Kama Unataka Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako, Acha Kuogopa Kufanya Mambo Haya.

Kuwa na mafanikio makubwa na unayoyataka katika maisha yako ni kitu cha muhimu sana. Na ili uwe na mafanikio hayo, kuna umuhimu mkubwa wa wewe kubadili namna unavyoishi sasa. Kama utaendelea kuishi maisha unayoishi hivi sasa na huku ukiwa unataka mafanikio makubwa yatokee kwako ni kitu ambacho hakitawezekana.

Ili uweze kusonga mbele na kufanikiwa, kuna vitu ambavyo utalazimika kuvibadili au kuachana navyo kabisa katika maisha yako. Kama hautachukua hatua ya kuachana na vitu hivi mapema uwe na uhakika utaendelea kuishi maisha yaleyale siku zote. Na kati ya mambo unayotakiwa kubadili na kuachana nayo ni kuacha kuogopa sana maisha.

Umefika wakati wa kutenda bila kuogopa chochote na achana na mambo yanayokukwamisha na kukuzuia kufikia kwenye kilele cha mafanikio. Maisha hayakusubiri wewe kama huchukui hatua mapema yanazidi kusonga mbele na miaka inakatika tu. Ukijichunguza kwa makini utagundua kuwa vipo vitu vingi ambavyo umekuwa ukiviogopa na vimekuwa kizuizi kikubwa cha wewe kufanikiwa.

Kumbuka dunia tuliyonayo sasa imesonga  mbele sana,  kwa nini ukubali  kusimama  palepale  ulipokuwa miaka  kumi nyuma.  Huna haja ya kuogopa na  kuamini tena  wengine  ndio  wanaoweza  kufanikiwa,  sasa ni  zamu  yako ya kuishi maisha ya mafanikio. Kama kweli unataka mafanikio makubwa katika maisha yako, acha kuogopa kufanya mambo haya tena:-

1. Acha kuogopa kujitoa mhanga.

Kama unataka ndoto zako zitimie na kufanikisha malengo makubwa unayoyataka ni lazima ujifunze kujitoa mhanga juu ya ndoto zako. Watu wengi huwa wanapenda mafanikio makubwa yawe kwao, lakini huwa hawajali suala hili sana la kujitoa mhanga. Bila kujitoa mhanga itakuwa ni ngumu sana kutimiza baadhi ya ndoto zako.

Kuna wakati katika kufanikisha malengo yetu kiuhalisia mambo huwa yanakuwa magumu na wengi hujikuta wakiacha ndoto zao zikipotea. Kitu pekee ambacho kitakuokoa na kukufanikisha ni kujitoa mhanga. Ni kweli unaona mambo  magumu sana, lakini hakuna kukata tamaa. Pigana mpaka tone la mwisho, jilipue kwenye ndoto zako, mwisho utafanikiwa .

Watu wengi wenye mafanikio makubwa duniani walijitoa kwenye ndoto zao hadi zikafanikiwa. Acha kuogopa kujitoa mhanga juu ya ndoto zako na kisikutishe kitu chochote unaweza. Kama ni shida ulizonazo ni za muda tu. Mbele yako yapo mafanikio makubwa sana usiyoyajua. Mafanikio hayo utayapata kama tu, kama utaamua kung’ang’ania ndoto zako bila kuacha.

2. Acha kuogopa kujiwekea malengo makubwa.

Haijalishi unaishi wapi, huna pesa au ni maskini kiasi gani lakini kitu muhimu unachotakiwa kuwa nacho ni lazima uwe na ndoto kubwa. Wapo watu ambao huwa wanaogopa kuwa na ndoto kubwa maishani mwao eti ni kwa sababu hawana pesa. Ni watu ambao wanasubiri wawe na pesa za kutosha ndio wawe na ndoto kubwa.

Kujiwekea malengo makubwa katika maisha yako ni kitu ambacho haulipii. Kama ndoto hazilipiwi ni nini kinachokuzuia kuota ndoto kubwa? Hata kama unalala darajani hauzuiliwi na mtu wala polisi hawataweza kukukamata eti kwa kuwaza kwamba, lazima siku moja uje umiliki Hotel kubwa kama Kilimanjaro Hotel. Kikubwa uwe na mipango na malengo utafika.

3. Acha kuogopa sana matatizo uliyopitia.

Inawezekana kabisa kuna sehemu uliumizwa katika maisha yako sasa unaogopa tena kusonga mbele. Kama upo katika hali hii isikukatishe tamaa, acha kuumia kwa sababu ya hasara pengine uliyoipata wala acha kusimama endeleza ndoto zako. Maumivu uliyonayo sasa hivi yasikuzuie kuendeleza ndoto zako hata kidogo.

Kumbuka maumivu ni sehemu ya kukua na sehemu ya kujifunza pia katika maisha yetu. Kama kuna sehemu ulikosea katika mradi wako acha ile tabia ya kitoto ya kuzira na kusema sitaki tena kusikia habari hiyo, unataka mafanikio makubwa katika maisha yako, acha kuogopa sana matatizo.( Unaweza ukasoma pia Vitu Muhimu Unavyotakiwa kukumbuka Wakati Mambo Yako Yanapokwenda Hovyo )

4. Acha kuogopa kuishi maisha ya mafanikio unayoyataka.

Asije akakuzuia mtu kwa kukuambia huwezi kufanikiwa kwa malengo uliyojiwekea. Wapo watu ambao katika maisha yetu huwa ni wepesi sana kukatisha tamaa wenzao. Kwa kulijua hilo ni muhimu sana kuwa nao makini, maana wasije wakakufanya ukaachana na ndoto zako na ukawa mtu wa kuogopa kuishi maisha ya mafanikio unayoyataka.

Jifunze kuishi kwa malengo uliyojiwekea, fuata ndoto zako na pia kuwa dereva wa maisha yako mwenyewe kwa kuishi maisha ya mafanikio unayoyataka. Achana  na watu watakao taka kukupangia maisha yako ya mafanikio. Kumbuka kila mtu hapa duniani amekuja na malengo yake, acha kuyumbushwa, simama imara na tekeleza mipango yako kikamilifu.

5. Acha kuogopa kufanya mabadiliko.

Kati ya vitu vigumu katika maisha ya mwanadamu ni kufanya mabadiliko. Hata kama ipo wazi kabisa kwamba mabadiliko hayo yataleta faida kwake bado pia huwa ni ngumu kubadilika. Hii yote inaonyesha ni jinsi gani sisi tukiwa kama binadamu, ni tulivyokuwa wagumu kubadilika.

Kwa hiyo hapo utaona kabisa kufanya mabadiliko katika maisha yako inahitajika ujasiri, ili uweze kushinda hilo na kufanikiwa kusonga mbele. Kama nilivosema wakati naanza makala hii ni lazima kubadili baadhi ya tabia zetu mbaya ili tufanikiwe. Acha kuziogopa kuzifanyia mabadiliko tabia zinazokukwamisha kufanikiwa.

6. Acha kuogopa kujifunza kutokana na makosa.

Ni kweli kuna sehemu umekosea katika maisha yako, lakini kila unapokumbuka inakuuma sana na mpaka unashindwa kujifunza kutokana na makosa uliyoyafanya. Ninachotaka kukwambia acha kuogopa kujifunza kutokana na makosa ambayo yameshafanyika na isitoshe yamepita.

Chukua hatua muhimu ya kusonga mbele. Tambua nini kilichopelekea wewe ukashindwa kwa kile ulichoshindwa sasa. Baada ya hapo kaa chini, tafuta suluhu itakayokutoa hapo badala ya kukaa chini na kuanza kulalamika na kulaumu bila sababu. Kumbuka hili siku zote watu wa AMKA MTANZANIA huwa htulalamiki wala hatuogopi kitu nawe naomba uvae ujasiri huo.

Kama unataka kufikia viwango vya juu vya mafanikio unayoyataka, jifunze kutoyaogopa mambo hayo katika maisha yako, hii itakusidia sana kusonga mbele.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA NA KISIMA CHA MAARIFA kwa kujifunza mambo mazuri yatakayobadili maisha yako.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO  kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

IMANI NGWANGWALU


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: