana akikosa mtu wa kumnunua ataishia kufanya kazi ngumu kwenye ukuta wa babeli.

Walipofika babeli walishangaa kuona watumwa wengi sana wakifanya kazi ngumu huku wale wanaoshindwa wakipewa adhabu kali sana.Aliangalia jinsi watu walivyokuwa wamebeba matofali na walishindwa walisukumwa pembeni na kuumia hata kufa. Aliangalia hali ile na kusema hiki ndio kinachomsubiri kama akikosa mtu wa kumnunua kwenye soko la watumwa. Meggido alikuwa mmoja wa watumwa waliokuwa kwenye msafara ule na walikuw kaziru sana na Sharru. Baada ya kuona kuna uwezekano mkubwa wa kutengana na kila mtu kwenda kivyake Meggido alimshauri Sharru kitu kimoja, alimwambia ipende sana kazi, kama utanunuliwa na mtu fanya kazi ka juhudi zako zote, hata kama mtu huyo hataithamini kazi hiyo wewe ithamini. Ifanye kazi kamarafiki yako, usiogope au kufikiri sana kwa sababu ni ngumu, ifanye kwa juhudi kubwa na fikiria unachokizalisha jinsi ambavyo kinawasaidia watu wengi.

Baada ya karibu watumwa wote kununuliwa na Sharru kuona kwamba anaweza kukosa mtu wa kumnunua na hivyo kwenda kufanya kazi kwenye ukuta wa babeli, alitokea bwana mmoja na Sharru alimfuata na kumshawishi kwamba yeye ni kijana anayependa kufanya kazi na kama akimnunua atamzalishia sana. Mtu yule alivutiwa na Sharru na hivyo kumnunua. Siku hiyo Sharru alijiona ni mtu mwenye bahati kuliko wote babeli.

Tutaendelea na simulizi hii yenye kutufunza mengi kwenye uchambuzi ujao.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia uhuru wa kifedha.

TUPO PAMOJA.