Karibu kwenye sehemu hii ya uchambuzi wa vitabu na sasa tunachambua kitabu THINK AND GROW RICH. Katika sehemu iliyopita ya uchambuzi tuliona hatua sita za kufikia lengo lolote la kifedha au utajiri unaotaka. Naamini umeshatengeneza hatua zile, kama bado tafadhali rudia tena kusoma makala ile na utengeneze maelezo mafupi kwa kupitia hatua zile sita. Unaweza kuisoma makala ile kwa kubonyeza maandishi haya.

Kama tulivyoona kwenye sehemu ya uchambuzi iliyopita, kuwa na hamu kubwa na shauku ya kufikia mafanikio ni hitaji la msingi sana katika kufikia mafanikio.

Huwezi kuwa tajiri kama hutakuwa na hamu na shauku kubwa ya kupata fedha na pia kuamini kwamba utapata utajiri huo. Kama huwezi kujiona ukiwa tajiri kwenye ndoto zako huwezi kufikia utajiri. Sasa hivi tunaishi kwenye ulimwengu uliobadilika sana ambapo mtu yeyote anaweza kuanzia chini sana na akafanya juhudi na kufikia mafanikio makubwa sana.

Wale wote ambao tupo kwenye mbio za kufikia utajiri tunatakiwa kujua kwamba dunia ya sasa inahitaji mawazo mapya, njia mpya za kufanya mambo, viongozi wapya, ugunduzi mpya, njia mpya za kufundisha, njia mpya za kufanya biashara, vitabu vipya, vipindi vipya vya redio, na hata njia mpya za burudani. Katika mahitaji yote haya mapya, kuna sifa moja ambayo mtu anapaswa kuwa nayo ili aweze kutumia fursa hii vizuri. Mtu anatakiwa kujua NI NINI HASA ANATAKA na awe na HAMU NA SHAUKU kubwa ya kupata kile anachotaka. Dunia inahitaji watu wanaoweza kuota ndoto kubwa na kuzifanyia kazi ndoto hizo ili ziweze kuwa kweli.

Uvumilivu na kuwa na mawazo chanya ndio hitaji kubwa la kuweza kuwa na ndoto kubwa. Wale wanaoogopa mawazo mapya wameshashindwa kabla hata ya kuanza. Wale wote wanaodhubutu kuota ndoto kubwa na kuzifanyia kazi wamefanikiwa sana. Kila kitu tunachokiona leo, kuanzia majengo marefu ya gorofa, usafiri wa angani, majini, ardhini, teknolojia mpya, havikuanza mara moja. Bali ni watu walikuwa na ndoto ya kuleta mabadiliko, wakaifanyia kazi na sasa tunafaidi matunda yake.

Hata wewe kama utakuwa tayari kutengeneza mawazo ambayo yataboresha maisha ya wengine una nafasi kubwa sana ya kupata mafanikio.

MAFANIKIO HAYAHITAJI KUJITETEA, KUSHINDWA HAKURUHUSU VISINGIZIO.

Kama kitu unachotaka kufanya ni sahihi na unaamini unaweza kukifanya anza kukifanya. Weka kila ulichonacho na usisikilize wengine wanasema nini pale unapokutana na changamoto, kumbuka kila changamoto, kila kushindwa kunakuja na mbegu ya mafanikio.

Henry Ford(tajiri wa enzi hizo marekani) kijana aliyekuwa masikini na aliyekosa elimu, alipata ndoto ya usafiri usio wa kutumia farasi. Alianza kufanyia ndoto yake kazi kwa kutumia vifaa alivyokuwa navyo na hakusikiliza wengine wanafanya nini wala kukata tamaa. Aliweza kufanikiwa sana na kuwa mmiliki wa kiwanda kikubwa sana cha magari.

Thomas Edison, aliota kuwepo kwa taa inayotumia umeme, alianza kuifanyia ndoto yake kazi. Japokuwa alishindwa zaidi ya mara elfu kumi hakukata tamaa na matokeo yake leo hii kila mtu anafurahia taa ya umeme. Watu wanaofanyia kazi ndoto zao na kufanikiwa HUWA HAWAKATI TAMAA.

Watu wote waliofanikiwa kwenye maisha wameanzia sehemu ngumu sana, wameshindwa na kukatishwa tamaa ila wao waliendelea kung’ang’ania. Ni katika nyakati ngumu sana za maisha yao ndipo walipoweza kufanya mabadiliko kwenye maisha yao na kuona mafanikio makubwa. Kwa sababu mambo yanapokuwa magumu kweli ndio unatambulishwa kwa nafsi yako nyingine.(tutajifunza kuhusu nafsi hii nyingine baadae)

Watu wengi waliofanikiwa walianza kuona mabadiliko katika nyakati ambazo ni ngumu sana kwenye maisha yao. Hapa ndipo wlaipopata fursa ya kutumia kila uwezo walionao na hivyo kujikuta wakitumia uwezo mkubwa ulio ndani yao. Kupitia hadithi za mafanikio za watu wengi utakubali kwamba hakuna mtu aliyeshindwa bali yule aliyekubali kushindwa yeye mwenyewe.

Kabla ya kumaliza hatua hii ya kwanza ya kuelekea kwenye mafanikio, fungua akili yako sasa kwa moto wa matumaini, ujasiri na uvumilivu. Kwa kuwa na sifa hizo tatu na kama umeelewa dhana ya kuwa na hamu na shauku kubwa ya mafanikio basi hakuna chochote ambacho kitakushinda.

Kuna tofauti kati ya KUTAMANI kuw ana kitu na KUWA TAYARI KUPOKEA KITU HIKO. Hakuna aliye tayari kupokea chochote mpaka pale atakapoamini anaweza kukipata.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.