Tabia ya kuahirisha mambo ni adui mkubwa sana wa kufikia mafanikio makubwa. Hii ni tabia ambayo ipo kwa watu wengi na ni tabia rahisi sana kuifuata kutokana na asili ya binadamu ya kutopenda kufanya mambo yanayochosha au kuumiza.

Kwa bahati nzuri ni kwamba unaweza kuondokana na tabia hiyo ya kuahirisha mambo na ukawa na uzalishaji mkubwa utakao kuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo unayoweza kuyafanya ili kuondoa tabia ya kuahirisha mambo.

1. Ondoa hofu ya kushindwa.

Hofu ya kushindwa ni moja ya vitu vinavyokufanya uendelee kuahirisha kufanya au kuanza kufanya mambo uliyopanga kufanya. Unapoona kwamba unaweza kushindwa hamasa ya kuanza jambo hilo inakuwa ndogo sana. Ondoa hofu ya kushindwa na ona kwamba unaweza kufanikiwa kama utaweka juhudi na maarifa. Pia usijione kwamba wewe umeshindwa kutokana na kuwa na tabia ya kuahirisha mambo. Amini kwamba unaweza kuondokana na tabia hiyo na kufikia mafanikio makubwa.

2. Tumia tabia ya kuahirisha mambo kama nafasi ya kujijua zaidi.

Kila unapopanga kufanya jambo halafu ukaahirisha, tumia muda huo kujijua zaidi. Jua ni kitu gani kimekufanya uahirishe jambo hilo, jua ni sababu zipi ambazo umejipa za kujihalalishia kuahirisha ulichopanga kufanya na pia jua ni kitu gani unaona rahisi kufanya na hivyo kinakuzuia kufanya mambo uliyopanga kufanya. Kwa kujua vitu hivi inakuwa rahisi kwako kuweza kuepuka mtego huo wa kuahirisha mambo wakati mwingine. Tabia ya kuahirisha mambo ni kama mtego na hivyo bila kuujua unajikuta kila mara unanasa kwenye mtego huo.

3. Fanya tathmini ya muda mfupi na muda mrefu wa jambo husika.

Pale ambapo unapanga kufanya jambo halafu ukaanza kuona unaahirisha, jipe muda wa kufanya tathmini za muda mfupi na muda mrefu ya faida ya jambo hilo. Mara nyingi huwa tunaahirisha mambo bila ya kujua ni kiasi gani tunapoteza au ni jinsi gani tunajinyima faida kubwa baadae. Kwa kujua faida ambazo ungezipata kwa kufanya jambo hilo, kila muda unaotumia kuliahirisha unajua kabisa kwamba unapoteza faida ambayo ungeipata kama ungefanya jambo hilo.

4. Kuwa na malengo na mipango inayoeleweka.

Kwa kuwa na malengo makubwa kwenye maisha yako na pia kuweka mipango ya kufikia malengo hayo utajua ni kitu gani unatakiwa kufanya ili kufikia malengo hayo. Hivyo tabia ya kuahirisha mambo inapokujia unajua moja kwa moja kwamba kwa kuendekeza tabia hiyo unajinyima nafasi ya kufikia malengo yako makubwa. Kila mara jipe picha ya jinsi maisha yako yatakuwa bora kama ukifikia malengo uliyojiwekea, hii itakusukuma na kukuondolea tabia ya kuahirisha mambo.

5. Kuwa na orodha ya mambo unayofanya kila siku na kila saa.

Muda ni kitu cha ajabu sana, unaweza kujiona unao muda mwingi na wa kutosha ila unashangaa siku inaisha hujafanya jambo lolote la kukufikisha kwenye mafanikio makubwa. Kila siku asubuhi, au jioni kabla ya kulala, orodhesha kwenye kijitabu chako mambo ambayo unataka kuyakamilisha kwenye siku husika. Yapange mambo hayo kutokan na umuhimu wake, yaani jambo lililopo kwenye nafasi ya kwanza kwenye orodha liwe ndio jambo muhimu kuliko yote, likifuatiwa na mengine katika utaratibu huo. Pia weka muda maalumu wa kufanya kila jambo uliloweka kwenye orodha. Yafanye mambo hayo kwenye muda uliojipangia na ukishakamilisha jambo likate kwenye orodha yako. Kwa kufanya hivi utajikuta unakamilisha mambo mengi kuliko pale ambapo utakuwa unafanya kiholela.

6. Gawa jambo katika sehemu ndogo ndogo.

Hii ni moja ya changamoto ambazo zinawazuia watu wengi kushindwa kukamilisha mambo waliyopanga kufanya. Labda nikuulize swali moja; unawezaje kumla tembo? Jibu ni rahisi, unamchukua tembo, unamchinja, unakata nyama vipande vidogo vidogo, unapika kisha unakula. Pamoja na urahisi huo lakini bado watu wengi wanakwama kwa kumuangalia tembo mzima na kusema ni vigumu sana kumla tembo kwa sababu ni mkubwa. Hivi ndivyo ilivyo hata kwenye mambo tunayopanga kufanya, usikatishwe tamaa na ukubwa wa jambo unalotaka kufanya, bali chukua jambo hilo na ligawe katika sehemu ndogo ndogo na kisha zifanyie kazi sehemu hizo. Baada ya muda utajikuta jambo uliloliona kubwa mwanzoni limekuwa dogo na rahisi kufanya.

7. Jipange na kuwa na matumizi mazuri ya muda wako.

Kama hujajipanga, yaani unafanya jambo pale tu unapojisikia, tabia ya kuahirisha mambo lazima itakuwa karibu na wewe. Ni muhimu kujipanga na kujua ni mambo gani unayotaka kufanya na pia kujua utayafanya wakati gani. Pia jua ni mambo gani ambayo unayafanya ila unaweza kumpa mtu mwingine na akayafanya vizuri kama unavyofanya wewe. Kuna baadhi ya mambo unayongangania kufanya kila siku yanakufanya uahirishe kufanya mambo ya msingi kwenye maisha yako.

8. Jihamasihe mwenyewe, au tafuta kitu cha kukuhamasisha.

Kuna wakati ambapo unaweza kujaribu mambo yote ya kukufanya uache kuahirisha mambo ila bado ukashindwa kuanza kufanya jambo. Katika wakati kama huu unahitaji hamasa ili kuweza kufanya kile unachotaka kufanya. Hamasa hii inaweza kutoka ndani yako mwenyewe au kutoka kwenye vyanzo vingine. Kupata hamasa ya ndani yako mwenyewe angalia ni mambo gani makubwa ambayo umewahi kufanikisha huko nyuma, pia jione kama mtu ambaye anajua kile anachofanya. Kama hamasa kutoka ndani haisaidii unaweza kutumia hamasa kutoka nje, angalia watu wengine ambao wameweza kufanikisha mambo makubwa lisha ya kuanzia chini kabisa, hii itakusukuma kuchukua hatua muhimu.

9. Tumia mpango wa dakika tano.

Siku zote kuanza jambo ni vigumu kuliko kuendeleza jambo. Unaweza kuona shida sana kuanz ajambo ila ukishalianza kuendelea inakuwa ni rahisi sana. Ili kuepuka ukinzani huu mkubwa kwenye kuanza jambo tumia mpango wa dakika tano. Katika mpango huu jiambie kwamba unakwenda kufanya jambo hili kwa dakika tano tu, baada ya hapo utaondoka na kufanya kile kinachokuvutia zaidi kufanya. Ukishaanza kufanya na dakika tano zikaisha jiambie tena utaendelea kwa dakika tano tu, na ukifanya hivi mara tano utajikuta unasahau kabisa kama dakika tano zimefika. Ukitumia njia hii kwa nidhamu hakuna kitakachokushinda kufanya.

10. Ungana na watu ambao wanaweza kukufuatilia.

Ni rahisi sana mtu kufanya kazi aliyopanngiwa na mwajiri wake hata kama haipendi kuliko kufanya jambo ambalo analipenda ila hakuna anayemsimamia. Sehemu kubwa ya watu wanahitaji usimamizi wa karibu ili kuweza kutekeleza majukumu yao. Ndio maana watu wengi wanaotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri wanajikuta kwenye matatizo makubwa sana. Ili kujiondoa kwenye matatizo haya ya kuahirisha mambo, tafuta mtu au watu ambao unaweza kuwa unaripoti kwao. Waambie watu hao ni kitu gani unataka kufanya na umepanga kukikamilisha baada ya muda gani. Kisha pangeni muda ambao utakuwa ukiwaeleza maendeleo yako katika mpango huo. Hii itakusukuma kutekeleza kile ulichopanga kufanya.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo unawezakuyatumia na ukaondokana na tabia ya kuahirisha mambo. Ni vitu rahisi sana ambavyo kila mmoja wetu anaweza kuvifanya. Kama utaahirisha hata kuvifanya vitu hivi basi wewe unaweza kusahau kuhusu mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.