Habari za leo mpenzi msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA, karibu kwenye kipengele hiki cha uchambuzi wa vitabu ambapo tunapata nafasi ya kujifunza mambo mazuri yanayopatikana kwenye vitabu mbalimbali.
Kwa mwaka jana tulifanikiwa kufanya uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD na uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON. Katika vitabu hivi viwili tulijifunza mambo mengi sana kuhusiana na kazi, biashara, na hata fedha.
Ni matumaini yangu kwmaba umeweza kuyatumia yale uliyojifunza na umeanza kuona mabadiliko makubw akwenye maisha yako. Kama bado hujaanza kuyatumia unasubiri nini sasa? Muda wenyewe ndio sasa, huu ndio muda bora kwako wa kuboresha maisha yako.
Sasa tunafungua mwaka na kitabu kingine ambacho ni THINK AND GROW RICH kilichoandikwa na Napoleon Hill mwaka 1935. Kwa kifupi kitabu hiki kinaelezea ni jinsi gani mafanikio na utajiri vinatokana na mawazo yetu wenyewe. Mwandishi alifanya utafiti kwa miaka 25 kwa kuwahoji watu waliofanikiwa na walioshindwa na aligundua kwamba watu waliofanikiwa wana tabia zinazofanana na sehemu kubwa ya mafanikio yao inatokana na wanavyofikiri.
Utangulizi.
Mwandishi wa kitabu hiki, Napeleon Hill, alipata nafasi ya kuzungumza na mmoja wa watu matajiri wa kipindi hiko Andrew Carnegie. Andrew alimpa changamoto ya kuwafuatilia watu matajiri kwa kipindi cha muda usiopungua miaka 12 ili ajifunze tabia zao na kuwafundisha wale ambao hawana muda w akufuatilia na kujua watu waliofanikiwa wanafanyaje mambo yao.
Andrew alikuwa na kanuni yake ya maajabu ambayo ilimpatia mafanikio makubwa sana. Na alitamani kanuni hiyo ifundishwe kwenye mfumo wa elimu kwani ingeweza kupunguza muda wa elimu hadi kufikia nusu ya muda mtu anaotumia. Aliweza kutumia kanuni hiyo kwa watu ambao wana elimu kidogo sana ila wakaweza kufikia mafanikio makubwa. Kwa uzoefu huo, Andrew alikubali kwamba mengi yanayofundishwa shuleni hayana uhusiano wa karibu na kufanikiwa kwenye maisha.
Utajifunza kanuni hiyo kwenye uchambuzi huu na kama unajua kile kweli unachokitaka kwenye maisha yako hapa utapata mbinu ya kuweza kukifikia. Kanuni hii imetumiaka na watu wengi sana na wameweza kufikia mafanikio makubwa. Hiki ni moja ya vitabu ambavyo vimeuzwa sana duniani na kimeweza kutengeneza watu wengi waliofanikiwa.
Japokuwa kanuni hii haijaelezwa wazi wazi, hivyo kwa wale wanaojua ni nini wanataka ndio wanaweza kuigundua kanuni hii na kuitumia.
Ili uweze kupata unachotaka kuna gharama utahitajika kulipa, hakuna kitu cha bure. Hivyo ili uweze kutumia kanuni hiyo itakayobadili maisha yako kuna gharama itabidi ukubali kutoa.
Kabla hujaanza kujifunza kupitia kitabu hiki kumbuka kwamba MAFANIKIO YOTE YANAANZA NA WAZO.
Tukutane kwenye makala ijayo kwa kuanza uchambuzi wa kitabu hiki.
TUPO PAMOJA.