Mwaka 2015 bado ni mchanga kabisa, na hivyo hata kama unajiona umechelewa bado una nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko kwenye maisha yako katika mwaka huu wa kipekee. Hatua ya kwanza kabisa ambayo kwa mtu makini kama wewe(wasomaji wote wa AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA ni watu makini) utakuwa umeshaifanya ni kuweka malengo na mipango. Kama kwa njia yoyote ile ulipitiwa na kusahau kuweka malengo yako ya mwaka huu 2015, usiendelee kusoma makala hii kwanza, chukua kalamu na kijitabu chako na andika malengo unayotaka kufikia mwaka huu, mika mitano iyajo na hata miaka kumi ijayo. Ukishamaliza kuandika malengo hayo na kuyawekea mipango, rudi hapa uje umalizie kiungo hiki muhimu cha kukuwezesha kuufanya mwaka 2015 kuwa mwaka ambao utaangalia nyuma na kusema mwaka ule ndio maisha yangu yalibadilika kabisa.

Kuwa na malengo ni hatua muhimu sana kufikia mafanikio kwenye maisha yako. Ila kuandika tu malengo hakutakufanya uyafikie, tena malengo haya hutayafikia kwa siku moja tu. Bali utafanya mambo madogo madogo kila siku na ukiyajumlisha yote ndio unapata mafanikio makubwa. Kwa maana hii basi unahitaji kujijengea tabia nzuri utakazokuwa unazifanya kila siku ili zikusukume kufikia malengo yako.

SOMA; Wajasiriamali Wenye Mafanikio Hufanya Mambo Haya Matano Kila Siku.

Leo hapa tutajadili tabia kumi unazotakiwa kuwa unazifanya kila siku na tafadhali sana anza kuzifanya leo. Kama umekuwepo kwenye KISIMA CHA MAARIFA kwa muda mrefu utaona tabia nyingi hapa tumeshazijadili katika kipengele cha kujijengea tabia za mafanikio. Jifunze tabia hizi na anza kuzifanyia kazi leo hii, na sio kusubiri kesho, maana wote tunajua kwamba kesho ni vigumu sana kufika.

1. Amka asubuhi na mapema.

Hii ni tabia muhimu sana ya kufanya kila siku. Kila siku hakikisha unaamka mapema kabla ya watu wengine kuamka. Kwa kuamka mapema unapata faida ya kuwa mbele ya wengine, maana wakati wengine wamelala wewe tayari umeshaianza siku yako. Pia unapata wakati mzuri ambao hauna kelele na akili yako imepumzika vya kutosha hivyo unaweza kufikiri vizuri bila ya kusumbuliwa. Tumia muda huu wa asubuhi kupitia malengo na mipango yako na hata kufanya baadhi ya kazi zako muhimu. Pia utatumia muda huu kufanya tabia nyingine ambayo tutaijadili hapo chini.

2. Soma.

Ni muhimu sana kusoma kila siku. Usidhubutu kukubali siku yako ipite bila ya kupata muda w akujisomea, hata kama ni muda wa nusu saa. Kwenye siku ya masaa 24 kama utakosa nusu saa tu ya kujisomea haupo makini na maisha yako. Unapojisomea unajiongeze amaarifa, unachokoza akili yako ifikiri zaidi naunalisha akili yako mawazo chanya ambayo yatakusaidia kufikia malengo yako na mafanikio makubwa.

3. Fanya mazoezi.

Mazoezi ni muhimu sana kwa ufanisi mzuri wa mwili wako. Pata muda w akufanya mazoezi kila siku kwenye maisha yako. Sio lazima yawe mazoezi magumu, bali mazoezi yoyote yatakayokufanya uchangamshe mwili wako. unapofanya mazoezi, mwili wako unatoa kemikali inaitwa endorphins, hii ina nguvu kubwa kuliko madawa ya kulevya aina ya morphin na inakufanya ujisikie vizuri na kuwa na furaha na pia kuweza kufanya kazi kwa mud amrefu bila ya kuchoka.Kama ukiweza kufanya mazoezi kila siku asubuhi basi unakuwa na siku yenye ufanisi mkubwa sana.

4. Shukuru.

Kila siku pata muda wa kushukuru kwa maisha ambayo unayo. Hata kama maisha yako hayajafikia viwango unavyotaka, shukuru kwamba umeweza kujitambua na sasa unafanyia kazi kuboresha maisha yako. Shukuru kwamba una afya njema na unaweza kufanyia kazi amlengo yako. Shukuru kwamba unazungukwa na watu wanaokupenda. Na pia mshukuru kila mtu anayefanya jambo jema kwako. Kwa njia hii utashangaa kuona unapata zaidi na zaidi. Ila ukiwa mtu wa kulalamika tu, utaendelea kupata yale unayolalamikia.

5. Ipangilie siku yako kabla ya kuianza.

Kama unataka kuwa na ufanisi mkubw akwenye siku yako, hakikisha unaipangilia kabla ya siku yenyewe kuanza. Kila siku jioni andika mambo matatu muhimu ambayo unataka kuyafanya kwenye siku inayofuatia. Unapoandika mambo hayo na kulala, akili yako inayafanyia kazi na utakapoamka utaona ni rahisi sana kwako kujua unaanzia wapi. Lakini kama utaendelea kwenda na siku bila ya mipango utashangaa unafanya chochote kinachotokea mbele yako na kw anjia hiyo huwezi kufikia mafanikio.

6. Fanyia kazi vipaumbele vyako.

Kuna vitu vingi sana unavyoweza kufanya kila siku, lakini sio vitu vyote unavyotaka kufanya ni muhimu kwako hasa kwenye kufikia malengo yako na mafanikio kwa ujumla. Weka vipaumbele vyako na kila siku anza kwa kufanyia kazi vipaumbele vyako. Usikubali kushawishika kuanza kufanyia kazi mambo mengine wakati yale muhimu kwako bado hujayakamilisha. Vitu vingine unavyotamani kufanya utavifanya baada ya kukamilisha yale ya kipaumbele kwako. Fanya hivi kila siku na utashangaa kuona maisha yako yanabadilika sana.

7. Fanya tathmini ya siku yako.

Kila siku jioni kabla ya kulala chukua dakika chache na ufanye tathmini kwa siku yako. Angalia siku yako nzima ilikwendaje. Andika ni mambo gani makubwa uliyoweza kufanya na kufanikiwa. Pia andika ni mambo gani uliyoshindwa kuyakamilisha. Pia tumia muda huo kuangalia kama kweli uliweza kutumia muda wako vizuri na hata fursa zilizojitokeza mbele yako. Kwa kufanya hivi kila siku itakufanya uweze kujirekebisha mapema hasa pale mambo yanapokwenda vibaya.

8. Kila mara nenda hatua ya ziada.

Kila siku fanya kitu cha ziada ukilinganisha na ulichotegemewa kufanya. Kama ni kazi, fanya jukumu la ziada au fanya kitu kwa ubora zaidi ya ulivyofanya jana. Kama unafanya biashara, fanya kitu cha ziada tofauti na mteja alivyotegemea. Kwa kuwa na mtazamo huu wa kufanya kitu cha ziada kila siku utajiona unakuw abora zaidi kadiri siku zinavyokwenda.

9. Boresha eneo moja la maisha yako kila siku.

Kila siku weka mpango wa kuboresha eneo moja kwenye maisha yako. Weka mpango w akufanya kitu ambacho kitafanya eneo hilo kuwa bora zaidi. Inaweza kuwa kuboresha mahusiano yako na mwenzi wako na hivyo kumfanyia kitu cha kumfanya aone unajali. Inaweza kuwakuboresha ufanyaji kazi wako na hivyo kujifunza mbinu bora zaidi. Chohote kile unachotaka kiwe bora kwenye maisha yako, kila siku fanyia kazi maeneo hayo.

10. Ishi wakati uliopo.

Kila siku jitahidi sana kuishi kwenye wakati uliopo, furahia maisha uliyonayo sasa na furahia kazi au biashara unayofanya. Utashawishika kufikiria jana na makosa yaliyopita, ila hayo yamepita na huwezi kubadili chochote. Utashawishika kuhofu kuhusu kesho na siku zijazo, ila hizo bado hazijafika na kuhofu kwako hakutosaidia lolote. Ishi leo jifunze kwa yaliyopita, jiandae kwa yajayo, ila furahia wakati ulionao leo.

Hizo ndio tabia kumi za kufanya kila siku, KILA SIKU, kwa mwaka huu 2015 ili uweze kuleta mabadiliko makuwba kwenye maisha yako na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kama umesoma vizuri tabia hizo utakuwa umeona kwamba hakuna tabia ambayo inahitaji uwe unatokea kwenye familia za kitajiri, au uwe na digrii au uende ukakope hela ndio uweze kufanya tabia hiyo. Hizi ni tabia ambazo unaamua mwenyewe kuanza kuzifanya hapo ulipo na unaanza kubadili maisha yako. Kama kweli unataka kubadili masiah yako anza kufanya tabia hizo leo, kama utasema unazifanya kesho naomba nikupe kwaheri, maan hutozifanya.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA, KAMA KWELI UTAFANYA HAYO ULIYOJIFUNZA.