Hatua ya kwanza kabisa ya kuelekea kwenye mafanikio ni kuwa na hamu au shauku kubwa sana ya kufanikiwa. Katika hadithi ya Edwin tuliyoona kwenye uchambuzi uliopita, kilichomfanya akamtafute Edson ni hamu yake kubwa ya kutaka kufanikiwa. Hakukubali kurudishwa nyuma na kikwazo chochote.

Edwin alikuwa na hamu kubwa sana ya kufanikiwa, hayakuwa matumaini, haikuwa mategemeo tu bali ilikuwa hamu ambayo haikuweza kuzuiwa na kitu kingine chochote. Na hamu yake hii kubwa ilimwezesha kupata nafasi ya kufanya biashara na Edson japo hakuwa na chochote cha kuanzia.

Edwin aliweza kufanikiwa kwa sababu alikuwa na lengo kubwa ambalo aliwekeza nguvu zake zote, uwezo wake wote, akili yake yote, juhudi zake zote na kila kitu alichokuwa nacho mpaka alipoweza kufanikiwa. Hakufanikiwa lengo lake mara moja, ilimchukua muda, ilibidi afanye kazi za hovyo, lakini yote hayo hayakumkatisha tamaa. Aliendelea kupigania ndoto yake mpaka ilipotimia. Alifanya kazi kwa Edison kwa zaidi ya miaka mitano bila ya kuona dalili zozote za kupata nafasi ya kuwa mshirika wa Edison, lakini hii haikumfanya asahau au kuacha lengo lake kuu. Japokuwa watu wengine walimuona kama mfanyakazi wa chini sana kwenye maabara ya Edison, yeye mwenyewe alijiona kama mshirika wa Edison tokea siku ya kwanza anafika pale.

Hapa tunaona ni jinsi gani nguvu ya hamu na shauku kubwa inavyoweza kuleta mabadiliko makubwa. Edwin alikwenda pale akiwa tayari anajiona ni msirika wa Edison, hakwenda pale kuona kama Edison atakubali awe mshirika wake na wala hakwenda pale kujaribu kumchawishi Edson awe mshirika wake, alikwenda pale kwa lengo moja tu ambalo lilikuwa wazi kabisa, KUWA MSHIRIKA WA BIASHARA WA EDISON. Na aliweza kufikia lengo lake.

CHOMA MADARAJA.

Moja ya kitu kinachoweza kumfanya mtu awe na shauku kubwa ya kufanikiwa ni kuchoma madaraja yanayoweza kumhakikishia usalama.

Zamani kidogo kulikuwa na kiongozi mmoja wa kivita mbaye alikuwa anaenda kupigana vita na kisiwa kingine. Majeshi na nguvu za wapinzani wake zilikuwa kubwa sana kushinda za kwake. Bwana yule alichukua wanajeshi wake wote wakapanda boti kuelekea kwenye kisiwa. Walipofika kwenye kisiwa kile aliagiza maboti yote yaliyowaleta yachomwe moto. Baada ya hapo aliwahutubia wanajeshi wake na kuwaambia mnaona maboti yanaungua moto kule, hii ina maana hatuwezi kukimbia vita hii, ni lazima tupigane tushinde au tushindwe na tuuwawe wote. Wanajeshi wale walipigana kwa shauku kubwa na walishinda vita ile.

Mtu yeyote anayetaka kushinda jambo lolote linalomrudisha nyuma au kufikia mafanikio makubwa lazima awe tayari kuchoma madaraja yanayomhakikishia usalama hata kama aklishindwa. Kwa mfano kwenye hadithi ya boti hapo juu, kama boti zile zingekuwepo wanajeshi wangepigana wakijua kwamba hata wakishindwa wataingia kwenye maboti yao na kukimbia. Ila kwa kuwa walijua hakuna njia yoyote ya kuondoka pale ila kushinda, walipigana kw anguvu zao zote na hatimaye wakashinda.

Kila binadamu aliyefikia umri wa kuelewa fedha, anatamani kupata fedha. Lakini kutamani hakuwezi kukuletea utajiri. Kuwa na hamu kubwa ya kuwa tajiri na kufanya hili kuwa lengo lako kubwa kw akuliwekea mipango na kutokata tamaa kutakuletea utajiri.

Hatua sita za kufikia utajiri.

Kuna hatua sita ambapo hamu au shauku ya utajiri inaweza kukuletea utajiri wa kweli. Hatua hizo ni;

1. Amua ni kiasi gani cha fedha unachotaka. Ni lazima uamue namba na uiandike, kuna sababu za kisaikolojia ambazo tutajifunza kwenye uchambuzi mbeleni.

2. Amua ni kitu gani upo tayari kulipa ili kupata kiasi hiko cha fedha. Kumbuka hakuna kitu cha bure.

3. Amua tarehe ambayo unataka uwe umeshafikisha kiwango hiko. Ni muhimu sana, usipokuwa na tarehe ya mwisho unaweza usifikie.

4. Tengeneza mpango wa wewe kuweza kufikia lengo lako hilo kubwa. Na anza kutekeleza lengo hilo mara moja iwe uko tayari au la, anza kutekeleza hatua moja baada ya nyingine.

5. Andika kwa usahihi na kueleweka maelezo mafupi yanayotaja kiasi cha fedha unachotaka, muda unaotaka kukipata, eleza kile ulichotayari kutoa ili kupata fedha hizo na eleza mpango utakaotumia kupata fedha hiyo.

6. Soma maelezo hayo uliyoandika hapo juu kwa sauti mara mbili kila siku. soma asubuhi na mapema unapoamka na soma usiku kabla ya kulala. WAKATI UNASOMA TENGENEZA PICHA KWENYE AKILI YAKO KAMA TAYARI UMESHAZIPATA FEDHA HIZO.

Ni muhimu sana kufuata hatua hizo sita kama zilivyoelezwa hapo. Maelezo utakayoyasoma kila siku yatakujengea hamu kubwa ya kupambana ili kufikia kiwango hiko unachotaka. Na unaposoma soma kwa sauti, kuna sababu ya kisaikolojia ambayo itakufanya kuchukua hatua kwa kasi zaidi. Pia unaposoma maelezo haya kila siku yanakufungua macho yako na kuanza kuziona fursa za kukuongeze akipato chako mpaka kifikie pale unapotaka. Tutajifunza hili kwenye chambuzi zinazokuja.

Kwa leo fanya zoezi hili muhimu ili upate maelezo utakayokuwa unayasoma kila siku.

Tutaendelea na sehemu ya pili ya uchambuzi huu kwenye makala ijayo.

Tafadhali tushirikishe kwenye maoni hapo chini vitu vitano ulivyojifunza kwenye uchambuzi huu. Fanya hivyo, itakusaidia sana kuchukua hatua, maana wengi hawafanyi hivi na inawagharimu kwa kukosa somo muhimu ambalo watatoka na kwenda kulifanyia kazi.

Tafadhali leo tushirikishe mambo matato uliyojifunza hapa.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.