Kama ilivyo kwenye jambo lolote kwenye maisha, watu wanaoingia kwenye ujasiriamali kwa mara ya kwanza huwa wanafanya makosa mengi sana. Kwa wale wanaogundua makosa haya na kuyatumia vizuri wanaweza kufanikiwa sana. Ila wale wanaoshindwa kujifunza kupitia makosa yao huishia kushindwa na kukata tamaa kabisa.

Kama unataka kuingia kwenye ujasiriamali ni vyema kujifunz amakosa wanayofanya wengine ili uokoe muda ambao ungeupotez akwa kufanya makosa haya mwenyewe. Kama tayari upo kwenye ujasiriamali bado kuna mambo mengi unaweza kujifunza hapa ili kuwa bora zaidi na kuwezakufikia mafanikio kwa kile unachofanya.

Yafuatayo ni makosa sita yanayofanywa na wajasiriamali wengi wageni;

1. Kutokufanya utafiti wa kutosha kwenye soko.

Utafiti ni nguzo muhimu ya kujua kama biashara yako inaweza kufanikiwa.  Tumia muda wako kufanya utafiti wa kutosha kuhusu soko lako, wajue wateja wako, jua kile wanachotaka na jua ni jinsi gani unavyoweza kuwafikia. Kufanya utafiti vizuri kutakusaidia kujua kama wazo lako la biashara linaweza kufanyika na kujua muundo wa biashara utakaotumia kabla hata ya kuingia sokoni.

2. Kutokuweka thamani kubwa kwenye bidhaa au huduma.

Baadhi ya wajasiriamali wageni hufikiri njia nzuri ya kuteka soko ni kutoa bidhaa au huduma za bei rahisi. Au kupunguza bei pale ambapo wanaona hawapati wateja. Hii ni kushindwa kutengeneza thamani kwenye bidhaa au huduma wanayotoa. Na pale mtu unapopunguza bei sana baadhi ya wateja wataogopa kununua bishaa au huduma yako kwa kuhofia inaweza kuwa ya ubora wa hali ya chini sana. Panga thamani ya bidhaa au huduma yako na kisha washawishi watu kwamba thamani hiyo ni kubwa kwa bei unayotoa. Kama ni kutoa punguzo unaweza kutoa ila sio kwa muda mrefu.

3. Kufikiria kila mtu atakuwamteja wako.

Wajasiriamali wengi wageni hufikiri kwamba biashara waliyokuja nayo kila mtu anaweza kuwamteja na hata kwenye kutafuta wateja wanatafuta kila mtu. Ukweli ni kwamba hakuna bidhaa au huduma inayoweza kutumiwa na kila mtu. Hata kama ni ya bei rahisi kiasi gani au ni ya muhimu kiasi gani bado kuna watu hawataihitaji. Hivyo badala ya kutumia gharama na muda mwingi kumfikia kila mtu tafuta aina ya wateja ambao unajua bidhaa au huduma yako itawafaa kisha fanya nao biashara.

4. Kutokuwa mvumilivu.

Moja ya hitaji kubwa sana la kuwa mjasiriamali ni kuwa na uvumilivu. Unahitaji kuwa na uvumilivu wa kuendelea kufanya utafiti, kuendelea kuboresha wazo lako la biashara na kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ndio uweze kufikia mafanikio. Hutaanza biashara leo halafu kesho uwe umeshapata faida kubwa, hizi ni ndoto za mchana.

5. Kutokufanya vitu vinavyoleta fedha.

Wajasiriamali wengi wageni hujikuta wakifurahia kupanga na kubadili biashara yao kila siku. Mara kwa mara hujikuta wakifikiria njia za kuboresha biashara zao. Japokuwa hiki ni kitu kizuri lakini kwa bahati mbaya sio kitu ambacho kitakuletea fedha kwa sasa. Unahitaji kuelekeza nguvu zako nyingi kufanya vitu ambavyo vinaleta fedha ili biashara iweze kuendelea kuishi. Unahitaji kuwa unaongea na wateja, kutoa bidhaa au huduma na majukumu mengine ambayo yanazalisha fedha.

6. Kutumia fedha kwenye maeneo ambayo sio sahihi.

Wajasiriamali wengi wageni hujikuta wakitumia fedha nyingi mwanzoni kwenye maeneo ambayo sio muhimu sana. Wengi hujikuta wakitumia fedha nyingi kutangaza biashara zao kwa njia mbalimbali ambazo hazinauhakika wa kuleta wateja. Wengine hutumia fedha nyingi kununua vifaa ambavyo havihusiani na uzalishaji au utoaji wa huduma au bidhaa za biashara yao. Ni muhimu kuelewa maeneo muhimu ya kutumia fedha zako ili kuhakikisha ukuaji wa biashara. Hayo mengine ambayo sio muhimu kwa sasa unaweza kuyafanya baadae.

NA KOSA KUBWA KULIKO YOTE AMBALO LINAFANYWA NA WENGI NI…. KUTOKUANZA.

Kuna watu wengi ambao wamekuwa kila mwaka wanasema wanataka kuwa wajasiriamali. Lakini wanaishaia kuweka mipango na hawachukui hatua. Hili ni kosa kubwa sana. Kama kweli unataka kuwa mjasiriamali anza sasa, anza kidogo na weka mipango ya kukua kuanzia hapo. Kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu 2015… JUST DO IT.

Unaendelea kusubiri nini? Na kama tayari ni changamoto zipi ambazo zinakusumbua kwenye ujasiriamali? Tushirikishane kwenye maoni hapo chini.